Waziri Mkuu huyo wa zamani, Edward Lowassa jana aliteka nyoyo za wakazi wa Ruvuma na mikoa jilani baada ya kuingia katika Uwanja wa Majimaji na kushangiliwa kwa nguvu na umati mkubwa wa makada wa CCM hali ambayo ilimfanya muda wote Lowassa atabasamu mapokezi hayo.
Tukio la kushangiliwa kwa Lowassa katika sherehe hizo lilianzia katika uwanja wa ndege wa mjini Songea wakati alipowasili huku makada mbalimbali wa chama na Serikali wakiwa na hamu kubwa ya kumuona na kupeana nao mikono.
Kushangiliwa kwa Lowassa kulikuwa tofauti na viongozi wengine wa chama hicho waliotangulia katika uwanja wa sherehe hizo kwa vile yeye alishangiliwa kwa muda mrefu huku muda wote yeye akiwa anawapungua mikono wananchi kushoto na kulia mwa uwanja.
Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli aliingia Uwanjani Majira ya Saa 5:15 asubuhi na kupanda jukwaani na kukaa viti vya nyuma akiwasubiri kuwapokea viongozi waandamizi wa Chama na Serikali ambao walihudhulia maadhimisho hayo
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa mjini hapa wameelezea kitendo hicho kuwa ni ujumbe maalumu unaotumwa kwa Viongozi waandamizi wa chama na serikali kuhusu chagua la wanachama wengi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwani chama kinatakiwa kumtendea haki Lowassa
Denis Mpagaze Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Askofu James Songea (Ajuco) akizungumzia kitendo cha lowassa kushangiliwa huko alisema kuwa Lowassa anapendwa na makundi yote katika jamii, hivyo kitendo hicho kinaleta ujumbe wa kuufikiria sana katika vikao vya juu vya chama chake
Mpagaze alisema kuwa sauti za watu wengi ni sauti ya mungu na ishara zake zinaonekana kila kukicha miongoni mwa jamii kuhusu mwenendo wa kisiasa wa Lowassa ndani na nje ya chama na serikali hivyo ili uchaguzi huo ndani ya chama uwe mzuri ni lazima chama kimpitishe Lowassa
Alisema kuwa ndani ya Chama hakuna mwenye nguvu kubwa ya kiushawishi kama Lowassa hivyo kitendo cha kumuhujumu kitaleta mpasuko na kuifanya nchi iyumbe kutokana na makundi mbalimbali ya chama kuwa upande wake hivyo wanaweza wakaamua chochote kwa maslahi yao
“Ukikutana na makada wengi wa chama na viongozi mbalimbali waaandamizi wa serikali utasikia wanavyomzungumzia huyo bwana ,sasa ukitafakari kwa kina utabaini kuwa nguvu aliyonayo ni kubwa na kitendo cha kuizuia kinaweza kuleta mpasuko mkubwa miongoni mwa makundi hayo”alisema Mpagaze
Lowassa ambaye ndiye waziri Mkuu pekee wa zamani ambaye amehudhulia maadhimisho hayo alionekana kuwa na mvuto mkubwa kwa watu kitu ambacho kwa madai ya makada wengi walisema ndicho kilichomfanya akae nyuma kabisa kuhofia kuharibu protoko za sherehe hizo
Duru za Kisiasa zinasema kuwa Kitendo cha Lowassa kushangiliwa kuliko viongozi wa chama na Makada waliotanga nia ndiko kulikomfanya Rais Kikwete ashindwe kumtambulisha kwa madai kuwa muda hautoshi kumbe anahofu ya kumtaja angeweza kuzua shangwe tena na kuonekana kuwa anamfanyia kampeni
Katika Maadhimisho hayo Makada waliotangaza nia ya kuutaka urais walikuwepo ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernad Membe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Stephen Wassira, Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi Mwigulu Nchemba na Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa
Imeelezwa kuwa kitendo cha Makada hao kutowatambulisha katika maadhimisho hayo kimewafanya wakose kushangiliwa na kuwa kivutio katika maadhimisho hayo na kuwagawa wanachama kifikra hali iliyoendelea kumn’garisha Lowassa katika harakati zake za kisiasa kwani makada wengi walikwenda kumpokea uwanja wa ndege na hata alipofika uwanjani alishangiliwa kuliko makada wenzake
Wakizungumza na Gazeti hili baadhi ya Makada wa Chama hicho ambao hawakutaka kutaja majina yao walisema kuwa Chama kinatakiwa kutenda haki ya kuwaruhusu watu wanaopenda kugombea nafasi mbalimbali za uongozi watangaze nia zao ili wanachama na wananchi wawajue mapema kabla ya uchaguzi
Walisema kuwa sio dhambi kwa mtu kujitokeza na kutaka nafasi ya uongozi na hasa ya Urais bali chama kinachotakiwa ni kusimamia maadili ya chama ili yafuatwe kwa wagombea ili wasiende kinyume na miiko na maadili ya chama.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete akiwahutubia Maelfu ya wanachama na mashabiki wa chama hicho waliohudhulia maadhimisho hayo alisema anaamini CCM ni chama kinachofuata taratibu za kuwapata viongozi wake bora kwa kutumia vikao vyake rasmi vinavyowateua ambavyo hukaa Dodoma.
Rais Kikwete alisema taratibu na kanuni za chama hicho kumpata mgombea zipo wazi na kuwa atakayechaguliwa, kila mtu atakayemsikia atasema “naam huyu ndiye’ na siyo yule ambaye akitangazwa watu wataanza kuguna.
“Baada ya kumtangaza tu, Watanzania wataseme hapo barabara. Kama hawapo wanaosikika sasa nendeni na mshawishi watu wazuri maana CCM ina hazina kubwa ya watu wazuri wanaofaa kuwa marais
“Maana nami leo sasa natoa siri, siku moja alikuja Kinana akanimbia amekuja muasisi mmoja, je umemuona? Nikamjibu sijamuona.
“… basi akanimbia sawa kama umemuona au hukumuona sawa lakini we zingatia ujumbe wake. Nami ninachotaka kusema CCM tuna utaratibu tumeweka wa kuteua wagombea kwa kuzingatia kanuni na taratibu na maadili ya chama chetu,” alisema.
“Ngoja niwape siri lakini si zote… Siku moja mzee mmoja tulikutana aliniambia maneno fulani nikamkatalia na baadaye nikakutana na Kinana akaniuliza kama nimemuona mzee huyo nikamwambia sikumuona akaniambia nitafakari maneno yake
Alieleza kuwa si dhambi kwa mtu kujitokeza na kutaka urais lakini ni vema maadili ya chama yafuatwe kwa wagombea kuliko kwenda kinyume na miiko na maadili ya chama hivyo wagombea mnatakiwa kufuata maadili ya chama na asiyefuata asije kutulaumu bali ajilaumu mwenyewe.
Hata hivyo Mara baada ya kumalizika kwa hotuba ya Rais Kikwete , Lowassa aliondoka kwa kupitia mlango mdogo wa kutokea uliopo chini ya jukwaa bila kuagana na makada wenzake huku mashabiki wake wakimsubiri kwa hamu bila kufanikiwa kukutana nae
Duru za Kisiasa zinaeleza kuwa Lowassa ni Mwiba mkali kwa wagombea wenzake na ndio maana anakuwa makini sana na nyenendo zake na hata kuondoka kwake jukwaani kabla ya Rais Kikwete kushuka kiliratibiwa kwa umakini mkubwa na wapambe wake kwani kungeweza kuzua shangwe na kuharibu dhima ya maadhimisho hayo
MWISHO
Chapisha Maoni