0
Na Gideon Mwakanosya,Iringa.

KUTOPEWA kipaumbele kwa ofisi za maafisa jamii na maendeleo katika bajeti kumetajwa kuwa miongoni mwa mambo yanayochangia kwa kiasi kikubwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kuendelea kushamiri katika jamii.

Hayo yalibainishwa na wanahabari walioko kwenye mafunzo ya masuala ya ukatili wa kijinsia yanayofanyika mkoani Iringa yakiwa yameandaliwa na Chama cha waandishi wa habari wanawake(Tamwa) ambapo washiriki wanatoka katika mikoa ya Mbeya,Iringa,Njombe na Ruvuma.


Wanahabari hao walisema ofisi za maafisa ustawi wa jamii zinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa fedha kutokana na halmashauri nyingi kutozipa kipaumbele ofisi hizo wakati wa upangaji wa bajeti.


Mmoja wa wanahabari hao Geofray Nilahi alisema wengi wa maofisa kutoka ofisi hizo wamekuwa wakilalamika kukosa fedha na ndiyo sababu hawatekelezi majukumu yao ipasavyo na badala yake wamebakia maofisini ambako kimsingi hawana kazi zaidi ya kupiga soga.


Nilahi alisema uhaba huo wa fedha umesababisha maafisa hao kushindwa kutekeleza majukumu waliyopewa ikiwemo utoaji elimu kwa jamii juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia hivyo kusababisha vitendo vya ukatili kuendelea kukithiri.


“Tunaendelea kulalamikia ukatili wa kijinsia na ukatili wa dhidi ya watoto kila kukicha,Wapo watu wenye dhamana ya kushirikiana na jamii ambao kimsingi wangesaidia kupunguza vitendo hivi lakini hawajapewa kipaumbelea katika bajeti.Hawawezi kuifikia jamii kwakuwa ofisi zao hazina pefa”


“Ni vema watawala na wale wanaopitisha bajeti wakaliona hili na kutambua athari zake.Maafisa ustawi wa jamii na wale wa maendeleo ya jamii wanaweza kwa kiasi kikubwa kuwezesha jamii kuishi maisha ya kuheshimiana na kupendana iwapo watafanya kazi yao.Lakini ofisi zao zimesahaulika kabisa.Imewalazimu kubaki ofisini na kukaa kwenye viti vya kuzunguka” alisema Nihahi.


Naye Joachim Nyambo alisema ni wakati kwa wadau wa masuala ya kijamii kujiuliza kwa kila mmoja ni kwa namna gani ameweza kujitoa katika kuhakikisha anakomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye jamii inayomzunguka na iwapo hajafanya basi atambue kuwa ana deni la kutekeleza hayo.


Kwa upande wake Tumaini Msowoya,alisema bado katika jamii kuna matukio mengi ya ukatili wa kijinsia na pia ukatili dhidi ya watoto ambao baadhi ya wanajamii wanaufanya pasipo kujua kuwa wanakosea.


Msowoya aliutaja ukatili ambao bado unaendelezwa kuwa ni pamoja na wanawake kupigwa na waume zao,wanawake kutumikishwa sambamba na utakasaji kwa wanawake wanaofiwa na waume zao.


Mwisho.

Chapisha Maoni

 
Top