0
KAMANDA WA POLISI MKOA WA RUVUMA ZUBER MWOMBEJI


NA STEPHANO MANGO,SONGEA

JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma linawashikilia wakazi wawili wa vijiji vya Mseto na Liparamba wilayani Nyasa kwa tuhuma za kukutwa wakiwa wamelima  mashamba mawili ya Bangi  yenye ukubwa wa heka tano  ambayo inadaiwa yamekuwa yakitegemewa na watu wanaojihusisha  na  biashara haramu ya kuuza bangi wilayani humo.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Zumberi Mwombeji akizungumza na gazeti hili jana ofisini kwake amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Thadei Ngonyani(26) mkazi wa kijiji cha Mseto na Philimoni Kumburu (58) mkazi wa kijiji cha Liparamba ambao wote walikamatwa juzi majira ya saa za mchana.
Alifafanua zaidi kuwa Jeshi la Polisi Mkoani Humo limefanya Msako Katika maeneo mbalimbali dhidi ya watu wanaojihusisha na kilimo cha zao la bangi na msako ulianza  katika wilaya ya Nyasa.

Kamanda Mwombeji alieleza kuwa katika tukio la kwanza huko katika kijiji cha Mseto kilichopo kata ya Liparamba tarafa ya Mpepo askari polisi wakiwa kwenye msako mkali walifanikiwa kumkamata Ngonyani akiwa amelima zao hilo la bangi lenye ukubwa wa heka tatu.

Alieleza zaidi kuwa katika shamba hilo  Ngonyani alikuwa amechanganya na mazo mengine pembeni kwa lengo la kuficha bangi ambayo ilikuwa katikati ya shamba.

Katika tukio la pili  inadaiwa kuwa Kumburu mkazi wa kijiji cha Liparamba naye alidakwa na askari polisi baada ya kubainika kuwa anashamba la bangi lenye ukubwa wa heka mbili ambalo ndani ya shamba hilo ameotesha miche mingi ya bangi na pembeni amepanda mahindi kwa lengo zao hilo haramu la bangi lisionekane kwa urahisi.

Alisema kuwa mara tu baada ya kuwakamata watuhumiwa hao taratibu za kuharibu bangi hiyo zilifuata sambamba na kuichoma moto chini ya ulinzi mkali wa polisi na watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara tu upelelezi utakapokamilika

MWISHO 

Chapisha Maoni

 
Top