WAZIRI MKUU PINDA AMWAGA MISAADA VETA SONGEA
NA STEPHANO MANGO,SONGEA
WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda amewataka watanzania wenye moyo wa kuwasaidia wananchi wakiwemo wajasilia mali wadogo kutoa misaada mbalimbali hata kama ni midogo lakini itawasaidia kuinua kipato chao na kujikwamua kiuchumi.
Hayo aliyasema jana wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vyerehani 20 ikiwa ni ahadi yake aliyoitoa Julai 20 mwaka jana kwa wanachuo wa chuo cha ufundi stadi VETA cha mjini songea kilipozinduliwa.
Alisema kuwa vyerehani hivyo vyenye thamani ya sh. Milioni 4 vinapaswa kutunzwa ili viweze kuwasaidia wanachuo hao ambao wamehitimu mafunzo yao ya ufundi wa ushonaji na si vinginevyo.
“ Ndugu zangu huu msaada ambao nautoa leo ni kitu kidogo sana lakini ninaamini kuwa utawasaidia wahitimu wakiwa majumbani mwao na wataona umuhimu wa mafunzo ya VETA japo kuna watu wanaamini kuwa msaada lazima uwe ni kitu kikubwa lakini hata kidogo mtu kinamsaidia.”alisema Waziri mkuu.
Hata hivyo amewataka VETA kuendela kuwa wabunifu wa kuongeza taaluma zaidi ya ufundi ili kuendana na soko la ajira kama lilivyo hivi sasa na kwamba watanzania wengi wanahitaji kuyapata mafunzo ya ufundi ili kuweza kuwaongezea vipato vyao vya kila siku na ameahidi kutoa sh. Milioni 10 ambazo zitaweza kuwasaidia shughuli mbalimbali za ufundi kwa wanafunzi wanaosoma chuoni hapo.
Mapema Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu akimkaribisha Waziri Mkuu Pinda kukabidhi vyerehani hivyo kwa wahitimu wa chuo cha VETA katika fani ya ushonaji alisema kuwa ni vyema wanachuo wakaona umuhimu wa kuvitunza vyerehani hivyo walivyopewa kwani ni msaada mkubwa kwao na utaweza kuwaongezea kipato katika maisha yao ya kila siku.
Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi ya VETA kanda ya nyanda za juu kusini Kabaka Ndenda akisoma taarifa ya utoaji wa vyerehani zilizoahidiwa na waziri Mkuu Pinda alisema kuwa chuo kimeamua kuanza na fani ya ushonaji kutokana na uzoefu kwamba wanaojiunga na fani hiyo waliowengi ni wanafunzi wa kike.
Alisema kuwa pamoja na ukweli kwamba kunatatizo la ukosefu wa ajira nchini lakini kundi ambalo ni hatarishi zaidi ni wasichana hivyo vifaa hivyo ni njia nzuri ya kuwawzesha wahitimu kupambana na ajira.
‘’Katika utekelezaji wa ahadi yako y ash. Milioni 10 ya Julai 20 mwaka jana uliyoitoa tumetumia sh. Milioni 4 kununua vyerehani 20 na sh. Milioni 6 itatumika kununua vifaa vya kuanzisha kituo cha kuongeza ujuzi na kuwajengea uwezo zaidi wahitimu wahitimu wa fani ya ushonaji kabla hawajaingia rasmi kwenye soko la ajira”alisema Ndenda
Hata hivyo aliiomba Serikali kuiangalia Veta kisera kama mkombozi wa ajira kwa vijana katika kipindi hiki ambacho dunia nzima inakabiliwa na janga la ukosefu wa ajira hasa kwa kundi la vijana ambalo ni nguvu kazi muhimu hapa nchini.
MWISHO.
Stephano Theofrida Mango
P.O.BOX 835, SONGEA, RUVUMA- TANZANIA.
SIMU: 0755-335051, 0715-335051, 0784-335051, 0778-335051,
Chapisha Maoni