0
Na STEPHANO MANGO,Songea.

MGOMBEA wa udiwani kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM katika kata ya Msamala Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma Isaacki Lutengano amewaahidi mambo makubwa wananchi wa kata hiyo kuwa endapo watampa ridhaa ya kuwa mwakilishi wao kwenye baraza la madiwani la Manispaa hiyo kazi ya kwanza kuimarisha miundo mbinu ya barabara pamoja na kulimaliza tatizo la upatikanaji wa maji ya bomba.

 Lutengano aliyasema hayo jana kwenye ofisi ya afisa mtendaji wa kata ya Msamala muda mfupi baada ya kurejesha fomu ya kuwania nafasi hiyo aliyokuwa ameichukua siku tatu zilizopita baada ya kuibuka mshindi na kuteuliwa ndani ya chama hicho.

 Alisema kuwa licha ya kata hiyo kuwa na  eneo kubwa la mraba  lakini kumekuwepo na changamoto mbalimbali za mambo ya kijamii ikiwemo na suala la ukosefu wa miundombinu ya uhakika kama barabara  hasa za kupita kwenye mitaa.

  Alieleza zaidi kuwa tatizo la upatikanaji wa maji katika eneo la kata hiyo ni kubwa hivyo endapo atachaguliwa kuwa diwani wa kata hiyo kwa kushirikiana na watalaamu wa idara ya maji watahakikisha kuwa tatizo hilo linapungua au kuisha kabisa.
 

Kwa upande wake Happnes Haule ambaye ni mgombea udiwani viti maalumu kupitia chama hicho aliwaeleza waandishi wa habari kuwa wagombea wote wa udiwani kwenye kata hiyo wamekuwa na mshikamano wa pamoja hivyo endapo watachaguliwa watakuwa msaada mkubwa kwa wananchi ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi.
 

Naye afisa mtendaji wa kata ya Msamala Esta Kosa  alisema kuwa kata hiyo mpaka jana mchana wagombea wa tatu wamesharudisha fomu ambapo aliwataja kuwa ni ,Isaacki Lutengano wa CCM,Issa Chamajaa wa Chadema na Kudeka Haule wa ACT ,Wazalendo.
          MWISHO.

Chapisha Maoni

 
Top