0
NA STEPHANO MANGO,SONGEA

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, kikundi cha zaidi ya watu 40 wanaodaiwa kupandikizwa na Mbunge wa Jimbo la Mbinga, Gaudence Kayombo katika kijiji cha Ruanda kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kimewashambulia kwa kuwarushia mawe waandishi wa habari ambao wamenusurika kujeruhiwa vibaya, wakati walipokwenda kijijini hapo kutekeleza majukumu yao ya kikazi.
 
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela amezungumza na vyombo mbalimbali vya habari na kueleza kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 17 mwaka huu majira ya saa 6:30 mchana  kijijini humo, ambapo waandishi hao walivamiwa na kikundi hicho akiwemo na Mwenyekiti wa kijiji, Deograsias Haulle kwa kupigwa na kurushiwa mawe.
 
Alisema Mwenyekiti Haulle ameumizwa mdomoni na puani ambako alipigwa na jiwe na mtu asiyejulikana na kwamba amepatiwa matibabu, katika hospitali ya wilaya hiyo na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
 
Msikhela aliwataja waandishi wa habari mkoani Ruvuma, ambao walikumbwa na mkasa huo kuwa ni; Kassian Nyandindi anayeandikia magazeti ya kampuni ya Businesstimes, Aden Mbelle na Pastory Mfaume kutoka redio ya Jogoo FM iliyopo mkoani hapa mjini songea.
 
Alisema kuwa hali hiyo ilijitokeza wakati wanahabari hao walipokwenda kutekeleza majukumu yao ya kikazi, kuandika habari za tukio la kufungwa kufuli Ofisi za kata ya Ruanda na baadhi ya wananchi ambao majina yao bado hayajapatikana.
 
Wakati walipokuwa wamekamilisha kazi yao wakijiandaa kurudi, ndipo kundi hilo ambalo lilijitokeza ghafla liliwashambulia waandishi hao na kwamba mwandishi wa habari Mbele, alipigwa jiwe katika eneo la usoni upande wa kulia.
 
Kamanda huyo wa Polisi aliongeza kuwa hivi sasa wamefanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja ambaye ni Daniel Komba maarufu kwa jina la Gadaffi, ambaye anadaiwa kuongoza kikundi hicho na kuleta vurugu hizo huku wengine wakiendelea kutafutwa, ili wachukuliwe hatua za kisheria.
 
Vilevile Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga naye amethibitisha juu ya tukio hilo na kusema;  “nimemwagiza OCD wa Mbinga, ahakikishe uchunguzi wa kina unafanyika na watuhumiwa waliohusika katika tukio wanakamatwa na taarifa zaidi tutaendelea kuzitoa baadaye ni wangapi, waliohusika katika jambo hili”, alisema Ngaga.
 
Aidha alipohojiwa  kwa niaba ya wenzake, mwandishi wa habari Nyandindi alisema kuwa yeye alinusurika kupigwa lakini aliokolewa na mtendaji wa kata hiyo ya Ruanda, Dominick Komba kwa kumhifadhi ndani ya nyumba yake ambayo ipo kijijini humo.
 
“Wakati kundi hili linawasili katika eneo la ofisi za kata ambako sisi waandishi wa habari tulikuwa tunafanya mahojiano na viongozi wa kata hiyo, ghafla tulijikuta tumezingirwa na kikundi hicho huku wengine wakipaza sauti wakisema sisi ni wafuasi wa Mbunge Kayombo hatuhitaji waandishi wa habari hapa kijijini kwetu ondokeni haraka sana, huku wengine wakileta fujo”, alisema Nyandindi.
 
Kwa upande wa waandishi wa habari wa redio Jogoo, katika kunusuru uhai wao walikimbia na kwenda kujificha nyumba jirani, zilizopo katika kijiji hicho.
 
Nyandindi aliongeza kuwa vurugu hizo zinatokana na mvutano wa kisiasa uliotawala katika kata hiyo ambao umesababishwa na Mbunge Kayombo, kutokana na kudondoka kwenye uchaguzi wa kura za maoni kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hivyo kikundi hicho kimekuwa kikiendeleza vurugu kijijini hapo na kusababisha kufunga makufuli katika ofisi za serikali za kata ya Ruanda.
 
“Baada ya kujinusuru na mkasa huu, tulikwenda kuripoti kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga, tumefungua jalada la kesi lenye namba MBI/IR/1370/2015 ambapo tunaviachia kazi vyombo vya dola viendelee kutekeleza majukumu yake ili sheria iweze kuchukua mkondo wake ikiwemo watuhumiwa waliohusika na tukio hili wakamatwe na kufikishwa Mahakamani”, alisema.
 
Hata hivyo jitihada za mtandao huu za kumpata aliyekuwa mbunge wa jimbo la mbinga mashariki Gaudence kayombo ziligonga mwamba baada ya kupigiwa simu ya kiganjani kuto pokelewa.
 
MWISHO. 

Chapisha Maoni

 
Top