0
JENISTA MHAGAMA AKIPOKEA ILANI YA UCHAGUZI WA CCM YA 2015-2020 TOKA KWA MGOMBEA URAIS DKT JOHN MAGUFURI
 
NA STEPHANO MANGO, SONGEA
JIMBO la Peramiho linaundwa na kata 16 zenye tarafa mbili za Ruvuma na Mhukuru ni miongoni mwa majimbo tisa ya uchaguzi yalipopo mkoani Ruvuma ambayo yanaendelea na harakati za kampeni za kuomba kura kwa wananchi wake ili kuunda Serikali ya Awamu ya tano

Jimbo hilo ndilo Jimbo pekee mkoani Ruvuma ambalo lilikuwa linawakilishwa na Mbunge mwanamke kupitia chama cha Mapinduzi(CCM) ambaye pia ni Waziri wa Sera ,Uratibu na Bunge Jenista Joakim Mhagama kwa kipindi cha miaka 10 ya Serikali ya awamu ya nne

Katika kipindi cha kura za maoni ndani ya Ccm Jenista Mhagama ndiye mgombea pekee katika majimbo yote tisa yaliyopo mkoani Ruvuma ambaye alipita bila kupingwa ndani ya chama chake kutokana na imani kubwa kutoka kwa wanachama wenzake

Hicho ndicho kilichonifanya nifuatilie mikutano yake ya Kampeni kwa wananchi ili niweze kujua anawaambia nini katika kipindi hicho cha miaka 10 ambayo alikuwa anawawakilisha katika jimbo hilo muhimu kiuchumi na kiutalii

Nimebahatika kuhudhuria mikutano yake mitano kwenye kata ya Maposeni, Parangu, Peramiho,Kilagano na kata ya Litisha ambayo alikuwa anaelezea utekelezaji wake wa ahadi na ilani ya chama chake kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita

“Nimejitahidi kutekeleza ilani ya ccm na ahadi zangu binafsi kwa asilimia 95 katika sekta ya Elimu, afya, nishati ya umeme,maji,barabara na ujenzi,Kilimo na ushirika,mifugo na uvuvi,ardhi na maliasili,biashara na masoko,mawasiliano,uwekezaji, michezo na ajira”alisema Mhagama

Mhagama alisema kuwa  jimbo hilo lenye kata 16 ikiwemo ya   Matimira ,Kilagano ,Ndongosi, Mpandangindo, Mbinga Mhalule, Mtyangimbole, Matumbi, Gumbiro, Nakahuga Magagura,peramiho,Mpitimbi,Mhukuru,Maposeni,Parangu,Litisha kuna mambo mengi sana yamefanyika kupitia sekta hizo kwa uchache nitayasema kwenye mikutano yangu na mengine mtayasoma wenye kwenye kitabu changu cha utekelezaji wa ilani kwa kipindi cha miaka 10 ya uwakilishi wangu

Nimefanikiwa kufika kwenye kila kijiji cha jimbo la peramiho na kufanya mikutano mbalimbali ya kichama na kiserikali na kufanikiwa kuibua miradi mingi na kuitekeleza katika sekta mbalimbali yenye tija na kuwafanya wananchi waendelee kushikamana na serikali yao

Alisema miradi mbalimbali imetekelezwa na kuwafanya wananchi waendelee kufurahia serikali yao kutokana na matumizi mazuri ya raslimali za Taifa chini ya uongozi mahiri kutoka chama cha mapinduzi ukiongozwa na Rais Jakaya Kikwete na watangulizi wake

Kwa kushirikiana na serikali ameweza kuhakikisha ujenzi wa visima 16 vya maji katika kijiji cha liweta, masigira na likuyufusi,kujenga miradi ya maji ya mtiririko katika vijiji vya lilondo,Maweso,Liula na maji ya mtiririko wa Luyelela ambao unaunganisha vijiji 7 na kuwafanya wananchi wa maeneo hayo kuondokana na adha ya maji

Kuna vijiji vichache bado vinakabiliwa na shida ya maji na wataalamu wameshaanza kutafutia ufumbuzi changamoto hiyo na hasa kuvibaini vyanzo muhimu vya maji na kuanza ujenzi wa miradi hiyo kwani kwa sasa huduma ya maji katika jimbo hilo inapatikana kwa asilimia 85

Vikundi vya ujasiliamali vya wanawake, wazee na vijana vimeundwa kwenye kila kata za jimbo hilo na kuwezeshwa fedha za mkopo na kupewa miradi ya kufuga mbuzi, kuku, ng’ombe na nguruwe hali ambayo imesaidia kupunguza kaya zilozo na  umaskini


Katika sekta ya elimu kuanzia elimu ya awali, msingi na Sekondari miundombinu imejengwa kwani kila kijiji kina shule ya msingi , kila kata ina sekondari na maabara moja au mbili na kufanya watoto wengi kupata haki hiyo ya elimu na kwamba kiwango cha ufauru kimeongezeka, wapo pia wanafunzi ambao anawasomesha mbunge

Zipo bado changamoto katika sekta hiyo ikiwemo nyumba za walimu, walimu wa sayansi ni wachache na baadhi ya sekondari hazina mabweni ya kukidhi wanafunzi wote hivyo katika kipindi kijacho cha uongozi wangu nitajitahidi kuyatatua

Sekta ya afya katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wangu nimefanikiwa kuhakikisha kila kata ina zahanati na huduma bora ya afya inatolewa kwa masaa 24 , ingawa zipo kata zina zahanati hadi mbili na kwamba zahanati hizo zote nimeziwekea umeme wa jua, pia tuna vituo vitatu vya afya pamoja na hospital moja hivyo wananchi wanapata huduma hiyo muhimu,

Alisema kuwa yapo mambo madogo madogo ambayo yanapaswa yafanyiwe kazi katika siku za karibuni na hata ilani ya Ccm ya 2015-2020  yameainishwa vizuri ambayo yanalazimisha Serikali ijayo kwa ushirikiano na Mbunge kuyafanya

Mtandao wa barabara katika kipindi cha miaka 10 nimejitahidi kuongeza kwa kasi,ujenzi wa barabara toka wino hadi ifinga umeendelea kuwakomboa wananchi wa eneo hilo, ujenzi wa vivuko , madaraja, na makalvet nao umeongezeka, jambo ambalo nawajibika mara nitakapochaguliwa tena ni kujenga barabara za kuunganisha vijiji vyote vya jimbo la peramiho na kuimarisha barabara hizo ili zipitike muda wote na kuwafanya wananchi waendelee kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo

Mhagama alisema kuwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo, serikali na Kanisa katoliki tumefanikiwa kusambaza umeme kwenye kata chache lakini pia serikali kupitia umeme wa Vijijini(REA) imefanikisha kufikisha umeme karibu kata zote na kwamba unaendelea kuunganishwa kwa wananchi

Lengo ni kuwafikiwa wananchi wote ambao wanataka nishati hiyo kwa matumizi ya ujenzi wa viwanda vidogovidogo, matumizi ya majumbani na matumizi mengine ya kiuchumi kwa vijana na kuwafanya washughulike na wajipatie kipato

Sekta ya kilimo na ushirika tumejitahidi kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo , zana za kilimo,na watu wamelima wengi sana na kufanya uzalishaji wa mazao ya kilimo kuwa mkubwa, changamoto ambayo inatukabili kwa sasa ni kuwa na viwanda vya kusindika mazao hayo, soko la uhakikia la ununuzi wa mazao hayo

Jambo la kuwakopa na kuwalangua wakulima sasa mwisho kwani ilani ya Chama imeitaka Serikali ijayo kusimamia kikamilifu na kuwajali wakulima, hivyo nikichaguliwa naamini tutaibana serikali ili ihakikishe inawajengea viwanda vya usindikaji mazao wakulima ili kupandisha thamani ya mazao yao

Pia wananchi wameweza kujiunga kwenye vyama mbalimbali vya kuweka na kukopo na kufanikiwa kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali, kusomesha na kujenga vitega uchumi ambayo vinawaingizia vipato

Sekta ya mifugo na uvuvi nayo kwa kipindi cha uwakilishi wangu niliiwekea vipaumbele sana kwani wapo wafugaji ambao walipewa mbuzi, ng’ombe, kuku na nguruwe kwa mkopo na wapo wengine wamemaliza mikopo yao na wanaendelea kunufaika na miradi hiyo mizuri ambayo inawaongezea lishe na kipato

Kwa upande wa uvuvi nimejitahidi kuwapatia wananchi wenye mabwawa mbegu za samaki bora, na miradi ya uchimbaji wa mabwawa mapya unaendelea na kwamba upimaji wa viwanja nao unaendelea kwa kasi na kuwafanya wananchi wengi kumiliki mashamba na viwanja vya biashara na makazi

Sekta ya maliasili nimefanikiwa kuunda vikosi kazi vya kulinda misitu, vyanzo vya maji, idadi ya wafugaji nyuki  imeongezeka, mizinga ya nyuki nayo na uvunaji wa asali umeongezeka,vitalu vya miche vimeongezeka, idadi ya misitu iliyotengwa na kuhifadhiwa imeongezeka na hata uchomaji wa misitu ovyo umepungua

Upatikanaji wa simu kwa wakazi wa jimbo hilo umepanuka kwani kwenye kata zote kuna  mawasiliano na upatikanaji wa televisheni, redio na magazeti nayo umerahisha wananchi kuelewa mambo mengi ya kitaifa na kimataifa na kuwa fanya kuwa kijiji kimoja

Kwa upande wa utawala bora katika kata zote kuna ofisi ya afisa mtendaji wa kata na katika vijiji vingi kuna ofisi ya mwenyekiti wa kijiji jambo ambalo linarahisisha upatikanaji wa huduma za kiutawala kwa wananchi

“Nimejitahidi katika kipindi cha mika 10 ya uwakilishi wangu kuligawa jimbo la peramiho na kupatikana jimbo jipya la madaba na wilaya mpya ya madaba jambo ambalo limepunguza kero za wananchi wa kata ya Wino, Igawisenga,mkongotema ambao walikuwa wanasafiri umbali mrefu siku mbili hadi tatu kufuata huduma songea” alisema Mhagama

Alisema wakati anaingia jimboni humo kwa mwaka 2005 hali ya jimbo hilo ilikuwa mbaya sana katika sekta zote lakini nafarijika kwa kutimiza ahadi zangu, na kitendo cha kuhamisha makao makuu ya halmashauri kutoka songea mjini na kujenga makao makuu ya halmashauri kijiji cha Lundusi peramiho kutaharakisha utatuzi wa changamoto ndogo zilizobaki ambazo kimsingi zimeainishwa vizuri kwenye ilani

Leo nasimama kifua mbele nikiwa na furaha za kutekeleza ilani ya Ccm ya mwaka 2005-2015, hivyo najitokeza mbele yenu tena kuomba kura zenu ili niwe mbunge tena ili niweze kumalizia changamoto zilizobaki kwani kwa ushirikiano mkubwa tutafanikiwa

Ni vema ikakumbukwa kwamba kufanya kazi pamoja ni umoja na kudumu katika umoja ni maendeleo, hivyo tuunganishe vipaji vyetu viwe timu moja ya mafanikio kwa maendeleo ya wanaperamiho kwa kuchagua viongozi bora wa Ccm kwa nafasi ya Udiwani , urais na ubunge ifikapo octoba 25 mwaka huu

Wananchi mnatakiwa kukipigia kura chama cha mapinduzi kwani kimeweza kuifanya peramiho kuwa kioo cha maendeleo kitaifa na ing’ale kimataifa kutokana na ushirikiano mlionionyesha kwa kipindi hiko chote cha miaka 10 ya uwakilishi wangu na ndio maana Rais Jakaya Kikwete kwa kuwaheshimu wananchi wa Jimbo la Peramiho aliweza kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo na sasa  kaniteua kuwa Waziri Sera, Uratibu na Bungea , alisema Jenista

Mwandishi wa Makala haya
Anapatikana 0715-335051
MWISHO

Chapisha Maoni

 
Top