0
            KAMANDA WA POLISI RUVUMA MIHAYO MSIKHELA
 
NA STEPHANO MANGO,SONGEA
 
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linamsaka mganga wa kienyeji ambaye jina lake limehifadhiwa mkazi wa eneo la Lilambo manispaa ya songea kwa tuhuma za kumnywesha dawa Lucia Zimbili (65) mkazi wa kijiji cha Maposeni Peramiho ambaye inadaiwa alikuwa analalamikiwa na ndugu zake kuwa amemroga Edward Soko aliyefariki dunia siku chache kabla ya tukio hilo.
 
Habari zilizopatikana jana ambazo zimezibitishwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma Mihayo Msikhela zimesema kuwa tukio hilo limetokea Julai 12 mwaka huu majira ya saa za usiku huko katika eneo la Lilambo nje kidogo ya manispaa ya Songea.
 
Kamanda Msikhela alifanunua zaidi kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio nyumbani kwa mganga wa kienyeji ambaye jina lake limehifadhiwa mwanamke mmoja Lucia Zimbili alifariki dunia baada ya kunywa dawa aliyokuwa amepewa na mganga wa kienyeji.
 
Alifafanua zaidi kuwa Lucia alinyweshwa dawa hiyo na mganga wa kienyeji kwa lengo la kutambua kama kweli alihusika au hakuhusika na kifo cha Edward aliyekuwa amefariki Julaiu 7 mwaka huu huko katika kijiji cha maposeni nje kidogo ya mji mdogo wa Peramiho.
 
Alieza zaidi kuwa baada ya kufariki Soko inadaiwa ndugu wa ukoo walikaa na kisha walimtuhumu Lucia kuwa ndiye aliyemroga na baadaye waliamua kwa pamoja kwenda kwa mganga wa kienyeji kwa lengo la kubaini ukweli wa tuhuma hizo ambako walipofika mganga wa kienyeji aliwapokea na alianza kuwasikiliza tatizo walilokuwa nalo.
 
Alisema kuwa baadaye mganga huyo alianza kuwapa dawa ambayo aliwapa kwa masharti kuwa dawa hiyo wanatakiwa kunywa kwamba kila mmoja atakayekunywa dawa hiyo madhara yakimkuta ndio atakeyekuwa amehusika na kifo cha Edward ndipo kila mmoja alipoanza kunyweshwa dawa ambayo mda si mrefu Lucia alianza kubadilika na  kufariki dunia.
 
Hata hivyo uchunguzi wa awali wa polisi umebaini kuwa mara tu baada ya kifo cha Soko wanaukoo wote kwenye msiba chini ya uongozi wa Biatus Soko walikutana kwa pamoja kwa lengo la kutafuta sababu za kufariki ndugu yao ambapo baada ya kikao walimtuhumu Lucia kuwa ndiye aliyehusika kwa kifo cha ndugu yao.
 
Kamanda Msikhela alifafanua zaidi kuwa kutokana Lucia kukataa kuhusika na tuhuma hizo ndugu kwenye kikao cha familia hiyo waliamua kwa pamoja kwenda kumpeleka kwa mganga kwa lengo la kuondoa ubishi uliojitokeza kati yao na Lucia.
 
Alisema kuwa wanafamilia hao baada  ya kifika kwa mganga walipewa maelekezo yenye masherti ambayo baadaye baada ya kunyweshwa dawa hiyo iliyomsababishia kifo Lucia na kwamba mganga huyo alipogundua Lucia amepoteza maisha alikimbia na kutokomea kusiko julikana na polisi inaendelea kumsaka.
 
MWISHO

Chapisha Maoni

 
Top