MGOMBEA
ubunge kupitia chama cha mapinduzi CCM jimbo la Songea mjini ,Leonidas Gama
amesema kuwa endapo wananchi watampa ridhaa ya kuwa mwakilishi wao kwenye Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
atahakikisha kuwa Manispaa ya Songea inakuwa na umeme wa uhakika pamoja na
viwanda ili kuinua uchumi kwa wakazi wa manispaa hiyo.
Gama aliyasema hayo
jana kwenye uzinduzi wa mikutano ya kampeni za Udiwani Ubunge na Urais kwa
jimbo la Songea mjini uliyofanyika kwenye viwanja vya malori vilivyopo kata ya
Majengo uliyohudhuliwa na mamia ya wakazi wa jimbo hilo.
Alisema kuwa Manispaa ya Songea ina maeneo mazuri ya kuweka
viwanda hivyo atahakikisha kuwa anawatafuta wawekezaji ndani na nje ya nchi ambao
watafika kujenga viwanda ambavyo vitaweza kutoa ajira kwa vijana.
Alifafanua zaidi kuwa pia atahakikisha kuwa kiwanda cha
Tumbaku ambacho kilishakufa siku nyingi
kinafufuliwa na kuanza shughuli ya kukausha Tumbaku ya wakulima jambo ambalo
limekuwa ni kero ya muda mrefu kwa wakulima wa zao hilo.
“Ndugu wananchi hakuna ubishi kuwa Manispaa ya Songea bado
ipo nyuma kimaendeleo hivyo inahitaji mbunge mwadilifu na mchapakazi kama mimi
ninayeyajua matatizo ya wakazi wa Manispaa ya Songea kwa mimi mzaliwa wa hapa
na ni mtoto wenu mwenye uchungu wa kutaka kuwasaidia wanasongea “alisema Gama.
Alieleza kuwa mkoa wa Ruvuma ikiwemo Manispaa ya Songea ni
maarufu kwa kilimo hivyo endapo atakuwa Mbunge atajitahidi kushauriana na
watalaam mbalimbali kuhakikisha manispaa hiyo inakuwa na mipango yakinifu kwa
kuwa na mazao mengine mbadala badala ya kutegemea zao la mahindi peke yake
ikiwemo na kutafuta masoko.
Aidha Gama alieleza kuwa pia atashughulikia kwa karibu kero
za wazee kwa kuhakikisha wanapata matibabu bila kuwepo usumbufu kwenye
zahanati,vituo vya afya na Hospital pamoja na kujenga hoja bungeni kuwa wazee
wote ni lazima wapate pesheni itakayoweza kuwasaidia kupunguza makali ya maisha
yao.
MWISHO.
Chapisha Maoni