Na Stephano Mango,Songea
MGOMBEA wa nafasi ya Ubunge jimbo la Songea mjini mkoani
Ruvuma kupitia tiketi ya chama cha Demokrasia na maendeleo(CHADEMA)Joseph
Fuime,amesema kuwa endapo wananchi watampa ridhaa ya kuwa mwakilishi wao
atahakikisha anafufua zao la tumbaku ambalo lilikuwa mkombozi mkubwa kiuchumi
kwa wananchi wa wilaya ya Songea na Namtumbo.
Fuime aliyasema hayo wakati alipokuwa akiwahutubia wananchi
waliofika kumsikiliza kwenye mkutano wa kampeni wa chama hicho uliofanyika
katika viwanja vya stendi ya malori
iliyopo kata ya Majengo mjini Songea.
Alisema kuwa ufufuaji wa zao hilo utakwenda sambamba na
ufufuaji wa kiwanda cha kusindika tumbaku cha SAMCU ambacho kilikuwa kinatoa
ajira zaidi ya 3000 kwa wananchi na wakazi wa mkoa wa Ruvuma wakiwemo
walemavu,vijana na wanawake.
Alisema kati ya mambo mengine atakayopambana nayo pindi
atakapochaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo la Songea mjini atahakikisha anapigania
suala la upatikanaji wa umeme wa uhakika
ili wawekezaji wengi waweze kujitokeza kuwekeza viwanda vidogo vidogo ambavyo
vitasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.
Aidha aliongeza kusema kuwa
atahakikisha anaboresha huduma za afya kwa kujenga Hospitali kubwa ya
rufaa pamoja na kukomesha tatizo la wagonjwa kulala kitanda kimoja watu watatu
watatu ambalo limekuwa kero kubwa kwa wagonjwa.
Naye mgombea wa nafasi ya Udiwani wa kata ya Majengo iliyopo katika Manispaa ya
Songea kupitia tiketi ya chama hicho,Idd Abdalah akizungumza katika mkutano huo
amewaomba wananchi wamchague tena ili aweze kumalizia kazi ya ujenzi wa
barabara kwa kiwango chalami amayo itafadhiliwa na mfuko wa benki ya dunia.
Abdalah aliyataja mafanikio yaliyopatikana katika kipindi
cha uongozi wake kuwa ni uingizwaji wa umeme kwenye shule ya msingi
Songea,ujenzi wa jiko katika shule ya sekondari Mbulani, ujenzi wa soko la majengo bila ya
kumchangisha mwananchi yeyote pamoja na kushawishi taasisi za kifedha ikiwemo
benki ya posta,Finca na benki ya wanawake kwa akili ya kusaidia kutoa mikopo
kwa wananchi wa kata ya Majengo.
MWISHO
Chapisha Maoni