0


Na Julius Konala,Makambako

CHAMA cha ushirika wa akiba na mikopo cha Mjimwema saccos kilichopo katika Wilaya ya Makambako mkoani Njombe kimetoa msaada wa branketi na shuka 100 zenye thamani ya shilingi 810,000 kwa ajili ya kusaidia Hospitali ya wilaya hiyo.

Mwenyekiti wa chama hicho Bartholomew  Sanga,akikabidhi msaada huo kwa mkuu wa mkoa wa Njombe  Dr. Rehema Nchimbi,mwishoni mwa wiki  alisema kuwa saccos hiyo imeamua kutoa msaada huo baada ya kutambua changamoto mbalimbali zinazoikabili Hospitali hiyo.

Sanga alifafanua kuwa msaada huo uliotolewa kwa ajili ya Hospitali hiyo kati yake branketi ni 50 na shuka 50 kwa  madai kwamba zimetolewa kwa lengo la kuwasaidia wagonjwa wanaopangiwa kulazwa hospitalini hapo.

Akipokea msaada huo mkuu wa mkoa wa Njombe Dr.Rehema Nchimbi,amekipongeza chama hicho kwa msaada wake na kutambua changamoto mbalimbali zinazoikabili Hospitali hiyo kitendo ambacho amekiita ni cha kiungwana.

Katika kuguswa na hilo Dr. Nchimbi alichangia kiasi cha shilingi 100,000 kwa ajili ya kuunga mkono jitihada zilizofanywa na Saccos hiyo kwa lengo la kusaidia Hospitali hiyo ya wilaya ya Makambako huku akiwaomba watu wengine na taasisi mbalimbali kuisaidia hospitali hiyo.

Kwa upande wake mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Makambako Vumilia Nyamoga,ameishukuru na kuipongeza saccos hiyo kwa msaada wake kwa madai kuwa utasaidia kupunguza changamoto iliyokuwa ikiikabili Hospitali hiyo na kudai kwamba ofisi yake itaangalia kila linalowezekana kwa ajili ya kuunga mkono jitiada hizo zilizofanywa na chama hicho katika kusaidia ya wilaya hiyo.

Wakizungumza muda mfupi mara baada ya kutolewa kwa msaada huo,baadhi ya wananchi waliofika kushuhudia tukio hilo walisema kuwa msaada huo utasaidia kupunguza changamoto za wagonjwa kulala bila ya kujifunika kutokana na upungufu wa mashuka na branketi.

MWISHO

Chapisha Maoni

 
Top