Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la
Lishe Tanzania(Panita) Tumaini Mikindo akifungua moja ya mikutano yake
NA STEPHANO MANGO,MBEYA
WADAU wa lishe nchini wametakiwa kushirikiana na kamati za
lishe za Halmashauri zilizopo kwenye kila Wilaya ili kufanya kazi kwa pamoja na
kuhakikisha kuwa hali ya watoto kupata utapiamlo au udumavu wa watoto unakwisha
Wito huo umetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la
Lishe Tanzania(Panita) Tumaini Mikindo alipokuwa akifungua warsha ya siku mbili
ya kuwajengea uwezo wadau wa Lishe kutoka kwenye mikoa ya
Iringa,Njombe,Ruvuma,Mbeya,Rukwa na Katavi inayofanyika kwenye ukumbi wa Gr
City Hotel jijini Mbeya
Mikindo alisema kuwa jukumu la kujenga afya njema kwa watoto
ni la kila jamii hivyo kila mmoja kwa nafasi yake atende haki kwa kutoa mchango
wake wa kiafya na kuijenga jamii bora isiyo kuwa na matatizo ya kiafya
Alisema kuwa ni aibu kuona jamii zinawekeza nguvu kubwa ya
kiuchumi na kilasilimali kwenye kutibu walioathirika na udumavu au utapiamlo
badala ya kujikita kuhamasisha kuzuia magonjwa hayo ambayo hasa yanawakuta
watoto wadogo na wale waliopo shule za msingi
Alifafanua kuwa jamii inaweza kuzuia magonjwa hayo kwa
kuzingatia kanuni za lishe, kulima bustani ndogo ndogo za mboga, matunda,
kuhifadhi vizuri chakula, kuhakikisha kuwa mama mjamzito kabla ya kujifungua
anakula vizuri na akijifungua ananyonyesha mtoto wake kwa uhakika
Alisema kuwa kaya zenye matatizo ya lishe zinapaswa
zitambuliwe na jamii ili ziweze kusaidiwa na kamati za lishe za wilaya kwani
ndani ya kamati hizo kuna wajumbe ambao wanahusika na masuala ya lishe
Awali Mratibu wa Miradi wa Panita Jane Msagati
akiwakaribisha washiriki alisema kuwa wadau wa lishe wanatakiwa kutambua kuwa
wao ndio chachu ya kupatikana kwa takwimu za matatizo ya lishe kwenye maeneo
yao kwani wao ndio wanaishi huko
Msagati alisema kuwa ili jamii iondokane na tabia ya
kulalamika ukosefu wa lishe ni lazima wadau wa lishe watimize wajibu wao kwa
kuwaelimisha namna ya upatikanaji wa mazao bora na utengenezaji wa lishe bora kwenye maeneo yao
Kwa upande wake Mshiriki kutoka Wilaya ya Rudewa Samwel
Mtitu alisema kuwa Serikali ilikuwa na nia njema ya kuanzisha Kamati za Lishe
za Wilaya lakini zinashindwa kufanya kazi kwa kigezo cha kutokuwa na fedha za
kuziendesha
Mtitu alisema kuwa ni muhimu Serikali ikatimiza wajibu wake
ambao kimsingi ulijiwekea kwa lengo zuri la kuhakikisha kuwa utapiamlo na
udumavu wa akili unakomeshwa kwa kushirikiana na wadau wa lishe waliopo kwenye
maeneo yao
MWISHO
Chapisha Maoni