MJUMBE WA BARAZA LA MICHEZO TANZANIA ZAINAB MBIRO
NA STEPHANO MANGO, SONGEA.
MJUMBE wa Baraza la
Michezo la Taifa (BMT) hapa nchini, Zainabu Mbiro amewaomba waandishi wa
habari wasaidie kufichua migogoro iliyopo katika klabu za michezo ili
mamlaka husika, ziweze kuchukua hatua na kuweza kuondokana na matatizo
yaliyopo ambayo yanarudisha nyuma maendeleo katika sekta ya michezo.
Mbiro
alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mkoani
Ruvuma, ambapo pia aliipongeza timu ya Majimaji mkoani humo kwa
kuendelea vizuri katika michezo mbalimbali ya soka.
Kadhalika
alitoa rai kwa kamati za mpira wa pete mkoani humo, kuhakikisha kwamba
wanakwenda hadi katika ngazi za wilaya kuunda kamati ambazo zitaweza
kuimarisha mchezo wa netiboli, na kuwa endelevu.
Alisema kuwa
vyama vya michezo hapa nchini, viongozi wake wasipokaa na kuviendesha
vizuri, hawataweza kuvifanya visonge mbele na kuifanya jamii ishindwe
kufikia malengo yake katika sekta ya michezo.
“Waandishi wa
habari narudia tena kutoa wito kwenu, mtusaidie kufichua matatizo
yanayosababisha sekta hii ya michezo ishindwe kusonga mbele, fichueni
ili wahusika waweze kuwajibika ipasavyo”, alisema.
Mbiro ambaye
pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Netiboli Tanzania (CHANETA) na pia
Mkuu wa wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya alisisitiza kuwa viongozi husika
waliopo madarakani katika vyama vya michezo, kuzingatia maadili ya kazi
zao ili kuweza kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima miongoni mwa
wadau wa michezo hapa nchini.
MWISHO.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Chapisha Maoni