MWALIMU ALIYEWADHALILISHA WANAFUNZI ASHUSHWA CHEO NA KUHAMISHWA SHULE
MKUU WA MKOA WA RUVUMA SAID MWAMBUNGU
NA STEPHANO MANGO,SONGEA
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu amemvua madaraka na kumhamisha makamu mkuu wa shule ya sekondari Namabengo wilayani Namtumbo Shaibu Champunga ambaye alikuwa akituhumiwa na wanafunzi wa shule hiyo kuwa ana lugha chafu na amekuwa akiwadhalilisha wanafunzi kwa kuwashika matiti na makalio pamoja na kuwachapa viboko visivyokuwa na idadi kinyume na sheria za shule.
Akizungumza na gazeti hili juzi kwa njia ya simu mkuu wa mkoa huyo Mwambungu alisema kuwa amechukua uamuzi huo wa kumvua madaraka na kumhamisha makamu mkuu wa shule Champunga juzi alipokwenda kusikiliza kero za wanafunzi ambao hivi karibuni walikuwa wameandamana kwa kutembea kwa miguu kutoka Namabengo wilayani Namtumbo kwenda songea kwa lengo la kutaka kuonana naye licha ya kuwa maandamano hayo yalipigwa stop na askari polisi wa wilaya ya Namtumbo.
Mwambungu alieleza kuwa aliamua kwenda kwenye shule hiyo kwa lengo la kusikia kilio chao wanafunzi ambao walikuwa wanataka kuonana naye na badala yake malalamiko hayo waliyatoa kwa katibu tawala wa wilaya ya Namtumbo Alkwini Ndimbo ambaye baadaye aliwasiliana na uongozi wa shule hiyo kisha wanafunzi waliofanya maandamano walihojiwa na walikili walifanya maandamano bila kibali jambo ambalo lilipelekea kupewa adhabu kwa kuchapwa viboko vitatu kila mwanafunzi na wanafunzi ambao wanadaiwa kuwa ni viongozi walisimamishwa masomo kwa muda wa wiki tatu na wanaporudi shuleni wanatakiwa waje na wazazi wao kwa hatua nyingine ya kinidhamu.
Mwambungu alisema kuwa alipofika kwenye shule hiyo hatua ya kwanza aliichukua kwa kuongea na wanafunzi wote ambao walieleza kero nyingi dhidi ya makamu mkuu wa shule hiyo Champunga na baadaye alikutana na walimu pamoja uongozi wa shule lakini ilibainika kuwa Champunga alikuwa na mapungufu mengi amabayo yalimfanya alazimike kumvua madaraka na kumhamisha shule na amewataka walimu pamoja na uongozi wa shule hiyo kuona umuhimu wa kuzingatia kanuni na sheria pale wanapochukua hatua ya kutoa adhabu kwa wanafunzi .
Machi 1 mwaka huu majira ya asubuhi wanafunzi 106 wa kidato cha sita wa shule ya sekondari namabengo waliandamana kwa kutembea kwa miguu umbali wa kilometa 16 kutoka Kijiji cha Namabengo wilayani Namtumbo hadi kijiji cha Mlete kilichopo nje kido ya manispaa ya songea ambako walizuwiwa na askari polisi wa Namtumbo licha kuwa wao walikuwa wanataka kwenda kuonana na mkuu wa mkoa kupeleka malalamiko yako dhidi ya makamu mkuu wa shule hiyo.
MWISHO
Chapisha Maoni