KAMANDA WA POLISI MKOA WA RUVUMA MIHAYO MSIKHELA
NA STEPHANO MANGO,SONGEA
JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma limemtia mbaroni Janati Haji (32)
mkazi wa kijiji cha Rwinga Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma kwa tuhuma za
kukutwa na meno sita ya tembo ambayo alikuwa ameyapakia kwenye pikipiki
akitokea kijijini Rwinga kwenda Songea Mjini.
Akizungumza na Tanzania Daima jana ofisini kwake Kamanda wa Polisi
wa mkoa wa Ruvuma Mihayo Msikhela alisema kuwa tukio hilo lilitokea mwishoni
mwa wiki huko katika kijiji cha Rwinga.
Msikhela alisema kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio Askari
Polisi wa wilaya ya Namtumbo wakiwa katika msako maalumu walifanikiwa
kumkamata Haji akiwa na Meno sita ya Tembo aliyokuwa amebeba kwenye pikipiki
yenye namba ya usajili T448 CZT aina ya SAN LG.
Alifafanua zaidi kuwa inadaiwa haji alikuwa akiyasafirisha meno
hayo ya Tembo kwenda Songea ambako inadaiwa ndiko alikokuwa anatarajia kuyauza.
Alisema kuwa Polisi kwa kushirikiana na maafisa wa Idara ya
Wanyama pori wanafanya jitihada ili kupata thamani ya nyara hizo na mtuhumiwa
atafikishwa mahakamani mara tu upelelezi utakapo kamilika.
Kamanda Msikhela alisema kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo bado
linaendelea na msako mkali ili kuwabaini watu wanaojihusisha na biashara hiyo
ya meno ya Tembo kwenye mbuga ya wanyama ya selou.
MWISHO
Chapisha Maoni