NA STEPHANO
MANGO,PERAMIHO
MGOMBEA ubunge kupitia chama cha
mapinduzi CCM jimbo la Peramiho Jenista Mhagama amesema kuwa endapo wananchi
watampa ridhaa ya kuwa mwakilishi wao kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania atahakikisha kuwa Halmashauri ya Songea Vijijini inakuwa na umeme
wa uhakika pamoja na viwanda ili kuinua uchumi kwa wakazi wa Halmashauri hiyo.
Mhagama aliyasema hayo jana
kwenye uzinduzi wa mikutano ya kampeni za Udiwani Ubunge na Urais kwa jimbo la
Peramiho uliyofanyika kwenye viwanja vya maposeni vilivyopo kata ya Maposeni
uliyohudhuliwa na mamia ya wakazi wa jimbo hilo.
Alisema kuwa Halmashauri ya Songea
Vijijini ina maeneo mazuri ya kuweka viwanda hivyo atahakikisha kuwa
anawatafuta wawekezaji ndani na nje ya nchi ambao watafika kujenga viwanda
ambavyo vitaweza kutoa ajira kwa vijana.
Alifafanua zaidi kuwa pia
atahakikisha kuwa kiwanda cha Tumbaku ambacho kilishakufa siku nyingi
kinafufuliwa na kuanza shughuli ya kukausha Tumbaku ya wakulima jambo ambalo
limekuwa ni kero ya muda mrefu kwa wakulima wa zao hilo.
“Ndugu wananchi hakuna ubishi kuwa
Halmashauri ya Songea Vijijini bado ipo nyuma kimaendeleo hivyo inahitaji mbunge
mwadilifu na mchapakazi kama mimi ninayeyajua matatizo ya wakazi wa Halmashauri
ya Songea Vijijini kwa mimi mzaliwa wa hapa na ni mtoto wenu mwenye uchungu wa
kutaka kuwasaidia wanaperamiho “alisema Mhagama
Alieleza kuwa mkoa wa Ruvuma ikiwemo
Halmashauri ya Songea Vijijini ni maarufu kwa kilimo hivyo endapo atakuwa
Mbunge atajitahidi kushauriana na watalaam mbalimbali kuhakikisha manispaa hiyo
inakuwa na mipango yakinifu kwa kuwa na mazao mengine mbadala badala ya
kutegemea zao la mahindi peke yake ikiwemo na kutafuta masoko.
Aidha Mhagama alieleza kuwa pia
atashughulikia kwa karibu kero za wazee kwa kuhakikisha wanapata matibabu bila
kuwepo usumbufu kwenye zahanati,vituo vya afya na Hospital pamoja na kujenga
hoja bungeni kuwa wazee wote ni lazima wapate pesheni itakayoweza kuwasaidia
kupunguza makali ya maisha yao.
MWISHO.
Chapisha Maoni