0
WAHITIMU WAKILA KIAPO CHA UADILIFU
 
Na Stephano Mango,Songea
VIJANA 1124 waliojiunga na jeshi la kujenga taifa operesheni Kikwete kwa mujibu wa sheria awamu ya kwanza wamehitimu mafunzo ya miezi mitatu katika kikosi cha 842 KJ Mlale wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.
 
Kati ya vijana hao 1091 wavulana na 1032 wasichana huku vijana 8 wakishindwa kumaliza mafunzo kutokana na utoro.
 
Mkufunzi wa mafunzo hayo Meja Abdusaloom Shausi alisema,kwa muda wote wa miezi mitatu vijana hao wamejifunza mambo mbalimbali kama uzalishaji mali,sanaa,,mbinu za kivita,kwata,utimamu wa mwili na huduma ya kwanza.
 
Aidha,mambo mengine waliyojifunza ni kuhusiana na kujiepusha na maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi,ufugaji wa nyuki, utengenezaji tofari  za kuchoma na mahusiano kwa jamii.
 
Meja Shausi alisema,kutokana na mafunzo hayo wanategemea sana vijana watakuwa waadilifu na waaminifu kwa taifa,wazalendo,heshima na vijana wanaopenda ,kufanya kazi zao bila ya kusubiri kusukumwa na mtu mwingine.
 
Naye Mkuu wa kikosi hicho Meja Thomas Mpuku alisema, lengo la Serikali kurudisha mafunzo hayo baada ya kusimamishwa mwaka 1994 ni kuwajenga utayari vijana wanaojiunga na mafunzo kwa mujibu wa sheria na wale wa kujitolea  kimaadili,katika maisha yao,nidhamu na kuwaweka utayari pindi serikali itakapowahitaji.
 
Mbali na hilo Meja  Mpuku alisema, mafunzo hayo yatawafanya vijana hao kuwa viongozi wazuri mara watakapopata ajira serikalini na kwenye taasisi za watu binafsi.
 
Kwa Upande wake mkuu wa utumishi katika jeshi la kujenga taifa ambaye alimwakilisha MKuu wa Jeshi hilo Kanali Menas Mbele alisema,licha ya Jkt kutoa  mafunzo ya mbinu za kivita kwa vijana nchini,hata hivyo jeshi  hilo lina jukumu la kuwaanda vijana katika malezi bora ya kitanzania ili waweze kuipenda nchi yao.
 
Alisema,serikali itaendelea kutoa fedha  kwa ajili ya kufanya ukarabati na kujenga makambi mapya ili yaweze kuwa na uwezo wa kuchukua vijana wengi na kuishi katika mazingira mazuri.
MWISHO

Chapisha Maoni

 
Top