
NA STEPHANO MANGO, SONGEA
MGOMBEA wa nafasi ya Udiwani kupitia tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo kata ya Majengo iliyopo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma Bakari Likapo,amesema kuwa endapo wananchi watampa ridhaa ya kuwatumikia atahakikisha posho zake zote zinazotokana na vikao vya Baraza la Madiwani zitatumika kwa ajili ya kuchangia mfuko wa maendeleo ya kata hiyo
Likapo aliyasema hayo jana mwishoni
mwa wiki wakati alipokuwa akiwahutubia wananchi waliofika kumsikiliza kwenye
mkutano wa uzinduzi wa kampeni ya kata hiyo uliofanyika katika viwanja vya
Transfoma Majengo mjini Songea.
Alisema kuwa sababu kubwa
iliyomsukuma kuchangia mfuko huo wa maendeleo utakaoundwa katika kipindi cha
uwakilishi wake ni kwa ajili ya kusaidia makundi mbalimbali yasiyojiweza
ikiwemo watoto Yatima,wajane,wazee wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za
kununua pembejeo za kilimo,vijana pamoja na kuwalipia ada watoto wanaoishi
katika mazingira hatarishi.
Aidha kati ya mambo mengine
aliyoahidi kuwatekelezea wananchi wa kata hiyo kuwa ni kuanzishwa kwa viwanda
vidogo vidogo ambavyo vitasaidia kutoa ajira kwa vijana,kutoa mikopo ya
pikipiki kwa masherti nafuu kwa waendesha bodaboda,kupiga marufuku michango
mbalimbali isiyokuwa ya lazima kwenye shule za msingi pamoja na kupambana na
tatizo la kukithiri kwa takataka katika maghuba.
Naye Mwenyekiti wa wa chama cha ACT Wazalendo mkoa wa
Ruvuma,Mohamed Kudeka amewatahadharisha wananchi kuacha kugombanishwa na
bendera za vyama vya siasa badala yake wametakiwa kuwachagua viongozi wenye
fikra na mtazamo wa kimaendeleo na sio wacheza bao.
Hata hivyo mgombea Udiwani kupitia tiketi ya chama hicho kata ya
Misufini Manispaa ya Songea mkoani humo Delux Mayono amewataka wananchi kuacha
kuwachagua viongozi wanaotokana na chama cha Mapinduzi(CCM)kwa madai kuwa chama
hicho kimekuwa maarufu wa kuzalisha na kutengeneza mafisadi ambapo Ukawa ni
wanunuzi wa mafisadi hao.
Kwa upande wake mmoja wa kada wa
Chama cha Mapinduzi(CCM)wa kata ya Majengo Tumaini Msumba,ambaye alifika
kusikiliza Sera za chama hicho kwenye mkutano huo wa ACT alipopewa nafasi ya kusalimia,aliwataka
wananchi kuacha ushabiki wa vyama vya siasa na badala yake wajitokeze kwa
wingi kugombea nafasi za uongozi na
kusikiliza sera za vyama mbalimbali kwa ajili ya kuwapima wagombea watakaofaa
kuwaongoza.
MWISHO
Chapisha Maoni