0


                WAZEE WAKITEMBEA KWA TAABU KWENYE BARABARA YA VUMBI


NA STEPHANO MANGO,SONGEA


AWAMU ya nne ya Serikali ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete inaelekea mwishoni kwasababu ifikapo octoba 25 mwaka huu watanzania watapata fursa ya kuichagua Serikali ya awamu ya tano kwa mujibu wa Katiba ya Nchi kama ilivyohada yake


Kwa kutambua hilo octoba mosi mwaka huu ikiwa ni siku 24 mbele kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo kulikuwa na maadhimisho ya siku ya wazee duniani ambapo wanaharakati na wazee nchini waliungana na wazee wenzao duniani kuadhimisha siku hiyo muhimu, nilitamani siku hiyo Rais Kikwete angepata fursa ya kuwaaga wazee hao baada ya utumishi wake wa miaka 10 kama anavyoaga kwenye maaneo mengine


Na angesema namna alivyowaaidi wakati anaingia madarakani au alivyokuwa madarakani ili watanzania wote kwa pamoja wafahamu kipi ambacho alikiahidi kwa wazee na ametekeleza kipi na anawaachaje katika harakati za kutatua changamoto zao ambazo kila mara ifikapo octoba mosi ya kila mwaka kwenye maadhimisho yao ya siku ya wazee duniani walikuwa wanayatoa matamko mbalimbali yenye lengo la kuboresha ustawi wa maisha yao


Katika siku hiyo, matamko mbalimbali yamekuwa yakiendelea kutolewa kwa nia ya kuikumbusha serikali na jamii juu ya wajibu wao katika kuhakikisha kwamba wazee wanapata haki zao na kuitaka Serikali itemize wajibu wake muhimu wa kuwalinda na kuwathamini wazee nchini


Kwani natambua kuwa hadi sasa, masuala mengi mazuri kuhusiana na wazee yamebaki kuwa midomoni mwa jamii au kwenye nyaraka mbalimbali za serikali na kwamba utekelezaji kuhusiana na namna ya kumaliza kero za wazee umeendelea kuwa wa chini sana na matokeo yake, wazee wetu wameendelea kukabiliwa na changamoto nyingi za kimaisha.


Wazee wengi wameendelea kulalamika kuwa wametelekezwa na Serikali kwasababu haiwajali kwenye  lishe nzuri, makazi bora, matibabu ya uhakika na ulinzi madhubuti kwa ajili ya kupata haki yao ya msingi ya kuishi kama ilivyo kwa Watanzania wengine.


Kwa mujibu wa Sera ya Wazee nchini, mzee ni mtu mwenye umri wa miaka 60 au zaidi na ripoti ya sensa ya 
watu na makazi ya mwaka 2012 inaonyesha kuwa kundi hili linahusisha asilimia 5.6 ya watu wote takriban milioni 45 waliopo nchini.


Na katika muda huo watumishi wa umma na taasisi zake hufikia umri wa kustaafu ajira zao na wale wasio katika mfumo wa ajira rasmi pia hufikia hatua ya kupunguza majukumu ya kazi zao kwasababu ya umri, hivyo suala la uzee na kuzeeka ni dhana inayoelezea hatua ya mwisho ya makuzi ya binadamu yeyote  baada ya kupita katika hatua muhimu za utoto na ujana.


Kwa mujibu wa takwimu za kiserikali wazee nchini wanakadiriwa kufikia milioni 5.6 ikiwa ni miongoni mwao ni wazee waliostaafu ajira katika sekta binafsi na sekta ya umma lakini pia wapo wazee ambao walikuwa katika ajira zisizo rasmi kama kilimo, uvuvi na uchimbaji madini.


Hata hivyo cha kusikitisha ni kwamba licha ya idadi ya wazee kuwa ndogo kulinganisha na marika mengine kama vijana, bado wazee wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi zinazotishia ustawi wa maisha yao na hayo yanatokea,  huku taifa likiwa na rundo la nyaraka zinazozungumzia ustawi wa wazee na namna ya kushughulikia kero zao.


Leo Rais Kikwete anakaribia kuondoka madarakani huku akiwa ameshindwa kutekeleza Sera ya Taifa ya Wazee ya Mwaka 2003, ambayo inajaribu kutoa majawabu kadhaa kuhusiana na kero za wazee nchini.

Serikali iliandaa Sera yenye lengo la kutambua changamoto zinazowakabili wazee, kwa kuwa  ilitambua kuwa wazee ni rasilimali muhimu katika maendeleo ya taifa na ikasisitiza umuhimu wa kutengwa kwa rasilimali za kutosha kwa lengo la kuboresha huduma kwa wazee; kuwashirikisha wazee katika maamuzi muhimu yanayowahusu wao na taifa kwa ujumla na kutoa ulinzi wa kisheria kwa wazee kama kundi maalum, hayo yote yanaelezwa kwenye aya ya 1.3 ya sera hiyo.


Awamu ya nne inaondoka madarakani huku ikiwa na deni kubwa ya kushindwa kutekeleza Sera ya Hifadhi ya Jamii ya Mwaka 2003  na Sheria ya Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii ambapo sera ya Taifa ya afya ya mwaka 2007 iliyofanyiwa marekebisho inataja wazee kuwa ni kundi maalum litakalofaidika na huduma za afya.


Changamoto kubwa ambayo wazee wanakabiliwa nayo ni suala la matibabu na kuwa licha ya wazee hao kupewa vitambulisho vitakavyowawezesha wao kutibiwa bila malipo bado mpango huo hauonyeshi tija na kuendelea kuwapatia usumbufu wazee wetu na kutopata matibabu halisi na kuendelea kusumbuliwa na maradhi ambayo kimsingi yangepata tiba ya uhakika wazee wangekuwa salama


Licha ya Sheria Na. 1 ya Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii ya Mwaka 2001, ibara ya 10 (1) inaruhusu Kamati ya Afya ya Kata kuidhinisha wazee kusamehewa uchangiaji kwenye mfuko huu na kupewa kadi ya utambulisho wa matibabu bora bila malipo.


Ingawa katika katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,  pamoja na marekebisho yake,   ibara ya 12 (2) na ibara ya 14, zinazungumzia wazee kupewa heshima na kupata hifadhi kutoka serikalini na kutoka kwa jamii.


Tamko elekezi la Sera ya Ukimwi inasema Serikali na wadau mbalimbali wataanzisha mifumo ya hifadhi ya jamii kwa ajiri ya wazee ili kuboresha uwezo wao katika kukabiliana na madhara yatokanayo na VVU/UKIMWI jambo ambalo utekelezaji wake unasuasua


Sera ya Taifa ya idadi ya watu na tamko lake elekezi linahimiza kuanzisha hifadhi za kijamii zinazoshughulikia matatizo ya wazee, kuhimiza sekta binafsi, asasi zisizokuwa za Serikali na mashiriki ya kidini kuwekeza katika utoaji wa huduma za kijamii, hususan huduma za afya kwa jamii lakini mpaka sasa utekelezaji wake ni hafifu


Zipo pia sera nyingine nyingi ikiwemo sera ya taifa ya maafa ya mwaka 2004, sera ya taifa ya ardhi, sera ya taifa ya hifadhi za jamii ya mwaka 2003, sera ya lishe na sera zingine zinatamka mahitaji ya wazee lakini utekelezaji wake umeshindwa kutekelezwa

Pamoja na wingi wa nyaraka zinazozungumzia wazee, viongozi mbalimbali pia wamekuwa hodari katika kuelezea umuhimu wa ustawi wa wazee kwa taifa lakini wameshindwa kutekeleza ahadi zao


Akizungumza kuhusiana na serikali kutotimiza kikamilifu matakwa ya sera na ahadi ambazo zimekuwa zikitolewa na viongozi waandamizi wa serikali kwenye maadhimisho ya siku ya wazee duniani wilaya ya Songea yaliyofanyika kwenye viwanja vya Manispaa ya Songea Mkurugenzi wa Shirika linalohudumia Wazee Nchini PADI Iskaka Msigwa alisema kuwa wazee bado wanakabiliwa na changamoto nyingi kwani zingine zimeguswa kwa mbali na serikali lakini zingine bado kabisa hata hajijaguswa


Msigwa alisema kuwa hiyo haimaniishi kuwa serikali haifanyi chochote  yapo ambayo yamefanyika kama vile kuhakikisha huduma za afya zinapatikana bure kwa wazee wote  ingawa pia kuna kasoro nyingi katika hilo, ingawa juhudi zipo kwa kasi ndogo, lakini nguvu kubwa inahitajika ili angalau kumaliza nusu ya matatizo yanayowakabili.


“Wazee wengi wamekuwa wakiuawa kikatili kwa imani za kishirikina, na wakati huo hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa, hali inayozidi kutia shaka kila siku juu ya wazee wengi waliopo vijijini” alisema Msigwa

Alisema kuwa hali ya upatikanaji wa lishe imefanya afya za baadhi yao kudorora na pia kushambuliwa na maradhi kila mara hali ambayo inatishia uhai wa maisha yao na kwamba suluhisho katika matibabu ya wazee kama bima ya afya ya jamii maana bima itawasaidia hata kwenda kupata dawa katika maduka yaliyoidhinishwa


Wazee hao pia wanakabiliwa na matatizo  ya  kuishi katika nyumba zilizochakaa zisizo na wavu kwenye madirisha ya kuzuia mbu, vyoo  vya kujisaidia, maji safi ya kunywa na kuoga na kambi hiyo kukosa umeme kwa muda mrefu.


Kilio kingine cha wazee ni pensheni kwani upatikanaji wake itampa unafuu wa maisha wa kumudu mambo ya msingi, kwa kuwa wazee nao walishiriki ujenzi wa taifa kwa namna moja ama nyingine bila kujali alikuwa ni mfanyakazi katika sekta rasmi au la

Katika maisha ya jamii ya kila siku wazee  wanakubalika kuwa ni kisima cha ujuzi katika masuala mbalimbali  ya kijamii na pia walitumika katika kutoa mwongozo au ufumbuzi kwa jamii katika masuala muhimu katika nyanja za uchumi, siasa, utamaduni na hata imani.


Na kwamba zipo nchi ambazo wazee huheshimiwa sana kutokana na mchango wao katika jamii husika na hupatiwa mahitaji yote muhimu kama malazi, mavazi, chakula, uangalizi  wa fya zao na ulinzi


Ni muhimu sasa sera ya Taifa ya wazee ya mwaka 2003 ikapitishwa na kuwa sheria, ili mambo mengi yanayohusu wazee yasimamiwe kisheria kwani yapo ndani ya Sera hiyo kwani ni jambo la ajabu sana toka mwaka 2003 sera nyingi zimepitishwa na kuwa sheria lakini haifahamiki ugumu wa sera hiyo kutopitishwa na kuwa sheria upo wapi.


Ni lazima jamii ikakumbuka kuwa maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya wazee kwa kujielekeza zaidi katika vitendo kushughulikia kero za wazee na siyo maneno tupu kwani ikumbukwe kuwa vijana wa leo ndiyo wazee wa kesho.


Mwandishi wa Makala haya

Anapatikana 0715-335051
 
MWISHO



Chapisha Maoni

 
Top