0
Diwani wa Kata ya Matimila Menas Komba akila kiapo cha kuwatumikia wananchi wa kata yake kwa uadilifu na uaminifu mbele ya aliyekuwa Hakimu wa Mahakama ya Mkoa wa Ruvuma Aziza Lutalla


NA STEPHANO MANGO,SONGEA


WANANCHI wa Kata ya Matimila Wilaya ya Songea wametakiwa kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi wa Wabunge,Madiwani na Rais Octoba 25 mwaka huu ili kuwachagua wagombea wa nafasi hizo kutoka chama cha Mapinduzi ikiwa ni shukrani kwa maendeleo waliyoyapata katika sekta mbalimbali nchini


Wito huo umetolewa jana kwenye Mkutano wa hadhara wa  Kampeni uliofanyika kwenye Kijiji cha Liula, Mpingi na Kikunja na Mgombea Udiwani  wa kata ya Matimila Menas Komba ambaye pia ni diwani aliyemaliza muda wake wa uongozi katika kata hiyo


Komba alisema sababu za wananchi hao kuichagua Ccm zipo wazi hasa kwenye kata ya Matimila kwani hapo awali barabara nyingi zilikuwa hazipitiki na sasa zinapitika na madaraja pamoja na vivuko vimejengwa na kuwafanya wananchi kuendelea na ujenzi wa taifa kupitia shughuli zao mbalimbali za kiuchumi na kijamii


Alifafanua kuwa kwa kipindi cha mwaka 2015 na 2020 amejidhatiti  kushirikiana na Serikali kufungua barabara ya  Matogoro kwenda Kiheo hadi Liula B, barabara ya Matimila kwenda Kikunja ili iweze kurahisisha huduma ya usafiri na mawasiliano miongoni mwa vijiji hivyo


Alisema kuwa shule za msingi kwenye kata hiyo zilikuwa chache na hazina walimu wa kutosha lakini leo shule za msingi zipo kwenye vijiji vyote 6 vya kata hiyo na kwamba walimu wapo wa kutosha hali ambayo imesababisha kila mtoto mwenye umri wa kuanza shule anapata haki yake ya msingi ya elimu na kufanya kiwango cha elimu kuwa kikubwa kwenye kata hiyo na hata ufaulu wa kuingia kwenye sekondari ya kata umekuwa mkubwa sana


Alieleza kuwa upatikanaji wa huduma ya maji kwenye kata hiyo ni wa asilimia 92 kwa wananchi wake na kwamba tayari upembuzi yakinifu umeshafanyika kwenye vyanzo vipya vya maji na fedha zipo kwa ajiri ya kumalizia kazi za kutandaza mipira ya maji na kuwafanya wananchi hao wanapata maji safi na salama kwa wakati wote


Alisema kuwa katika kijiji cha Matimila A na B na Kijiji cha Mpangula kuna mradi wa maji kutoka katika milima ya Matimila mto Kazembe ambao umegharimu milioni 185 ambapo wananchi walichimba mifereji na kufikia mabomba umekamilika na sasa wanafunga koki kwa ajiri ya kutoa huduma hiyo muhimu


Alifafanua kuwa katika sekta ya afya kuna zahanati kijiji cha kikunja,liula na matimila lakini kwenye kijiji cha mpangula ujenzi wake umefikia hatua za kupaua na kwamba zahanati hizo zina wataalamu wa kutosha pamoja na nishati ya umeme jua


“Changamoto iliyopo kwenye Zahanati za Kikunja na Liula ni kukosekana kwa wodi za kuwalaza wagonjwa ambapo kwenye mpango wa 2015 hadi 2020 ni kujenga wodi hizo ,kujenga Kituo cha afya kimoja ili wananchi waweze kupata huduma muhimu za afya katika Vijiji vyao badala ya kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu” Alisema Komba


Alisema kuwa vikundi 35 vya wazee, kina mama na vijana kila kijiji vimewezeshwa na mfuko wa jimbo fedha za mtaji kwenye shughuli zao za kiuchumi kwenye kaya zao na kuwafanya waweze kujikimu katika maisha yao ya kila siku


Alieleza kuwa kata hiyo imefanikiwa kuingia kwenye mpango wa kupata umeme Vijijini(REA) ambapo katika awamu ya kwanza vijiji vya Liula,Mpangula, Matimila A na Matimila B na kwamna wananchi wanatakiwa kujiandaa kijasiliamali ili kuweza kunufaika na nishati hiyo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi


Alisema katika kipindi kijacho amejipanga kikamilifu kuisukuma selikari kuhakikisha wakulima wanapata masoko ya uhakika ya kuuzia mazao yao kupitia bei elekezi ili kumfanya mkulima aweze kunufaika na kilimo ambacho kimsingi ndio uti wa mgongo wa wakulima wa kata hiyo


Katika sekta ya michezo alisema vijiji vyote kumekuwa na mashindano ya Diwani Cup na kufanikiwa kupata zawadi mbalimbali na kuwafanya vijana kutumia muda mwingi kwenye michezo badala ya kuingia kwenye makundi mbalimbali maovu hali ambayo imeifanya kata hiyo kuwa ni kitovu cha amani na upendo


Kwa upande wake Katibu wa Ccm Wilaya ya Songea Rajab Uhonde alisema kuwa Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete kwa kushirikiana na Viongozi wengine wameweza kuwafikia wananchi katika sekta mbalimbali na kuwafanya waifurahie Serikali yao


Uhonde alisema kuwa kwa ushirikiano mkubwa ulioonyeshwa na mbunge wa Jimbo hilo Jenista Mhagama kuitekeleza vyema ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010-2015 kumeifanya chama hicho kutembea kifua mbele na kuwaeleza wananchi mafanikio yake


Alisema kuwa haoni sababu yoyote ya wananchi kuzubaishwa na propaganda kutoka vyama vya upinzani ambavyo lengo lake ni kufifisha mazuri yaliyofanya kwa kipidhi chote cha utawala wa serikali zilizopita kwani kila mmoja ni shahidi wa kasi ya maendeleo yanayotokea kwenye jamii zetu


“Kutoka na sababu hizo hakuna sababu ya kuiangusha Ccm madarakani bali muda muafaka umefika wa wananchi kukaa na wagombea na kuweka vipaumbele vyenu ili kuweza kutafuta kwa pamoja vikwazo ambavyo vinaonekana kurudisha nyuma maendeleo” alisema Uhonde

MWISHO


Chapisha Maoni

 
Top