0



Baadhi ya watoto wa kijiji cha Mkongotema wilaya ya Songea wakichota maji kwenye mabomba ya mtililiko baada ya kwa kukamilika(Picha zote na Stephano Mango)


Naibu waziri wa maji Amos Makala akizindua mradi wa maji ya mtiririko katika kijiji cha Mkongotema katika halmashauri ya Wilaya ya Songea vijijini wakati wa ziara yake ya siku 4 mkoani Ruvuma kukagua na kuzindua miradi ya maji wa kwanza kushoto mwenye shati la kijani ni Katibu wa CCM Wilaya ya Songea Rajabu Uhonde, katika mwenyeupinde mweusi kifuani ni Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Songea John Ulindi

Na Stephano Mango,Songea.


MAJI ni uhai katika maisha ya binadamu na viumbe hai wengine kwa kutambua hilo hivi karibuni Naibu Waziri wa maji Amos Makala alifanya ziara ya siku tano katika mkoa wa Ruvuma ya kutembelea na kukagua miradi ya maji  ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi (CCM) katika kipindi cha miaka 5.


Katika ziara hiyo Naibu waziri Makala alitembelea halmashauri tano za Mkoa wa Ruvuma ambazo ni Mbinga,Namtumbo,Halmashauri ya Manispaa  ya Songea na halmashauri ya Songea vijijini na aliweza kupata nafasi ya kuongea na wanachi ambao walitoa kero zao juu ya upatikanaji wa maji hasa maeneo ya vijijini ambako awali wananchi walikuwa wakitumia maji ya visima ambayo si salama kwa matumizi ya binadamu.


Awali katika ziara hiyo alianza kwa kutembelea halmashauri ya Songea vijijini ambako alipata fursa ya kujionea  mwenyewe na kuzindua mradi mkubwa wa maji ya mtiririko ambao unahudumia wananchi wa vijiji viwili vya Mkongotema na Magingo kata ya Mkongotema Tarafa ya Madaba ambapo mradi huo  hadi kukamilika umegharimu kiasi cha sh. Bilioni 1.6.


Makala anasema kuwa miradi ya maji inayotekelezwa kwenye halmashauri ni utekelezaji wa ilani ya CCM ya kuwapatia wananchi huduma ya maji hivyo hawana budi kuitunza kwa gharama kubwa kwani serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuwekeza kwenye miradi ya maji nchini.


Anasema kuwa miundombinu ya maji isipotunzwa vizuri inaweza kukosesha maji kutokana na uharibifu wa mazingira ambayo yanaweza yakasababisha wananchi wakaendelea kupata shida ya maji kama zamani jambo ambalo halileti maana kwa jamii.


Makala anaendelea kufafanuwa zaidi kuwa hali ya maji mkoani Ruvuma sio ya kuridhisha sana lakini serikali kupitia Wizara ya maji itajitahidi kupunguza tatizo hilo kwa kiasi kikubwa na si vinginevyo.


Hata hivyo Naibu waziri huyo amewaonya baadhi ya watu wanaoharibu vyanzo vya maji kwa kufanya shughuli za kibinadamu kwani hao wanarudisha nyuma juhudi za serikali za kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma ya maji kama inavyo stahili.


Makala pia ametumia nafasi hiyo kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Peramiho Jenista Mhagama ambaye pia ni Waziri wa Nchi ,sera na Uratibu wa Bunge kuwa ni mpiganaji mzuri kwani alimuandikia barua ya kuomba vijiji viwili vya Magingo na Mkongotema Vipatiwe huduma ya maji  tangu hapo amekuwa mfuatiliaji mkubwa hadi mradi huo umekamilika tofauti na wabunge wengine ambao wengi wao sio wafuatiliaji.


‘’Ndugu zangu niwaeleze leo kuwa Wizara ya maji ilikuwa haijui Mkongotema wala Magingo na hii ni matokeo mazuri ya kumchagua mbunge makini ambaye anajari wananchi wake bila kuangalia itikadi za vyama kwani maji haya hawatayatumia wanaCCM peke yao”alisema Makala


Makala alieleza zaidi kuwa kuna msemo usemao kuwa Tenda wema usingoje shukrani serikali imefanya mengi lakini changamoto haziwezi kuisha zote kwani pamoja mradi huo kuzinduliwa lakini hautoshi kwa kuwa familia zinazidi kuongezeka siku hadi siku hivyo wizara itaendelea kutoa fedha kwaajiri ya kuongeza vituo vya kuchotea maji kwani vilivyopo sasa ni 25 na kwamba vinahitajika tena vituo vingine 25 ili kuondoa kabisa tatizo la maji.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya watumia maji wa vijiji vya Magingo na Mkongotema (MAMKO) Gideon Mbilinyi anasena kuwa kukamilika kwa mradi huo wa maji katika vijiji hivyo imekuwa ni faraja kubwa kwa wananchi wakiwemo akina mama na watoto ambao kwa siku za nyuma kabla mradi huo hajakamilika walikuwa wanachota mbali na maeneo wanayoishi ambapo maji hayo hayakuwa salama.


Anasema kuwa mradi huo unatenki kubwa la maji lenye ujazo wa lita laki mbili za maji ambalo linatoa maji kwa wananchi wa vijiji hivyo na kwamba wananchi wao wenyewe wamejipanga kikamilifu kutumia maji kwa njia ya kuchangia kwa mara ya kwanza walifanikiwa kuchangisha kiasi cha sh.milioni 21 ambazo zimehifadhiwa benki.


Anasema kuwa Tenki la lililojengwa linauwezo wa kuhudumiwa wananchi zaidi ya 5000 lakini idadi ya wanavijiji vya Magingo na Mkongotema ni 4660 na mtandao wa maji uliopo unauwezo mkubwa wa kutiririsha maji kwenye vijiji vyote viwili na utaweza kudumu kwa zaidi ya miaka 25 ijayo na kuwa mfano kwa wakazi wa vijiji vingine.


Anasema kutokana na mradi huo wa maji kukamilika wananchi tayari wameelimishwa umuhimu wa kutumia maji ya bomba na kwamba katika kipindi cha mvua wameelimishwa namna ya kuvuna maji ya mvua kwa gharama nafuu na kila mwananchi anaweza kutengeneza tenki dogo la kuhifadhia maji ya mvua.


Pamoja na mafanikio aliyoyatoa Mwenyekiti wa Bodi hiyo ya watumia maji anasema kuwa wanakabiliwa na changamoto chache ikiwemo uelewa mdogo wa wananchi juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji kwani waliowengi hawajui sheria za kudhibiti vyanzi vya maji kuwa mwananchi anatakiwa kuacha mita 60 toka kwenye kingo za maji.


Mbilinyi anasema kuwa tayari wamejipanga kukabiliana na changamoto hizo kwa kuendela kutoa elimu kwa wanachi juu ya umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji na faida zake ili mmradi huo huweze kuwa endelevu na kuwanufaisha wote .


Elizabethi Mlowe mkazi wa kijiji cha Mkongotema anaeleza adha waliyokuwa wanaipata kabla ya kupatiwa mradi huo wa maji kuwa walikuwa wanatembea umbali merfu kwenda mtoni kuchota maji huku wengi walipatwa na masahibu ya kubakwa jambo ambalo lilikuwa linachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma shughuli mbalimbali za maendeleo kijijini hapo.


Winifrida Mfikwa mkazi wa kijiji hicho cha Mkongotema anasema kuwa kwa muda mrefu kabla mradi huo hajakamilika walikuwa wanakunywa maji ya visisma ambavyo si salama kwa matumizi ya binadamu na wakati mwingine walikuwa wanalazimika kufuata maji mtoni ambako kuna umbali wa kilomita 1 hivyo anaishukuru serikali kwa kuwaletea mradi huo wa maji na sasa kazi zao zinaendelea vizuri .

Kwa upande wake Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea John .A. Undili alisema upatikanaji wa huduma ya katika halmashauri inazidi kuimarika kwhivi sasa kuna miradi mipya ya maji katika vijiji 20 inayotekelezwa chini ya mpango wa  RWSSP na  BRN kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia
 2012/2013, 2013/2014 NA 2014/2015.


Undiri alisema kuwa vijiji vya MAGINGO NA MKONGOTEMA ni miongoni mwa miradi iliyokamilika na kufanya asilimia ya wananchi wanaopata maji safi na salama katika halmashauri ya wilaya ya Songea kupanda toka 47%  mwaka 2010 hadi 68% mwaka 2015.

Alisema kuwa jitihada za kuimarisha huduma ya maji katika halmashauri hiyo zinaendelea kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo ndani na nje ya nchi kama vile Wizara ya Maji, mbunge wa Jimbo la Peramiho Jenista Mhagama na wafadhiri mbalimbali


Naye mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Songea Sxbert Kaijage anaanza kwa kueleza kuwa mradi huo wa maji ya mtiririko katika vijiji vya Magingo mkongotema umegharimu kiasi cha sh. Bilioni 1.6 na wamechukuwa kwenye chanzo cha mto Mgombezi ambapo hadi sasa vituo 25 tayari vimefunguliwa.


Anaelezea mikakati ya mradi huo kuwa ni kutoa elimu juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira ,elimu kwa wakulima wanaopenda kulima kwenye vyanzo vya maji na uchomaji moto wa misitu na halmashauri imeweka sheria ndogo ndogo za kuwabana waharibifu wa mazingira ili kuhakikisha vyanzo hivyo vinakuwa endelevu.


Hata hivyo mkurugenzi Kaijage ameiomba Wizara ya maji kuwaletea fedha haraka ili kukamilisha baadhi ya miradi ya maji ambayo haijakamilika kutokana na uhaba wa fedha kwenye vijiji vya Lihula, Matimila na Likuyufusi ambako miradi yake imesimama kutokana na wakandarasi kutolipwa fedha zao kwa wakati.


Aidha katika ziara yake hiyo Naibu Waziri wa maji Makala ameipongeza halmashauri ya Wilaya ya Songea kwa kufanya vizuri na kuzitaka halmashauri zingine mkoani humo kuiga mfano huo ambapo hadi anaondoka Ruvuma ameoneshwa kutoridhika na miradi ya maji inayotekelezwa katika halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kutokana na ubadhirifu mkubwa wa fedha za mila na amehaidi kutuma tume ambayo itakwenda kukagua miradi hiyo ya maji na ikibainika hatua za kisheria zitachukuliwa juu yao.


Mwandishi wa Makala haya

Anapatikana kwa 0715335051

MWISHO.

Chapisha Maoni

 
Top