Afisa mtendaji wa kata ya Peramiho Salma Kipande
NA STEPHANO
MANGO,SONGEA
PERAMIHO ni eneo
maarufu ndani na nje ya Tanzania ambalo linapatikana kilometa 24 tu
kutoka mjini Songea mkoani Ruvuma na ina wakazi zaidi ya 14,000 kwa mujibu wa
sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012
ipo katika Halmashauri ya wilaya ya Songea na inaundwa na vijiji vinne ambavyo ni
Peramiho A,Peramiho B,Lundusi na kijiji cha nguvumoja .
Afisa mtendaji wa kata hiyo Salma Kipande anasema ili kuhakikisha
kuwa wananchi wa kata hiyo wanatekeleza kauli mbiu ya Rais John Magufuli kwa
Vitendo ya Hapa kazi tu kuna mipango kabambe ya maendeleo ambayo wameipanga
katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 inatekelezwa katika vijiji vyote vinne
ambayo vinaunda kata hiyo ambayo ndiyo kioo cha Halmashauri ya wilaya ya
Songea.
Katika kuhakikisha kuwa kauli ya hapa kazi tu inatekelezwa
kwa vitendo katika kata hiyo,afisa mtendaji wa kata hiyo , Salma Kipande
anasisitiza kuwa katika kikao cha kamati ya maendeleo ya kata hiyo
kilichofanyika hivi karibuni,moja ya mambo ambayo yalipitishwa na wajumbe wote
ni pamoja na kuwa na benki ya tofali ambapo kila kijiji kimeweka mkakati wa
kufyatua tofali laki tatu.
“Tofali hizo zitafyatuliwa kuanzia mwezi Juni na kuchomwa
mwezi Julai , vijijini vinne vinahusika ambavyo ni Peramiho A,Peramiho
B,Lundusi na Nguvumoja ambapo jumla tutakuwa na tofali milioni moja na laki
mbili ambazo zitatumika katika miradi mbalimbali ya ujenzi zikiwemo
ofisi,vyumba vya madarasa,zahanati pamoja na shughuli nyingine ambazo
zinahitaji tofali’’,alisisitiza.
Kwa upande wake kaimu mratibu elimu kata ya Peramiho Rashid
Pilly amesema kata hiyo ina jumla ya shule za msingi sita pamoja na shule mbili
za sekondari ambazo zinamilikiwa na serikali na kwamba kuna shule moja ya
sekondari ambayo inamilikiwa na Abasia ya Peramiho.
Hata hivyo amesema kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi
kata hiyo inafanya sensa ya wanafunzi pamoja na kupima eneo ambalo limepangwa
kujengwa shule mpya ya msingi ya Ukombozi katika eneo la Njunde Peramiho
linalokadiriwa kuwa na hekari 10 na kwamba kinachosubiriwa ni ramani kutoka
Halmashauri ya wilaya ya Songea vijijini ili kazi ya ujenzi iweze kuanza mapema
mwaka huu.
Hata hivyo kaimu mratibu elimu kata huyo ambaye pia ni
mwalimu mkuu msaidizi shule ya msingi Peramiho A ameitaja changamoto kubwa
ambayo inaikabili shule hiyo ni kuoza kwa vigae vilivyotumika kuezeka shule
hiyo ambapo msimu wote wa mvua wanafunzi wanashindwa kusoma kutokana na vyumba
viwili vya madarasa kuvuja hivyo kuathiri tendo la ufundishaji.
“Vigae vyote vilivyotumika kuezekea shule hiyo vimeoza
vinatakiwa kuondolewa ni vya muda mrefu badala yake shule iezekwe upya kwa
kutumia bati ili kudhibiti kuvuja kwa vyumba vya shule na kuathiri ujifunzaji
na ufundishaji’’, alisisitiza Pilly.
Naye mwenyekiti wa kijiji cha Nguvumoja ambaye ni kaimu
diwani wa kata ya Peramiho Joseph Ngonyani amesema kata ya Peramiho imedhamiria
kusonga mbele katika sekta zote ikiwemo elimu, afya, mazingira, mapato,michezo
na kuboresha huduma zote muhimu za kijamii kwa wananchi.
Hata hivyo aliitaja changamoto ya maji katika vijiji vya kata ya Peramiho imekuwa
kero kubwa katika vijiji vyote vinavyounda kata ya Peramiho na kusisitiza kuwa
katika kijiji cha Peramiho B kuna upungufu mkubwa wa maji safi na salama ambapo
katika vijiji vya Nguvumoja,Peramiho A na Lundusi maji yanapatikana kwa gharama
kubwa.
Amesema kuwa katika vijiji vya Peramiho A na Nguvumoja
umeanzishwa mradi wa maji ya bomba ambao unafahamika kwa kifupi cha majina ya
vijiji viwili yaani PENGU ambao ni mradi wa maji ya bomba unaoendeshwa kwa
umeme wa jenerata kutoka chanzo cha maji cha mto Namihoro.
“Wananchi wengi wanashindwa kulipia bili za maji katika
mradi huu ambapo gharama kwa mwezi inafikia hadi shilingi 50,000 na ndoo moja
inatozwa shilingi 50 hali ambayo inasababisha wananchi kushindwa kumudu kulipa
hivyo kubakia kuwa changamoto kwa wananchi masikini’’,alisema mwenyekiti wa
kijiji cha Peramiho A David Kapinga.
Hata hivyo utafiti ambao ulifanywa na waandisi wa maji wa
Halmashauri ya wilaya ya Songea katika vyanzo vya kata hiyo umebaini kuwa
vyanzo vyote vya maji vilivyopo vina maji ya kutosha kinachotakiwa ni serikali
kuwawezesha umeme wa TANESCO ili kupunguza gharama za kutumia jenereta za
mafuta ambazo zina gharama kubwa katika uendeshaji wake.
Kamati ya maendeleo ya kata ya Peramiho imependekeza kwa
kauli moja kuchimba kisima cha maji ili kutatua tatizo la maji katika shule ya
msingi kijiji cha Mnyonga yenye wanafunzi 200 kati yao wanafunzi 20 ni wenye
ulemavu wa akili.
Shule hiyo inatumia vyoo vya kisasa ambavyo vinahitaji maji
mengi ambapo hivi sasa kutokana na gharama kubwa ya kulipia maji inayotozwa
katika mradi wa PENGU,shule hiyo ina kosa maji hali ambayo inahatarisha
wanafunzi hao kupata magonjwa ya maambukizi hasa katika kipindi cha kiangazi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Peramiho A Jommo Mbilinyi alisema
kijiji chake kinaendelea kutekeleza kwa vitendo kauli ya Rais Magufuli kwa
vitendo ambapo tayari kijiji kimejenga zahanati ya kijiji ambayo imekamilika
kwa asilimia 80 pamoja na ofisi ya serikali ya kijiji ya kisasa ambayo
inatarajia kugharimu shilingi milioni 60 hadi itakapokamilika .
Afisa maendeleo ya jamii kata ya Peramiho
Pirmin Mbilinyi
Kwa upande wake Afisa maendeleo ya jamii kata ya Peramiho
Pirmin Mbilinyi amesema idara yake inafanya hamasa kubwa ya kuhakikisha kuwa
vikundi vya ujasirimali vilivyosajiriwa vinaundwa katika kata hiyo ambapo hadi
sasa katika kata nzima kuna vikundi vya ujasiriamali vilivyosajiriwa 20.
Mbilinyi anasisitiza kuwa
uhamasishaji mkubwa unafanywa na ofisi ya maendeleo ya jamii katika kata
hiyo kuhakikisha kuwa wananchi wake
wanakuwa mstari wa mbele kuhakikisha kata inasonga mbele kiuchumi ili kila
mmoja afanye kazi kwa bidii kama kauli
mbiu ya hapa kazi ilivyoagiza.
Akizungumzia mahusiano kati ya serikali kata ya Peramiho na
uongozi wa kanisa katoliki Abasia ya Peramiho,afisa mtendaji wa kata hiyo Salma
Kipande amesisitiza kuwa kanisa katoliki katika Abasia hiyo linashirikiana vema
na serikali kwa miaka mingi na kwamba limekuwa na mchango mkubwa katika
maendeleo ya kata hiyo hasa katika sekta ya afya na elimu.
Kipande anasisitiza kuwa kanisa katoliki linatekeleza kwa
vitendo kauli mbiu ya hapa kazi tu kwa sababu katika Taasisi mbalimbali
zilizopo katika Abasia hiyo kanisa limetoa ajira kwa watanzania pamoja na kutoa huduma muhimu za afya na elimu
katika ngazi mbalimbali kwa maendeleo ya watanzania na Taifa kwa ujumla wake.
Abasia ya Peramiho ina seminari kuu inayohudumia nchi nzima,hospitali
ya misheni ya rufaa inayohudumia watanzania kutoka nchi
nzima,chuo cha uuguzi,kiwanda cha uchapaji yaani Peramiho printing press,chuo
cha ufundi seremala,magari na umeme na tawi la chuo kikuu cha madaktari
Bugando.
Utafiti umebaini kuwa Peramiho inafahamika zaidi nje ya nchi
pengine kuliko miji mingine iliyopo kusini mwa Tanzania kutokana na mji huo
kuwa na historia ya namna yake kipekee.Peramiho inaunganishwa
na wabenediktini wa kanisa katoliki kutoka St.Otilia nchini
Ujerumani,ambao waliamua kuweka makao makuu yao katika Abasia ya Peramiho.
Wabeneditine hao waliingia kwa mara ya kwanza katika mji huo
mkongwe mwaka 1898 wakiongozwa na Kasian
Spiss.Tangu wakati huo wabenediktine hao wamekuwa na wakifanya mambo mazuri na ya kipekee katika
eneo hilo hali iliyosababisha kuutambua Peramiho kuwa ni eneo linalokidhi vigezo kuwa
na utalii wa kihistoria na
kitamaduni.
Mhifadhi kiongozi wa makumbusho ya Taifa Philipo Maligisu
anasema wabenediktine wa Abasia ya
Peramiho wametengeneza historia ya kipekee na kuvutia katika nchi ya Tanzania
ni pale walipoamua kujikita katika suala zima la elimu na kuamua kuwekeza
katika elimu zaidi ya miaka 100 iliyopita hadi sasa.
Wabenediktine hao
walizindua rasmi mji huo Julai 31,1898 na tangu hapo waliendelea na shughuli
zao wakiwa na mahusiano mazuri wakati huo na utawala wa machifu katika eneo
hilo.
Hadi sasa watanzania wengi hapa nchini bado hawajatambua
kuwa eneo la Peramiho lina historia ya kipekee inayowaunganisha wananchi wa
mkoa wa Ruvuma na sehemu nyingine duniani na hasa nchi ya Ujerumani ambao
wanaitambua sana Peramiho.
“Wananchi wa Ujerumani
wanaijua sana Peramiho pengine kuliko hata sisi watanzania,ndiyo
maana kizazi na kizazi wanasafiri kwa
gharama kubwa hadi katika mji huo ili kufanya utalii wa kihistoria kwa
kutembelea katika maeneo mbalimbali ya kihistoria na kujifunza mambo
mbalimbali”,anasisitiza Maligisu.
Sera ya taifa ya utamaduni ya mwaka 1997
ina tamka bayana kuwa eneo lolote
la kihistoria linapokuwa limetimiza miaka 100 moja kwa moja linaingia katika urithi wa
utamaduni wa taifa.
Kutokana na hali hiyo ukiangalia mji huo wa Peramiho tayari
umekidhi vigezo na maeneo yake yote ya kihistoria kuingia katika urithi wa
utamaduni wa taifa kwa ajili ya kujifunza elimu na utalii ndiyo maana makumbusho ya taifa inafanya
mchakato wa kuliingiza eneo la Peramiho katika urithi wa utamaduni wa taifa.
Mwandishi Anapatikana
0755-335051
www.mangokwetu.blogspot.com
Chapisha Maoni