ELIMU BURE NI UKOMBOZI KWA MTOTO WA KIKE NCHINI-MAPUNDA
NA STEPHANO MANGO,SONGEA
MJUMBE wa Kamati ya utendaji ya Taifa ya Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) mkoani Ruvuma, Jema Mapunda ameipongeza serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuamua kutoa elimu bure, ambapo kupitia utekelezaji huo itaweza kuwapa fursa watoto wa kike kupata elimu hiyo hadi sekondari kwa ufanisi mzuri.
Mapunda aliyasema hayo jana wakati wa mafunzo ya Walimu wanawake viongozi wa CWT mkoani hapa, alipokuwa akifungua
mafunzo hayo yaliyohudhuriwa na Katibu wa chama hicho mkoa, Shaibu Mohamed Omary yaliyofanyika mjini hapa.
Alisema kuwa familia nyingi zilikuwa zinasomesha watoto wao kwa kuwapa kipaumbele watoto wa kiume, huku wakike wakibaki
nyumbani kwa kisingizio cha kukosa ada na michango mbalimbali jambo hivi sasa limekomeshwa na Rais Dkt. Magufuli.
Alifafanua kuwa walimu wa kike, wanapaswa kuwa mfano mzuri kwenye maeneo yao wanayofanyia kazi kwa kuwahimiza wazazi
wahakikishe kwamba watoto wao wanawapeleka shule bila kujali kuwa ni wa jinsia gani.
Vilevile alieleza kuwa mafunzo hayo, yanawapa fursa ya kupata elimu ya sheria ya kazi na ujasiriamali ili walimu
hao wanawake toka wanapokuwa kazini wawe wanafanya maandalizi kujijenga kimaisha kabla ya kustaafu na kwamba
baadaye watakapofikia hatua ya kustaafu wasiweze kuwa ombaomba au tegemezi.
Alisema elimu hiyo pia itawawezesha walimu wanawake kupunguza changamoto ya kuwa na madeni mengi yasiyokuwa ya
lazima, na kuwafanya washindwe kutulia kwenye vituo vyao vya kazi na sio vinginevyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa dawati la jinsia na watoto mkoa wa Ruvuma, Mrakibu msaidizi wa Polisi Anna Tembo
alisema kuwa ukatili wa kijinsia unaweza kuwa ni kipigo, ngono zisizokuwa na utaratibu na kufanyiwa vitendo vya
kinyama hivyo aliwataka walimu hao huko waendako wakawe mabalozi wazuri katika maeneo yao ya kazi.
Anna alieleza kuwa vilevile walimu wanapaswa kupinga mfumo kandamizi unaochangiwa kwa kiasi kikubwa kutoa lugha ambazo
sio rafiki kwa jamii, pamoja na mila na desturi kandamizi zipigwe vita.
Alibainisha kuwa walimu wanasaidia kwa kiasi kikubwa kwa mambo mengi, hasa ikizingatiwa kuwa ndiyo wanaokaa kwa muda
mrefu na watoto shuleni tofauti na wazazi wao ambapo wanatakiwa kutoa elimu nzuri kwa wanafunzi hasa wa kike ili
waweze kuendana na maadili mema katika maisha yao yatakayowafanya waepukane na kudanganywa na matendo maovu.
MWISHO.
Chapisha Maoni