KADA WA CHADEMA JOSEPH FUIME
NA STEPHANO MANGO,SONGEA
ALIYEKUWA Mgombea Ubunge kupitia UKAWA katika jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma Joseph Fuime amesimamishwa uanachama wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutokabidhi nakala za matokeo ya uchaguzi kwa uongozi wa chama na kufungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi bila chama hicho kushirikishwa.
Akizungumza na Tanzania Daima jana ofisini kwake mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) wa wilaya ya songea John Mwankina alisema kuwa Fuime amesimamishwa uanachama tangu mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu.
Alifafanua zaidi kuwa Fuime ambaye pia aliwahi kuwa diwani wa kata ya Mjini katika kipindi cha 2010-2015 na aliwahi kuwa mwenyekiti wa chadema mkoa wa Ruvuma amekahidi kukabidhi nyaraka za nakala za matokeo ya uchaguzi wa ngazi ya ubunge wakati akifahamu kuwa yeye ndiye aliyekuwa mgombea na baada ya uchaguzi alitakiwa kutoa taarifa halisi kwenye chama chake lakini mpaka sasa ameshindwa kukutana na uongozi wa chama hicho iliufanye tathmini ya mambo mbalimbali ya shughuli za uchaguzi yaliyokuwa yamejitokeza.
Mwankina alisema kuwa Fuime anadaiwa Oktoba 4 mwaka jana majira ya saa za kazi alifika kwenye ofisi za chama hicho zilizopo katika eneo la Matarawe manispaa ya Songea na alimtolea lugha za matusi katibu wake wa chadema wa wilaya hiyo Olais Beda Ngoison aliyekuwa akimtaka atoe ufafanuzi wa fedha shilling laki 5 zilizokuwa zimetumwa na Afisa wa chama hicho toka makao makuu kwa ajili kufanyia ukarabati wa baadhi ya mapaa ya shule tatu za msingi za Mwembechai, sabasaba na Matarawe ambayo yalibomoka wakati mgombea Uraisi kupitia Ukawa Edward Lowassa alipokuwa kwenye mkutano wa kampeni uliosababisha kuhudhuliwa na mamia ya wakazi wa manispaa ya songea ambapo baadhi yao walilazimika kupanda juu ya mapaa ya shule ili kumsikiliza
Alieleza zaidi kuwa siku hiyo ya tukio baadhi ya watu waliofika kumsikiliza walisababisha mapaa hayo yaweze kubomoka jambo ambalo lilileta usumbufu mkubwa wa kupokea malalamiko mengi toka halmashauri ya manispaa ya songea pamoja na wazazi wa watoto wanaosoma shule hizo kutaka ukarabati huo ufanyike haraka iwezekanavyo na makao makuu walituma fedha hizo za kuanza ukarabati kupitia kwenye simu yake ya mkononi ambapo mpaka sasa uongozi wa wilaya wa chama hicho haujakabidhiwa.
Alisema kuwa pia chama hicho kilimtaka atoe sababu za msingi zilizomfanya afungue kesi ya kupinga uchaguzi kwenye mahakama kuu kanda ya songea ngazi ya ubunge jimbo la songea mjini bila chama kushirikishwa.
Hata hivyo kwa upande wake Fuime alipoulizwa na Tanzania Daima kuhusiana na kusimamishwa kwake uanachama alikiri kuwa chama kimemsimamisha lakini hawezi kusema lolote juu ya tuhuma zote alizopewa kwa kuwa muda bado na ukifika atakuwa na jambo la kuzungumza na alikanusha kuwa hana mpango wa aina yoyote wa kukihama chama licha ya kuwa kuna maneno mengi kuwa ana mpango wa kuhamia chama cha ACT Wazalendo, jambo ambalo alisema ni uzushi mtupu.
MWISHO
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Chapisha Maoni