0
Kulia ni Mbunge wa Songea Mjini, Leonidas Gama. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Thabiti  Mwambungu.mwenye koti jeupe ni mganga mkuu wa Hospital hiyo Dkt Daniel Malekela Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,akimsalimia mtoto
NA STEPHANO MANGO,SONGEA

MADAKTARI na Wahudumu wa afya wanaofanya kazi katika Hospitali ya Rufaa mkoani Ruvuma, wamejikuta wakiwa katika wakati mgumu baada ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, kuwajia juu na kukemea vitendo vya utoaji mimba ambavyo vimeshamiri katika hospitali hiyo.

Hali hiyo ilijitokeza katika ukumbi wa mikutano wa hospitali hiyo, ambapo Waziri Mkuu Majaliwa alimweleza Mganga mkuu, Daniel Malekela kwamba watumishi wake hasa madaktari wamekuwa na mazoea ya kufanya vitendo hivyo hasa kwa wanafunzi wanaosoma shule ya msingi na sekondari.

“Mganga Mkuu, hospitali yako inayosifa ya kutoa mimba, madaktari wamekuwa wakitumia wodi namba tano kufanyia kazi hii sasa natoa onyo kali ni marufuku kuanzia leo, sitaki kusikia tena jambo hili nitawafukuza kazi na kuwafunga”, alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri Mkuu huyo alifafanua kuwa utoaji mimba, umekuwa ukifanyika hata katika jengo la upasuaji lililopo hospitalini hapo na kuongeza kuwa jambo hilo hataki kuliona linarudia tena na kwamba, hatakuwa na msamaha wowote kwa atakayehusika na kitendo hicho.

“Nyiee………… ole wenu, Mganga mkuu na Mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa wa Ruvuma, hakikisheni hili jambo halijitokezi tena, likiendelea nitaanza kuwawajibisha ninyi”, alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu  huyo wakati alipokuwa ametembelea wodi za hospitali ya Rufaa ya mkoa huo, alijionea changamoto mbalimbali ikiwemo uchakavu wa majengo na malalamiko mbalimbali yaliyojitokeza kutoka kwa akina mama ambao walikuwa wakiuguza wagonjwa wao.

Akina mama hao kwa nyakati tofauti walimweleza kuwa wamekuwa wakikaripiwa na kutolewa lugha chafu, kutoka kwa baadhi ya waganga na madaktari wanaowahudumia jambo ambalo limekuwa kero kwao.

“Mmoja wa wagonjwa alimweleza Waziri Mkuu Majaliwa kwamba, “mimi binafsi hapa ninamgonjwa wangu amelazwa lakini naambiwa hakuna dawa nakwenda duka la dawa muhimu kununua ili mgonjwa wangu atibiwe, licha ya kununua dawa husika mganga wa zamu bado anataka nimpatie fedha ili ahudumie mgonjwa wangu je, hapo kuna haki”?, alihoji Rosemary Ngonyani.

Vilevile katika wodi ya watoto, walilalamikia kitendo cha watoto wao ambao ni wagonjwa kulazwa wawili wawili katika kitanda kimoja na kuiomba serikali iangalie kwa jicho la huruma tatizo hilo, ili liweze kupatiwa ufumbuzi.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Majaliwa alimuagiza Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma, Hassan Bendeyeko ahakikishe kuwa mkoa wake unatenga bajeti kwa ajili ya kupata fedha za kukarabati majengo ya hospitali hiyo ya rufaa na ujenzi wa majengo mengine mapya, ili kuweza kukidhi haja na kuondoka na kero ya kulala kitanda kimoja wagonjwa wawili.

Hata hivyo alitoa onyo kwa wanaotoa vifaa vya matibabu vya serikali na kuvipeleka kwenye zahanati, vituo vya afya au hospitali binafsi huku akijua kwamba ni kinyume na utaratibu atakayebainika atachukuliwa hatua ikiwemo kufukuzwa kazi.

MWISHO.

Chapisha Maoni

 
Top