0


MWENYEKITI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA SONGEA RAJABU MTIULA


NA STEPHANO MANGO,SONGEA


BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoa wa Ruvuma limemsimamisha kazi Kaimu Mhandisi wa Idara ya Maji John Undili kwa sababu ya uzembe na kutokuwa makini katika kusimamia miradi mbalimbali ya maji na kuisababishia Halmashauri hiyo hasara ya mamilioni ya fedha


Akitoa taarifa hiyo kwenye Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo juzi Mwenyekiti wa Halmashauri Rajabu Mtiula alisema kuwa Mhandisi Undili amekuwa akionyo mara kwa mara na Baraza na kumtaka asimamie kikamilifu miradi ya maji lakini amekuwa akishindwa kutekeleza wajibu wake


Mtiula ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Litapwasi alisema kuwa Mhandisi Undili alishindwa kusimamia miradi hiyo ya maji katika kipindi cha kuanzia januari hadi disemba mwaka 2015 na kuisababishia halmashauri hasara kubwa ya fedha na kuwakosesha wananchi huduma ya maji


Alisema kuwa Mhandisi huyo alizidisha uzembe zaidi mara baada ya Baraza la Madiwani kuvunjwa mwaka jana na kuelekea kwenye mchakato mpya wa kugombea na kumsababisha yeye kufanya madudu kwenye miradi hiyo


Alifafanua kuwa madiwani baada ya kuchaguliwa na kuapishwa pamoja na wataalamu 6 walitembelea miradi yote ya maji na miradi mingine 13 ili kuweza kuona miradi hiyo ambayo ilitekelezwa wakati madiwani hawapo kuanzia januari 13 hadi 19,2016 na kubaini miradi hiyo kujengwa chini ya kiwango


Alieleza kuwa miradi hiyo ya kijiji cha mpitimbi,matimira,magagura na parangu madiwani wamebaini mapungufu mengi sana katika miradi hiyo mikubwa na kulazimika kumsimamisha kazi kwa muda usiojulikana Mhandisi Undili na kwamba hatua zingine zitafuata dhidi yake kwani kamati ya uchunguzi ipo mbioni kuundwa kwa mujibu wa sheria ili kubaini mapungufu zaidi na mapendekezo watakayoyatoa kuhusu hatua za kisheria na kinadhamu zinazopaswa kuchukuliwa dhidi yake


Alisema kuwa Madiwani wamemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Sixbert Kaijage kumtafuta Kaimu Mhandisi mwingine ili aweze kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo haraka iwezekanavyo ili kuondoa kero kwa wananchi


Akizungumzia jambo hilo mbele ya Madiwani wa Halmashauri Mkurugenzi Mtendaji wa hiyo Sixbert Kaijage alisema kuwa tayari amemwandikia barua ya kumteua fundi sanifu mwandamizi Martha Luhumbi kuwa Kaimu Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo na kwamba majukumu yake yanaanza mara baada ya uteuzi


Kaijage aliwataka watumishi wote wa Halmashauri hiyo kufanya kazi kwa ueledi mkubwa na unaoendana na kasi ya utawala uliopo kwani wananchi wanaimani sana na Serikali yao yao hivyo kila mmoja akitimiza wajibu wake halmashauri itasonga mbele na wananchi watanufaika na serikali yao

MWISHO

Chapisha Maoni

 
Top