0


MBUNGE WA PERAMIHO JENISTA MHAGAMA

NA,STEPHANO MANGO

 JIMBO la Peramiho linaongozwa na Jenista Mhagama kwa tiketi ya chama cha Mapinduzi,likiwa ni jimbo pekee la uchaguzi linaloongozwa na mwanamke miongoni mwa Majimbo saba (7) ya liyopo mkoani Ruvuma . 

Mbunge huyo kwa sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, sera na uratibu wa bunge ambapo kabla ya hapo alikuwa ni Naibu waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi stadi ,akiwa ni Waziri Pekee kutoka Mkoa wa Ruvuma

Jimbo hilo lenye jumla ya kata 23 limeongozwa na Jenista kwa miaka 10 sasa akiwa ndiye mbunge pekee wa jimbo mwanamke ambapo Wakazi wake kama walivyo wapiga kura wa majimbo mengine nchini wanamatumaini ya utatuzi wa kero zao kutoka kwa Mbunge wao hususani katika sekta ya miundombinu,afya,maji,elimu,mawasiliano na uwezeshaji wa kiuchumi

Kufuatia kuwepo kwa dalili njema za mafanikio kwenye sekta mbalimbali kutokana na juhudi anazozifanya Mbunge wa Jimbo hili na ukaribu wake anaouonyesha kwa wapiga kura wake.

Licha ya matumaini waliyo nayo wapiga kura wa Jimbo hili kwa Mheshimiwa Mhagama, baadhi ya wananchi wamepaza sauti zao kuhusu kero zinazowasumbua. Ambazo wanataka zisikike kikamilifu kwa Mbungea wao wa Serikali ili hatua stahiki zichukuliwe kwa malengo ya kuleta ustawi katika maisha yao .

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao ambao ni wakazi wa kata ya Maposeni na magagura wamezilalamikia kero kuu nne za umeme, maji, soko na ushuru mkubwa wanaotozwa kwenye mazao yao pindi wanapoamua kuyauza au kuwapelekea ndugu na jamaa zao wanoishi mjini Songea.

Mkazi wa kata ya Magagura Nestory Ngailo anasema umeme ni tatizo katika baadhi ya maeneo katika  Jimbo hilo kwani wanaofaidika  ni wananchi wachache walio karibu na Peramiho,lakini maeneo mengi hakuna nishati hiyo muhimu

Damas Fuss mkazi wa Peramiho madukani anaongeza kwa kusema, tatizo hili linawafanya washindwe kujikwamua na umasikini wa kipato kwa sababu ya kukosekana kwa nishati hiyo muhimu kiuchumi. 

Hata hivyo, Clemence Mbawala anasema, taatizo la umeme linawafanya kuishi kwa kubahatisha kutokana na eneo hilo kukimbiwa na wawekezaji licha ya jimbo hilo kuwa na historia kubwa kitaifa na kimaifa. 

Hali hiyo iinawafanya wajione wametengwa kutokana na tatizo hilo kutoshughulikiwa kwa muda mrefu licha ya kero yenyewe kutambulika na kila kiongozi alisema Bw. Mbawala. 

 Ingawa Fussi na Mbawala walionyesha kuridhishwa na jinsi Mbunge wao anavyoonyesha azma ya kweli katika kushughulikia suala la ujenzi wa Shule, barabara na upatikanaji wa walimu wa kutosha katika shule za maeneo yao . 

 Kwa upande wa wakazi wa kata ya Parangu na Nakahuga wameeleza kuwa katika maeneo yao na ya jilani hakuna mtandao wa majisafi na salama, mawasiliano ya simu ni shida, ukosefu wa soko la uhakika la kuuzia mazao yao.

Hali ambayo inawalazimu kuuza mazao yao kwa walanguzi ambao huwanyonya kwa kununua bei za chini zaidi na endapo wakitaka kuepukana na walanguzi hao. Hukumbana na ushuru mkubwa wa Tshs. 2,000/= hadi 3,000/= kwa gunia moja la mazao ya kilimo kwenye vituo au mageti ya ukaguzi kutoka kwa maafisa wa serikali wasio waaminifu anasema Paulo Haule mkazi wa kata ya Parangu.

Kwa upande wa huduma ya maji kwa baadhi ya maeneo imekuwa ni kitendawili kisichopatiwa ufumbuzi kwa muda mrefu kutokana na kukosekana kwa mikakati ya kulimaliza tatizo hilo licha ya kero kuvumiliwa kwa miaka mingi. 

Naye Aloyce Komba anasema kero niyo ya maji ni tatizo kubwa ambalo linaonekana kusahaulika kwa viongozi wao kwa miaka mingi licha ya Mbunge wao kuwaahidi kulipatia ufumbuzi tatizo

Komba anasema kitendo cha kufuata maji umbali mrefu na wakati mwingine kuvikuta visima vya maji hayo vimekauka kutokana na wakazi wengi kuvitegemea kunachelewesha kuleta maendeleo kwani muda mwingi wanaupoteza kwenye kusaka maji. 

Hata hivyo, wakati wakilalamikia kero hizo kwa upande mwingine wakazi wa Jimbo hilo wamepongeza juhudi za Mbuge wao za kupambana kwa dhati kuwaletea miundombinu ya kujiletea maendeleo.

Hasa Kwa masuala yanayoonekana kuwa ni kikwazo kwao na kueleza jinsi sekta ya elimu, barabara, na afya zilivyopatiwa ufumbuzi na Mbunge wao ,ingawa walimtaka Mbunge wao kuongeza juhudi katika sekta za maji, umeme, soko la uhakika ili wawe na sehemu ya kuuzia mazao yao na hatimaye kupata pesa kwa ajili ya kufanikisha ndoto yao ya kuwa na maisha bora kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo aliinadi vyema na kusababisha kutwaa jimbo hilo 

Ukiweka kando hilo , baadhi ya maeneo ya jimbo hili hakuna mawasiliano ya simu kwani kabla ya kampuni ya simu ya Celtel haijabadilishwa na kuitwa Zain angalau mawasiliano yalikuwa yanapatikana kwa mbali.

Hata hivyo Akijibu kero hizo kwa lengo Mbunge wa Jimbo la Peramiho Jenista Mhagama alisema kwa kipindi cha miaka 9 ya ubunge wake amejitahidi kutekeleza ahadi zake muhimu alizowaahidi ambazo zilikuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo na kero kubwa kwa wakazi wa Jimbo hilo . 

Kwa upande wa mawasiliano ya simu kwenye kata chache ambako hamna hamewaomba wapiga kura wake wavute subira kidogo kwani ameshapeleka malalamiko kwenye makampuni husika na wameahidi kuongeza mitambo ili mawasiliano yawafikie kwa urahisi. 

 Akizungumzia kero ya soko na ushuru mkubwa anasema ameichukua kama changamoto na muda sio mrefu litakuwa limetatuliwa na mamlaka husika kwani tayari mipango iko tayari ya kulitatua jambo

Hata hivyo, amewaomba wapiga kura wake waamini kuwa yeye ndiye mtumishi na mkombozi wao na kero hizo anazitambua na ameanza kuzitatua kwani kuna kero zingine zinahitaji mikakati ya muda mrefu.

 Ingawa amewashukuru wapiga kura wake kwa kumkumbusha baadhi ya kero ambazo anatakiwa awatatulie na amewataka wasiwe na hofu kwani anawaahidi kuyatekeleza yote aliyoyaahidi

Mhagama alisema kuwa Jimbo la Peramiho ni kubwa sana na jiografia yake ni mbaya kutokana na hali hiyo wananchi wengi walikuwa hawafikiwi na huduma muhimu za Serikali lakini kwa sasa hali hiyo imebadilika na kwamba huduma muhimu zote zinapatika

Alisema ujenzi wa Halmashauri ukikamilika kwenye kata ya Maposeni kutamaliza kero ndogo ndogo zilizobakia kwani wananchi watakuwa jilani na halmashauri yao na kwamba kazi kubwa itakayokuwa imebaki ni kupigania jimbo hilo liwe Wilaya ili kusogeza huduma zaidi kwa wananchi

Mwandishi wa Makala haya
Anapatikana 0715-335051
www.mangokwetu.blogspot.com
MWISHO
 
 

Chapisha Maoni

 
Top