KADA WA CHADEMA FREDIRICK FUSSI AKITANGAZA NIA YA UBUNGE JIMBO LA SONGEA MJINI
NA STEPHANO MANGO,SONGEA
AFISA Mshauri Mwelekezi wa masuala ya Uchumi, Biashara na Uongozi Fredirick Fussi ambaye pia ni kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ametangaza nia ya kutaka kugombea ubunge wa jimbo la Songea Mjini kupitia Chama hicho ambapo ameeleza kuwa endapo atafanikiwa kuwa Mbunge atauondoa ukiritimba uliopo hivi sasa ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambayo alidai imekithiri kwa ubadhirifu kwa mamilioni ya fedha.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mchana kwenye Hotel ya Agopal ya mjini Songea Fussi amesema kuwa ameamua kutangaza nia ya kutaka kugombea jimbo hilo akiwa na lengo la kutaka kurudisha umiliki wa halmashauri ya manispaa ya songea mikononi mwa wananchi wenyewe tofauti na ilivyo hivi sasa.
Alisema kuwa matamanio ya wapiga kura ni kutaka kuitambua halmashauri yao jinsi inavyoweza kuwasaidia katika shughuli mbalimbali za maendeleo pamoja na huduma za jamii katika kupunguza matatizo yanayowakabili wananchi wa jimbo hilo.
Kada huyo wa CHADEMA alisema kuwa katika utendaji wake atazingatia mahitaji ya makundi yote ndani ya jamii ikiwemo kufuatilia fedha za miradi mbalimbali ambayo imekuwa ikitekelezwa kwa kiwango cha chini kwa uongozi uliopo hivi sasa ambao tayari ulishaanza kulalamikiwa na wananchi.
Fussi ambaye amedai kuwa ana elimu ya Shahada ya kwanza katika fani ya Uchumi na uongozi wa siasa ambayo aliipata kwenye chuo kikuu cha Mwalimu Nyerere alisema kuwa uchunguzi alioufanya kwa zaidi ya miaka miwili amebaini kuwa ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuna ubadhilifu wa fedha shilingi milioni 513 uliotokana na malipo yasiyo idhinishwa, manunuzi ya kifisadi yasifuata sheria za manunuzi na manunuzi yaliyofanywa bila ushindani wa bei.
Alisema kuwa licha ya kuwepo ubadhilifu ndani ya manispaa hiyo bado kumekuepo na tatizo la miundo mbinu ya barabara pamoja na usafi wa mazingira ambao umeonekana kuwa ni kero kubwa kwa wakazi wa manispaa ya songea.
Amesema kuwa wananchi wakimpa ridhaa ya kuwawakilisha kwenye Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania atajitahidi kutengeneza fursa za ajira hasa kwa makundi mbalimbali yakiwemo ya vijana na akina mama kwa kuishawishi serikali ianzishe viwanda ikiwa ni pamoja kuwatafuta wawekezaji wafike songea kuwekeza kwa maswala mabalimbali yakiwemo ya utalii kwa kuwa jimbo hilo limeshakuwa na sehemu za kumbukumbu ya mashujaa vita ya majimaji.
Aidha kada huyo wa Chadema Fussi amekuwa wa pili kutangaza nia ya kugombea Jimbo la songea mjini ambapo wa kwanza ni aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo ( CHADEMA) mkoa wa Ruvuma Joseph Fuime ambaye Oktoba mwaka jana akiwa kwenye mkutano wake wa hadhara uliofanyika kwenye soko kuu la songea alitangaza nia ya kutaka kugombea Ubunge kwenye jimbo hilo oktoba 2015.
MWISHO
Chapisha Maoni