0

Na Steven Augustino,
Tunduru.

WAKULIMA katika kata ya Muhuwesi, wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma wamewataka watendaji katika vijiji vya wilaya hiyo, kujenga ushirikiano wa karibu ili kuweza kusukuma mbele maendeleo yao. 

Rai hiyo ilitolewa na wakulima wa Chama cha ushirika cha Mumsasichema AMCOS, walipokuwa kwenye kikao chao cha wadau wa zao la korosho kilichofanyika katika ofisi za chama hicho kijiji cha Muhuwesi wilayani humo.

Mwenyekiti wa chama hicho, Issa Kambutu alifafanua kuwa kutokana na kuwepo kwa mmomonyoko mkubwa wa maadili ikiwemo kukithiri kwa vitendo vya wizi wa fedha za wakulima wa zao hilo, ukifanywa na baadhi ya viongozi hao sasa kuna kila sababu kujenga ushirikiano ili kuweza kudhibiti hali hiyo.


Kambutu alisema vitendo hivyo vya wizi vinafanyika hasa kipindi cha msimu wa zao hilo, ambacho ushuru hukusanywa na kwamba aliwataka kuwa na uzalendo ambao utaifanya hata Halmashauri ya Tunduru kuwa na mapato makubwa.

Watendaji hao wa vijiji, wanadaiwa kushirikiana na wanunuzi binafsi kufanya biashara ya kununua korosho kwa kuingia uwakala na makampuni binafsi ambayo ndiyo husuka mipango ya kupoteza mapato ya halmashauri na kuwanyonya wakulima wa zao hilo.

Awali akisoma taarifa ya mapato ya ununuzi wa korosho katika msimu wa mwaka wa 2013/2015 mwandishi mkuu wa AMCOS hiyo, Said Akimu aliwaeleza Wajumbe wa mkutano huo kuwa chama chao kilifanya manunuzi ya kilo 378,648 zenye thamani ya shilingi milioni 454,377,600 kiasi ambacho alidai kuwa ni kidogo hakilingani na hali halisi ya uzalishaji unaofanywa na wakulima wa wilaya hiyo.


Hali hiyo imeelezwa kuwa imetokana na viongozi husika kutotimiza wajibu wao ipasavyo, ikiwemo kusimamia mapato ya chama kuhakikisha kwamba hayachakachuliwi ili kuweza kufikia malengo.

Chapisha Maoni

 
Top