0
Mratibu wa shughuli hizo za kilimo hifadhi Abiudi Gamba

NA STEPHANO MANGO,SONGEA

WAKULIMA nchini wametakiwa kuiga teknolojia mpya ya kilimo hifadhi na elimu ya urutubishaji wa udongo kwa kuwa kilimo hicho kinaboresha afya ya udongo ambayo itaweza kuzalisha mazao kwa wingi na yenye ubora tofauti na uzalishaji wa mazao wa hivi sasa ambao unategemea mbolea za viwandani na si vinginevyo.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Songea Wensaria Swai kwenye maadhimisho ya siku ya wakulima iliyoandaliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya mtandao wa kilimo Hifadhi Afrika (ACTN) yaliyofanyika katika kijiji cha Madaba wilayani Songea na kuhudhuriwa na wakulima toka maeneo mbalimbali ya halmashauri hiyo na mikoa jirani.

Swai alisema kuwa umuhimu wa kilimo hifadhi katika kupunguza gharama za uzalishaji na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi yanasaidia kupunguza changamoto za gharama za ununuzi wa pembejeo pamoja na muda wanaotumia kwenye kilimo chao ambacho kimekuwa kikidhohofisha nguvu za wakulima.

“Ndugu zangu wakulima hasa viongozi wa vikundi na mashamba darasa niwaombe  muwe mabalozi wazuri katika kusambaza elimu ya kilimo hifadhi na urutubishaji wa udongo ambayo mkiielewa vizuri itaweza kuleta tija kubwa kwenu pamoja na serikali kwa ujumla.’’alisema Swai.

Kwa upande wake Afisa ugani wa tasisi hiyo wa kanda ya nyanda za juu kusini ambaye pia ni Mratibu wa shughuli hizo za kilimo hifadhi Abiudi Gamba alisema kuwa kilimo hifadhi ni njia pekee na mbadala ya kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao mbalimbali yakiwemo mahindi ,soya,maharage na mpunga.

Hata hivyo amezitaja changamoto wanazokutana nazo wakati wa kutoa elimu ya kilimo hifadhi kuwa ni uwelewa mdogo wa wakulima juu ya elimu hifadhi pamoja na ukosefu wa maafisa ugani katika baadhi ya vijiji mradi unapofanyika.

Aidha mradi huo ambao unatekelezwa kanda ya nyanda za juu kusini kwenye mikoa ya Iringa unatekelezwa katika Wilaya ya Kilolo ,Njombe katika Wilaya ya Ludewa na Ruvuma katika Wilaya za Namtumbo na Songea vijijini.

MWISHO.

Chapisha Maoni

 
Top