Na Mwandishi Wetu, Namtumbo
MFEREJI
wa maji uliojengwa kwa fedha za Serikali kwa ajili ya
kilimo cha umwagiliaji katika Kijiji cha Namahoka Kata
ya Ligera Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma wadaiwa umesombwa
na maji ya mvua iliyonyesha hivi karibuni.
Mwenyekiti wa
kikundi cha Songambele kinachojengewa mradi huo, Gaudens
Komba amesema kuwa mfereji huo umesombwa na maji kutokana
na tuta lililowekwa na Mkandarasi kukinga mfereji huo lilikuwa dogo
na baadhi ya sehemu ya mfereji huo zilititia.
Komba
alisema kuwa hiyo ni mara ya pili sasa kwa mfereji
huo kutokea dosari kwani mwaka 2007 mwezi mei
Serikali ilitumia shilingi milioni 67 kujenga mfereji huo
chini ya kampuni ya Legele civil works iliyokuwa
ikimilikiwa na Dastan Mtembele ambapo kabla ya kukamilika kwake
mfereji huo ulititia na kushindwa kupitisha maji kwenda
mashambani.
Aliongeza kuwa
pamoja na hayo Serikali ilitenga tena fedha kiasi cha milioni 297
kwa ajili ya kufanya marekebisho ya mfereji huo kwa
kuipatia tenda kampuni ya Modspan chini ya usimamizi wa
Ernest Mbawa kufanya kazi ya kuurekebisha mfereji huo ambapo
mpaka sasa kampuni hiyo imelipwa milioni 83 na baadhi ya sehemu
iliyofanyiwa marekebisho imesombwa na maji na zingine kutitia.
Fundi mkuu msaidizi anayejenga mfereji huo Shafii Magoto alisema kuwa sehemu iliyosombwa na maji imetokana na mkandarasi kuweka tuta dogo la kukinga mfereji huo na kuruhusu maji ya mvua kusomba tuta hilo kiurahisi na kuufanya mfereji huo kuvunjika.
Hata
hivyo Magoto alisema kuwa ujenzi wa mfereji huo umesimama kwa muda wa
miezi sita sasa kutokana na wao kutolipwa fedha yao kutoka kwa mwajiri wao
Ernest Mbawa na wanaishi katika mazingira magumu na wanashindwa kurudi kwao
kutokana na kukosa fedha za kurudia na hivi sasa wanajikita
katika kufanya kazi binafsi ili kujipatia fedha ya kula .
Mkandarasi
Mbawa kwa upande wake anawalalamikia viongozi wa kikundi cha
Songambele kwa kumcheleweshea kumwizinishia kuchukua fedha kwa wakati ili
aendelee kujenga mfereji huo na badala yake viongozi hao
hupenda kuendeleza malumbano na kuingiza migogoro isiyokuwa ya
lazima na kutumia muda mwingi kushughulikia migogoro inayoibuka kila
kukicha ndani ya kamati.
Mbawa aliwataka
viongozi wa kamati kumwizinishia fedha ili arekebishe sehemu iliyosombwa na
maji ya mvua na kuwalipa mafundi wake na waendelee na kazi.
Baadhi ya
wanakikundi wakiwemo Mohamedi Mangambila na Mohamedi Akida waliuambia
mtandao huu kuwa wamechoshwa na utendaji kazi wa Mkandarasi huyo walidai kuwa
wataandika barua kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Namtumbo kuomba kusimamisha mkataba wake kwa hoja ya kushindwa kujenga mradi huo
kwa wakati kuendelea kujenga mradi huo nje ya mkataba na pia mkandarasi
kutokuwa na mahusiano mazuri na kamati.
Mhandisi wa
halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Izakiel Nyirenda amethibitisha kuwepo
na mgogoro katika mradi huo na kusema kuwa sababu kubwa inayofanya mradi huo
kuyumba ni viongozi wa kikundi kuiona fedha katika mradi huo ni kubwa na
kwa namna fulani wanataka nao wapate mgao hali inayopelekea kuwepo na migogoro
katika mradi huo kila kukicha na mkandarasi kulazimika kutofanya kazi kwa
muda mrefu na kutotaka kumwizinishia fedha iliaendelee kujenga
mradi huo.
Nyirenda alidai kuwa sehemu ilisombwa na maji inarekebishika kwa haraka na kuruhusu maji kupita kama kawaida licha ya wanakikundi hao kutomtaka Mkandarasi huyo kwani wanakikundi wenyewe ndio waliopendekeza jina la Kampuni ya MODSPAN Inayosimamiwa na Ernesti Mbawa kujenga mradi huona kuziacha kampuni zingine nne zilizoomba kujenga mradi huo alisema nyirenda.
Kampuni ya MODSPAN ilisaini mkataba wa miezi sita toka tarehe30 mwezi novemba mwaka 2011 wa kurekebisha mfereji huo ambapo mpaka mei 2012 mkataba wake uliisha na wanakikundi inaonesha wazi hawakuridhika na utendaji kazi wa mkandarasi huyo na walifia uwamuzi wa kumwandika barua mkurugenziwa halmashauri ya wilaya hiyo ya kutaka kumsimamisha mkandarasi huyo na ndipo mgogoro ulipoanzia na mradi huo ukasimama mpaka hivi sasa. Mradi wa ujenzi wa mfereji huo umesimamisha kilimo cha umwagiliaji katika eneo hilo na kuwaacha wananchi kuziba mito kienyeji na kuendesha kilimo cha umwagiliaji kwa kujichimbia mifereji yao wenyewe na kuendesha shughuliza kilimo cha umwagiliaji.
Hata hivyo mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Steven Nana alipohojiwa na Mtandao huu kuhusiana na mgogoro wa mradi huo wa kilimo cha umwagiliaji alikili kuwa matatizo yapo lakini hawezi kuelezea lolote mpaka awepo ofisini kwake ambako angedai kuwa angeweza kupata ufafanuzi mzuri kutoka kwa maafisa wake wa kilimo na si vinginevyo.
MWISHO
Chapisha Maoni