0

NA STEPHANO MANGO,SONGEA


JUMLA ya vituo 216 vimetengwa kwenye jimbo la Peramiho lililopo katika Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma kwa ajili ya kupigia kura katika uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.


Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jana kwa niaba ya msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo Sixbert Valentine,Afisa uchaguzi wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Furaha Mwangakala,alisema maandalizi kwa ajili ya uchaguzi huo yamekamilika.


Mwangakala alifafanua kuwa katika kila kituo kutakuwa na wapiga kura 450 kwa lengo la kupunguza msongamano na kutoa fursa kwa wananchi wote wa jimbo hilo waliojiandikisha waweze kupiga kura bila ya kupata adha yeyote.


Aidha alisema kuwa kufuatia zoezi hilo jumla ya watu 67,334 wa jimbo la Peramiho wenye sifa ya kupiga kura wamejiandikisha miongoni mwao yakiwemo makundi maalum mbalimbali ya wazee,vijana wanawake kwa wanaume kwa ajili ya kutumia haki yao ya msingi ya kuwachagua viongozi wao.


Hata hivyo alieleza kuwa kwa upande wa maandalizi kwa ajili ya uchaguzi mkuu yanaendelea vizuri kwa madai kuwa mpaka sasa jumla ya wasimamizi wa uchaguzi 800 wameteuliwa,maboksi ya nyongeza ya bluu 40,meusi 40 na meupe 40 tayari yamekwisha wasili.


Afisa uchaguzi huyo aliendelea kuvitaja vifaa vingine vilivyowasili kuwa ni mabango ya hadhari,mabango ya vituo,mabango yamshale,nyembe za kukatia lakili,betrii za taa,vitabu vya maelekezo kwa watakaosimamia uchaguzi pamoja na fomu kwa ajili ya mafunzo ya wasimamizi wa vituo na makarani.


Mwangakala aliongeza kusema kuwa  kwa upande wa makundi maalum hususan kwa  watu wasioona tayari wamekwisha waandalia karatasi maalum za kupigia kura pamoja na kuwatengenezea utaratibu mzuri  wazee na akina mama wajawazito katika kupiga kura ili wasisimame kwa muda mrefu  vituoni kwa lengo la kuwaondolea uchovu


Hata hivyo baadhi ya wananchi wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili walisema kuwa wanashindwa kuelewa kutokana na matamko mbalimbali yaliyotolewa yakiwemo ya baadhi ya vyama vya siasa kuwaambia wafuasi wao kuwa wakipiga kura lazima wazilinde,sheria ya tume inasema piga kura kisha simama umbali wa mita 100 na vyombo vya dola vinasema piga kura rudi nyumbani hivyo hawaelewi wafuate ipi.


MWISHO

Chapisha Maoni

 
Top