0



MAMA REGINA LOWASSA AKIONYESHA ALAMA YA VEMA

NA STEPHANO MANGO, SONGEA



WAPIGA KURA nchini wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuzilinda mpaka matokeo yatangazwe na mamlaka husika kwenye vituo vyao ili waweze kujua hatma ya wagombea wao kwenye ngazi ya udiwani na ubunge nchini



Wito huo umetolewa jana na mke wa mgombea Urais kupitia umoja wa katiba ya wananchi(UKAWA) Regina Lowassa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja wa wazi vilivyopo kata ya Bombambili katika halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma



Regina alisema kuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995,2000,2005 na 2010 wapiga kura walilinda kura zao kwa amani na utulivu hata hivyo kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 kwa kutumia utaratibu kama wa awali na kwa sheria zilizile wanatakiwa kulinda kura zao bila kuingiliwa na mamlaka yoyote ya dola kwani kura hizo ni haki ya wananchi na sio mali ya Serikali



Alisema kuwa wananchi kwa kulinda kura zao wataondokana na fikra za hofu ya gori la mkono ambalo limekuwa likitamkwa na viongozi waandamizi ndani ya chama cha mapinduzi (Ccm) na badala yake wajitokeze kwa wingi kupiga kura na kuzilinda mpaka matokeo yatangazwe



Alifafanua kuwa wananchi wengi wanataka mabadiliko ya dhati ya kimfumo na kimaendeleo hivyo ni muhimu kutumia haki ya kidemokrasia kujitokeza na kupiga kura ili kupata viongozi makini kutoka kwenye Ukawa kwa maendeleo ya watanzania kiujumla



“Nawaomba akina mama wenzangu tushirikiane kikamilifu kufanya mabadiliko ya kweli katika uchaguzi wa mwaka huu ili tuweze kuzijenga familia zenye misingi bora ya kiafya, kielimu, kimiundombinu, kiuchumi na kiutawala ili tuwatendee haki vizazi vijavyo” alisema Regina



Alisema kuwa hakuna mtanzania ambaye haelewi uadilifu na uchapakazi wa Edward Lowassa kwenye nafasi mbalimbali alizopata kushika huko nyuma na namna wagombea wa Ukawa walivyokuwa wachapakazi hivyo ni vyema wagombea hao wakatendewa haki ya kuchaguliwa ifikapo octoba 25 mwaka huu ili waweze kutuletea Tanzania mpya



Kwa upande wake mgombea ubunge wa Jimbo la Songea Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Joseph Fuime aliwaomba wananchi wamsaidie kwa nguvu zote kuwapigia kura wagombea wanaotokana na ukawa ili iwe lahisi kufanya nao kazi kwani kwenye kata nyingi za jimbo hilo wameonyesha nia ya kuwachagua wagombea wa ukawa



Fuime alisema kuwa kura zikiwa nyingi hata kama wataiba bado ushindi utapatikana kwa wagombea wa Ukawa kwani wamekuwa na dhamira ya dhati ya kutatua changamoto za jimbo hilo na kwamba kwa upande wa mgombea urais Edward Lowassa ambaye ni kipenzi cha watanzania yupo tayari kupambana na umaskini na mifumo chakavu ya elimu



Naye Mgombea Ubunge wa Jimbo la Namtumbo kupitia chama cha Wananchi (CUF) Bonifansia Mapunda alisema kuwa wananchi wa jimbo la Namtumbo wako tayari kwa mabadiliko na wagombea wote wa ukawa wanatosha hivyo wananchi wasipoteze muda wao kusikiliza propaganda za Cccm



Mapunda alisema kuwa wapiga kura watumie haki yao ya msingi kuwapigia kura ili waweze kuleta mabadiliko ya kweli kwani sie maneno kidogo na kazi zaidi hivyo tambo za Ccm za kupiga push up na maneno ya kejeri kwa wagombea wa ukawa hayana nafasi yoyote katika ushindi



Alisema kuwa wanachokifanya wanaukawa ni kutengeneza ushindi uliodhahiri kwani wamechoka na ahadi hewa huku wananchi wakiendelea kuteseka na kuburuzwa zaidi ya miaka 50 ya uhuru bila kuonja matunda yatokanayo na uhuru



Awali Mwenyekiti wa Baraza la wanawake Chadema(Bawacha) mkoa wa Ruvuma Mariam Mtamike akifungua mkutano huo alisema kuwa wanawake wa chadema kwenye uchaguzi wa mwaka huu wako makini kuhakikisha ushindi unapatikana kwa wagombea wa ngazi zote kwenye mkoa wa Ruvuma



Mtamike alisema kuwa kwa kipindi kirefu Ccm imekuwa ikiwaonga akina mama chumvi, kofia, vilemba na furana bila kuwapa viatu au mboga za kuungia hiyo chumvi hivyo tumechoka na ulaghai wao na sasa tunatembea kifua mbele tukiyafuata mabadiliko

MWISHO






Chapisha Maoni

 
Top