DED MADABA AWATAKA WATENDAJI KUWAJIBIKA KATIKA MAENEO YAO YA KAZI
MKURUGENZI Mtendaji Halmashauri ya Madaba Robert Mageni
NA STEPHANO MANGO,MADABA
MKURUGENZI Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, Robert Mageni amewataka watendaji wa vijiji, mitaa na kata katika wilaya hiyo kushughulikia matatizo ya wananchi katika maeneo yao ya kazi, na sio kuwaacha wakitaabika peke yao bila kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Mageni alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na Madiwani wapya na Mbunge mteule wa Jimbo la Madaba, Joseph Mhagama wakati wa baraza la madiwani lilofanyika jana kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya kijiji cha Madaba
Alisema jimbo hilo ni jipya, hivyo linahitaji viongozi waliochaguliwa kuwa na mshikamano ili waweze kuboresha huduma za kijamii, ambapo alitolea mfano kama vile ujenzi wa vyumba vya maabara kwa shule za sekondari.
Mkurugenzi huyo alisema, watendaji wa serikali hawapaswi kulalamika badala yake wao ndiyo wanatakiwa kuwa mfano wa kuigwa na kuchukua hatua madhubuti, kumaliza kero za wananchi katika maeneo yao.
Aidha aliwataka watumishi hao kuwa na ushirikiano na madiwani walioteuliwa kuongoza kata zilizopo ndani ya wilaya ya Madaba, kwa kusimamia shughuli za maendeleo ya wananchi na kuwachukulia hatua za kisheria watu wanaoharibu mazingira ikiwemo ukataji miti na uchomaji misitu hovyo, ambao husababisha kuharibu na kupungua kwa vyanzo vya maji.
Chapisha Maoni