NA STEPHANO MANGO,SONGEA
BAADHI ya Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea
wamevitaka vikao vya uteuzi wa nafasi ya Umeya wa Halmashauri hiyo ndani ya
Chama cha Mapinduzi kuwatendea haki wagombea wenye sifa ya kuiongoza
halmashauri badala ya kuwabeba wagombea ambao hawana sifa
Wakizungumza kwa nyakati tofauti madiwani hao ambao
hawakutaka majina yao yatajwe walisema kuwa imebainika kuwa kuna baadhi ya
vigogo ndani ya chama kuwapeba baadhi ya wagombea kwa maslahi yao binafsi
badala ya kuangalia uwezo na sifa za wagombea hao
Walisema kuwa wapo madiwani ambao wana sifa nzuri za
kuiongoza halmashauri hiyo lakini vikao vya chama vinawapa alama mbovu kwa
sababu ya ukabila na kulinda maslahi yao hali ambayo itaathiri mchakato wa
uchaguzi mara baadha ya kamati kuu kuu kurudisha majina matutu ili yapigiwe
kura na kamati ya madiwani ya Ccm
“Madiwani tunataka vikao vitende haki kwa wagombea wenye
sifa katika mchakato wa kumpata kiranja wetu, kama kama mbunge au kigogo yoyote
atatuchagulia mtu wake kamwe kwenye uchaguzi tutamkataa na kumyima kura kama
ilivyofanyika mwaka 2005 na mwaka 2012 na endapo mamlaka inayohusika
italazimisha jambo hilo basi ieleweke wazi kuwa baraza la madiwani halitatawalika
na kupelekea maendeleo kudorora kutokana na chuki zitakazojitokeza miongoni mwa
madiwani ” Walisema
Walifafanua kuwa mwaka 2012 kulifanyika uchaguzi wa nafasi
hiyo lakini madiwani walimkataa mgombea na mamalaka zinazohusika zikalazimisha
Charles Mhagama awe Meya wakati hakuchaguliwa leo Halmashauri imekuwa katika
hali mbaya kiuchumi na kimaendeleo kuliko halmashauri zote za mkoa wa Ruvuma
kutoka na uongozi mbovu na chuki zilizojengeka miongoni mwa madiwani
Walieleza kuwa kanuni zinamtaka mgombea wa Umeya awe na
elimu ya kidato cha nne na kuendelea lakini tunashangaa kwenye mchakato huu
wapo wagombea wasiokidhi kiwango hicho cha elimu na vikao vinawabeba na kuwapa
alama nzuri
Walisema kuwa kwa hali ilivyokuwa kwenye halmashauri ya
Manispaa ya Songea kunahitaji kumpata kiongozi ambaye ana dhamira ya dhati ya
kuwatumikia wananchi na kuweka mipango stahiki ya kuifanya Halmashauri kuwa
bora kihuduma kwa wananchi na kwa kutambua kuwa Manispaa hiyo ni kitovu au uso
wa mkoa wa Ruvuma
Walisema ni muhimu sana kumpata kiongozi mzalendo na mwenye
moyo wa kushawishi wananchi waipende, waithamini, wailinde na wajivunie
halmashauri yao na awe kiungo muhimu kati ya madiwani na wananchi wao ambao
kimsingi kwa miaka mitatu iliyopita Serikali na wananchi walichukiana kutokana
na mahusiano mabovu yaliyojitokeza kwenye mchakato wa uchaguzi wa nafasi ya
umeya ulioziba nafasi ya Marehemu Ally Manya na kumuibua Charles Mhagama ambaye
hakuchaguliwa kutokana na mizengwe
Walieleza kuwa kiongozi ambaye ana hubiri udini au ukabila
sio kiongozi mzuri kwani akifanikiwa kuwatenga wananchi kwa dini zao au ukabila
wao atajenga tabaka kubwa ambalo mwisho wake ni kuvuruga amani na misingi ya
upendo miongoni mwa jamii
Alipotafutwa na gazeti hili Katibu wa Ccm Mkoa wa Ruvuma
Verena Shumbusho ili aweze kujibu malalamiko ya Madiwani simu zake za kiganjani
zilikuwa hazipatikani na alipotafutwa Katibu Msaidizi wa Mkoa aliyejitambulisha
kwa jina la Ngalawa alisema kuwa yeye sio msemaji wa chama na bosi wake hayupo
kwani amelazwa katika Hospitali ya Misheni ya Peramiho
Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa
majina ambayo walichukua fomu ya kugombea nafasi hiyo na yanajadiliwa kwenye
vikao vya Ccm mkoa kabla hayajapelekwa kwenye kamati kuu Taifa kwa maamuzi
zaidi ni Golden Sanga diwani wa Kata ya Bombambili,Yobo Mapunda Diwani wa Kata
ya Lilambo, Lutengano Izack Diwani wa Msamala, Abdul Mshawej Diwani wa Kata ya
Subira, Musa Mwankaja Diwani wa Kata ya Mateka na Osmund Kapinga Diwani wa Kata
ya Mwengemshindo
MWISHO
Chapisha Maoni