0

MGOMBEA UMEYA SONGEA GOLDEN SANGA

NA STEPHANO MANGO,SONGEA

KADA wa Chama cha Mapinduzi na Diwani wa Kata ya Bombambili Golden Sanga (Sanga One) amechukua na kurudisha fomu ya kugombea nafasi ya Umeya wa Manispaa ya Songea katika kipindi cha 2015 hadi 2020

Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye viwanja vya Ofisi ya Ccm Wilaya ya Songea mgombea huyo alisema kuwa ameamua kuchukua na kurudisha fomu kwani amejipima na amejiona anatosha kuwa kiranja wa madiwani

Alisema kuwa kwa hali ilivyokuwa kwenye halmashauri ya Manispaa ya Songea kunahitaji kumpata kiongozi ambaye ana dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi na kuweka mipango stahiki ya kuifanya Halmashauri kuwa bora kihuduma kwa wananchi

Alifafanua kuwa ni muhimu sana kumpata kiongozi mzalendo na mwenye moyo wa kushawishi wananchi waipende, waithamini, wailinde na wajivunie halmashauri yao na awe kiungo muhimu kati ya madiwani na wananchi wao

Alisema kuwa kiongozi ambaye ana hubiri udini au ukabila sio kiongozi mzuri kwani akifanikiwa kuwatenga wananchi kwa dini zao au ukabila wao atajenga tabaka kubwa ambalo mwisho wake ni kuvuruga amani na misingi ya upendo miongoni mwa jamii

“Nilipokuwa diwani mwaka 2005 hadi 2010 nilikuwa mwenyekiti wa kudumu wa kamati mbalimbali za halmashauri na niliweza kufanikisha mambo mbalimbali kwa maendeleo ya Halmashauri hivyo naifahamu na nimeitumikia halmashauri kwa misingi hiyo natosha kuwa Mstahiki Meya” Alisema Sanga

Naye Katibu wa Ccm Wilaya ya Songea Juma Mpeli alisema kuwa mchakato wa utoaji wa fomu na urudishaji umeanza novemba 29 na utakamilika Disemba 1 mwaka huu na baada ya hapo kutakuwa na vikao vya chama ngazi ya wilaya na ngazi ya Mkoa kwa ajiri ya mapendekezo na kasha majina hayo yatapelekwa kwenye kamati kuu ya Taifa kwa hatua zingine kabla ya madiwani kupiga kura

Mpeli alisema kuwa mpaka sasa waliochukua fomu ya kuomba nafasi ya umeya ni wanne ambao ni Golden Sanga diwani wa Kata ya Bombambili,Yobo Mapunda Diwani wa Kata ya Lilambo, Lutengano Izack Diwani wa Msamala na Abdul Mshawej Diwani wa Kata ya Subira
MWISHO




Chapisha Maoni

 
Top