0



NA STEPHANO MANGO,SONGEA

IDARA ya elimu msingi kitengo cha Taaluma katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imetupiwa lawama kwa kile kinachodaiwa kuwepo kwa baadhi ya maofisa elimu wa idara hiyo kuigawa ofisi na kutengeneza makundi hali iliyochangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa kiwango cha elimu katika Manispaa hiyo na kuifanya kuwa ya mwisho katika halmashauri 8 zilizopo katika mkoa wa Ruvuma.

Baadhi  ya walimu wa kuu wa shu;e za msingi na waratibu elimu kata ambao wameomba majina yao yahifadhiwe wameilalamikia idara ya Taaruma katika Manispaa hiyo kwa kuendekeza chuki na majungu ambayo hayana msingi na kusababisha elimu kushuka mpaka kuwa Halmashauri ya mwisho katika Mkoa wa Ruvuma

Walisema kuwa ni jambo la aibu sana kutokea kwani Manispaa ya Songea ina kila kitu ambacho kinaweza kuwafanya wanafunzi wafaulu kupitwa na halmashauri za Wilaya ambazo miundombinu yake ni duni na hazina walimu wa kutosha

Walisema kuwa  kitendo kinachofanywa na viongozi wa idara ya Taaluma kinakwamisha maendeleo ya elimu kwa kutokana na uroho wa madaraka ambao unasababisha makundi na uzembe kazini na kusababisha kushuka kwa elimu

Walieleza zaidi kuwa kuna waratibu elimu kata 7 na walimu wakuu 15 wamejipanga kukwamisha jitihada za kupanda kwa kiwango cha elimu katika manispaa ya songea kutokana na mgogoro uliopo kwenye idara za elimu na wanasiasa nao wamekuwa wakiendekeza mgogoro huo kwa maslahi yao binafsi

“Makundi hayo ambayo yanapelekea kuwayumbisha walimu na kushindwa kutekeleza  majukumu ya utendaji wao wa kazi katika kufundisha kwenye shule mbalimbali  za msingi katika Manispaa hiyo ni lazima utatuliwe na mamlaka husika bila kuingiza siasa” walisema

Walisema kuwa chanzo kikubwa cha mgogoro wa kielimu katika Halmashauri hiyo na kujengeka kwa makundi ni kunatokana na mmoja wa maofisa elimu hao ambaye alikuwa anakaimu idara hiyo kukataa  kukabidhi ofisi kwa Afisa elimu aliyeteuliwa na wizara kushika nafasi hiyo huku wakituhumiana kuwahonga baadhi ya Madiwani wa Baraza lililopita kwa ajili ya kupigania kushika nafasi hiyo.

Kufuatia mkutano maalum uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa shule ya sekondari ya wasichana Songea(Songea girls) kati ya Mbunge wa jimbo la Songea mjini  Leonidas Gama na walimu wa shule za msingi Manispaa ya Songea pamoja na maafisa wa idara ya elimu hivi karibuni walimu hao walimwelezea Mbunge huyo changamoto mbalimbali zilizopelekea Manispaa hiyo kushika nafasi ya mwisho katika mtihani wa taifa kimkoa ni kwa sababu ya kuwepo kwa madai ya walimu ya muda mrefu na idara kutosikiliza shida na kero zinazowakabili walimu.

Aidha walizitaja changamoto nyingine zilizopelekea Manispaa hiyo kushindwa kufanya vizuri katika mtihani wa taifa kimkoa mwaka jana kuwa ni pamoja na walimu kuhamishwa hamishwa ovyo kwa sababu ya chuki inayotokana na makundi pamoja na kuwepo kwa matabaka baina ya baadhi ya maofisa elimu na walimu na baadhi ya maofisa elimu wasiokuwa na sifa kupewa nafasi ya kushikilia idara.

Walieleza kuwa sababu za kushuka kwa kiwango cha ufaulu zipo nyingi ndogo ndogo lakini kubwa kuliko zote ni jipu ambalo lipo kwenye idara ya taaluma hivyo bila kuwahamisha wahusika wa idara hiyo ni vigumu sana kuinua kiwango hicho kwani idara hiyo ndio imekuwa chanzo cha migogoro baini ya waratibu wa elimu na wakuu wa shule za msingi pia na madiwani kwasababu ya uchu wa madaraka

Walisema kuwa sababu nyingine inayochangia  kushuka kwa kiwango cha elimu  ni  idara kushindwa kugharamia huduma za matibabu pindi mwalimu anapougua,uchache wa walimu pamoja na kuwepo kwa idadi kubwa ya wanafunzi katika darasa moja.

Afisa elimu msingi Manispaa ya Songea Edith Kagomba,alipohojiwa na gazeti hili alikiri kuwepo kwa uhamisho wa mara kwa mara kwa walimu kwa ajiri ya kurekebisha ikama na baadhi ya uhamisho wa walimu ulikuwa ukishinikizwa  na baadhi ya Madiwani wa Baraza lililopita kwa sababu ya chuki zao binafsi kwa walimu

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Songea mjini Leonidas Gama,alisema kuwa atahakikisha anashirikiana na serikali katika kuangalia uwezekano wa kutatua kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili walimu ili waweze kupandisha kiwango cha ufaulu ikiwa pamoja na kuwapiga marufuku Madiwani wenye tabia ya kushinikiza kuhamishwa kwa walimu kusikokuwa na kikomo kwa sababu zao binafsi.

Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Jenifa Omolo alisema kuwa analifahamu hilo na tayari hatua ndogo ndogo za kiutumishi zinaendelea kuchukuliwa dhidi ya madai husika

Alipotakiwa kuelezea kwanini jambo hilo limekuwa kero na kusababisha mifarakano katika idara hiyo na kuzalisha watoto wasio na taaluma, alijibu kuwa yeye ni mgeni na kwamba atafuatilia kwa karibu jambo hilo ili aweze kulimaliza kwa muda muafaka
MWISHO

Chapisha Maoni

 
Top