WANAFUNZI 10 WASIMAMISHWA SHULE, 96 WACHAPWA VIBOKO VITATU KILA MMOJA
NA STEPHANO MANGO,SONGEA
WANAFUNZI 10 kati ya wanafunzi 106 wa kidato cha sita katika shule ya Sekondari Namabengo Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma waliokuwa wameandamana kwenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu kumpelekea malalamiko dhidi ya makamu mkuu wa shule hiyo Shaibu Champunga ambae anatuhumiwa kuwa na lugha chafu na vitisho kwa wanafunzi wamesimamishwa kwa muda wa wiki tatu kwa makosa ya nidhamu na kushawishi wenzao kufanya maandamano yasiyo na kibali
Akizungumza na gazeti hili jana Katibu Tawala wa Wilaya ya Namtumbo Alkwin Ndimbo alisema kuwa baada ya wanafunzi kuandamana zilifanyika jitihada za kuwarudisha shule ili kubaini tatizo lililojitokeza ambapo alimwagiza Afisa Elimu wa Sekondari wa wilaya hiyo Patrick Atanas achukue hatua za haraka kwa kukutana na viongozi wa shule na wanafunzi ili kuona tuhuma zinazomkabili Makamu Mkuu wa shule hiyo
Ndimbo aliesema kuwa baada ya Afisa Elimu Atanas na uongozi wa shule ya Sekondari hiyo pamoja na wanafunzi wote kukaa na kuangalia chanzo cha maandamano hayo ilibainika kuwa wanafunzi 106 kutoka Namabengo hadi Kijiji cha Mlete umbali wa kilometa 16 walifanya kosa la kuandamana bila kufuata utaratibu pia walikuwa ni watovu wa nidhamu kwa kuvunja kanuni na sheria za shule kwa kuondaka eneo la shule bila idhini ya walimu ambapo makosa hayo wanafunzi walikiri kuyafanya hivyo uongozi wa shule uliamuru wanafunzi 96 wachapwe viboko vitatu kwa kila mwanafunzi na wanafunzi 10 ambao ndio walikuwa vinara wa maandamano hayo wamesimamishwa masomo kwa wiki tatu na mara wakimaliza adhabu hiyo wanatakiwa waende na wazazi kwa hatua zaidi za kinidhamu
Alisema kuwa tuhuma ambazo wanafunzi wamemtuhumu mwalimu Champunga sio za kweli kwani katika mahojiano mbalimbali yaliyofanyika hakuna aliyeweza kuthibitisha tuhuma hizo hivyo hawawezi kumchukulia hatua bila kuwa na ushahidi watuhuma hizo
Awali wanafunzi hao waliandamana juzi kwa wakimtuhumu makamu mkuu wa shule Champunga kutoa vitisho na lugha za matusi kwa wanafunzi,kuchapwa viboko visivyo na idadi,kuingi kwenye bweni la wanafunzi wa kike nyakati za usiku bila kuongozana na matroni na kuwalazimisha kufanya mapenzi pamoja na kuwazuia wanafunzi wa kike kulala bwenini.
Kutokana na malalamiko ya wanafunzi hao walitaka kwenda kumwona mkuu wa mkoa ili aweze kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero zao juhudi za kutaka kuonana na mkuu huyo wa mkoa ziligonga mwamba wakati wamesha tembea kwa miguu kilomita Zaidi ya 16 kabla ya kufika Songea mjini ambako askari polisi wakiongozwa na mkuu wa polisi wilaya ya Namtumbo kuwazuia wasiendelee na maandamano.
Wanafunzi hao walikutwa kijiji cha Mlete kilicho nje kidogo ya manispaa ya Songea ambapo askari polisi waliwaamuru wasimame ndipo mkuu wa polisi wilayani humo aliwataka waeleze sababu za kufanya maandamano bila kibali,wanafunzi hao walimweleza kuwa kila mtu anahaki ya kuongea kwa kuwa walishatoa malalamiko yao kwa mkuu wa shule lakini hayakusikilizwa hivyo waliona vema wakakutane na mkuu wa mkoa labda ataasikiliza.
Muda mfupi baadae alifika katibu tawala wa Namtumbo Alkwine Ndimbo na kusikiliza malalamiko mengi ya wanafunzi ambapo walimweleza kuwa makamu mkuu wa shule ya Sekondari Shaibu Champunga hawamtaki shuleni hapo kwa sababu anatuhumiwa kuwa na lugha chafu zenye kejeri ikiwa ni pamoja na kuwataja kwa majina wanafunzi wanaodaiwa kuwa na ugonjwa wa Ukimwi.
Walisisitiza kuwa shule hiyo haina miundombinu mizuri ambapo wamedai kuwa vyoo ni vibovu havifai kutumika,baadhi ya madarasa hayana sakafu paja na kwamba wanalazimika kwenda umbali mrefu kufuata maji.
Baada ya viongozi hao kusikiliza malalamiko ya wanafunzi waliwataka warudi shuleni ili wakatoe maamuzi mbele ya wanafunzi wote pamoja na walimu jambo ambalo wanafunzi walikubali na kusitisha maandamano.
MWISHO
Chapisha Maoni