0
                                    RPC RUVUMA ZUBERI MWOMBEJI
NA STEPHANO MANGO,SONGEA

MKAZI mmoja wa Kitongoji cha Halale kilichopo kata ya Kigonsela wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma Francis Nkondola ambaye umri wake haukuweza kufahamika mara moja amekutwa amekufa  huku akininginia  juu ya mti mrefu baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani huku mke wake akiwa amemwachia ujumbe mzito mezani.

Habari zilizopatikana jana mchana mjini hapa ambazo zimezibitishwa na Kaimu kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma Yahaya Athumani zimesema kuwa tukio hilo limetokea jazi majira ya saa 10 jioni kwenye eneo la minara ya kampuni ya simu za mikononi katika kitongoji cha Halale
.
Alisema kuwa inadaiwa siku hiyo  kabla ya tukio Nkondola na familia yake walikuwa wamepanga kwenda shambani majira ya asubuhi lakini aliwaamuru watoto wake pamoja na mkewe watangulie kwenda shambani yeye angefuata baadaye.

Alifafanua kuwa familia yake pamoja na mkewe walikwenda shambani mpaka muda ulipofika wa kurudi nyumbani Nkondola hakuweza kuonekana lakini walipofika nyumbani kwao walikuta barua mezani ambayo ilikuwa imeandikwa na baba yao Nkondola ikiwa na ujumbe mzito

Alisema kuwa ujumbe mzito ulkiokuwa umeandikwa na Nkondola ulisema kuwa (Mke wangu urudi nyumbani nisomeshee watoto wangu nimeamua kujiua mtanikuta kwenye mnara wa simu mkachukue pesa shilingi laki tano kwa mama Deni ili zisaidie watoto, nimechoka kuzurura kudai pesa zangu)

Alieleza zaidi kuwa watoto hao walipouona ujumbe huo walikwenda hadi kwenye eneo la Mnara  ambako walimkuta Nkondola ananing’inia kwenye mti baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani aliyokuwa ameifunga kwenye mti.

Kaimu kamanda wa Polisi Athumani alisema kuwa baadaye watoto wake walitoa taarifa kwa uongozi wa serikali  ya Kijiji cha Kigonsela ambao ulifika kwenye eneo la tukio kisha uliwasiliana na kituo kikuu cha Polisi cha Mbinga mjini na askari polisi wakiwa wameongozana na Mganga walifika kwenye eneo la tukio ambako ilibainika kuwa Nkondola alikuwa ameshakufa kwa kujinyonga na kamba ya katani.

Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na polisi umebaini kuwa chanzo cha Nkondola kujinyonga ni baada ya watu anaowadai pesa ambayo haifahamiki ni kiasi gani kumzungusha kwa muda mrefu bila mafanikio jambo ambalo lilimfanya apate hasira na kujichukulia sheria mkononi.

Alisema kuwa polisi bado inaendelea kufanya upelelezi wa kina ikiwa ni pamoja na kujiridhisha zaidi kama kuna mtu yeyote anayehusika katika tukio hilo ambalo limewaachia watoto ndugu jamaa na familia kiujumla majonzi.

MWISHO

Chapisha Maoni

 
Top