0
NA STEPHANO MANGO,SONGEA

ABIRIA 10 kati ya abiria 30 waliokuwa wakisafiri kwenye boti wakitokea mitomoni wilaya ya Songea Vijinini mkoani Ruvuma  kwenda mnadani katika Wilaya hiyo wanahofia kufa maji baada ya boti hiyo kuzama kwenye mto Ruvuma

Habari zilizopatikana jana mjini Songea zimeeleza kuwa boti hiyo ilikuwa imesheheni abiria pamoja na mizigo ikiwa inapelekwa kwenye mnada wa hadhara ambao upo jilani na kijiji cha Mitomoni mpakani mwa Tanzania na nchi jilani ya Msumbiji kwa ajiri ya biashara zao

Jitihada za Gazeti hili zimefanywa ili kuupata ukweli wa tukio hilo kwa kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Zuberi Mwombeji hazikufanikiwa baada ya kuelezwa kuwa alikuwa ameungana na Kamati ya ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Ruvuma ambayo imekwenda kwenye eneo la tukio hilo

Hata hivyo Gazeti hili liliweza kuwasiliana kwa njia ya simu na Afisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Ruvuma Hamis Kutiku ambaye alieleza kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa amekwenda kwenye eneo la tukio katika Kijiji cha Mitomoni ili kwenda kujiridhisha ukweli wa tukio hilo licha ya kuwa taarifa za awali ambazo zimelifikia jeshi hilo zimedai kuwa inahofiwa kuwa watu 10 wamekufa maji kutokana na ajari hiyo na wengine 20 wamenusurika

Kutiku alisema kuwa taarifa kamili ya tukio hilo zitapatikana mara baada ya kamati ya Ulinzi na Usalama kufika eneo la tukio na kurudi mjini hapa kwa hatua zaidi za kiulinzi na kiusalama

Jitihada za kumpata Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Ruvuma Dkt Binith Mahenge hazikuzaa matunda kwani naye ameungana na vyombo vya ulinzi na usalama kwenda kwenye eneo la tukio ambako mawasiliano ya simu hayapatikani kiurahisi na kwamba juhudi za kumtafuta zinaendelea aweze kutoa ufafanuzi zaidi

MWISHO

Chapisha Maoni

 
Top