MKURUGENZI WA MANISPAA YA SONGEA JENIFA OMORO
NA STEPHANO MANGO,SONGEA
Taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa Hesabu za
serikali(CAG) imetoa Hati Safi katika
miradi yote mitatu ya Halmashauri ya manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Ofisa habari wa manispaa ya Songea Albano Midelo ameitaja
miradi iliyopata Hati Safi katika manispaa hiyo kuwa ni pamoja na mradi wa maji(NWSDP),mradi wa afya Health Basket Fund(HBF) na mradi wa
kilimo na mifugo Agriculture Sector Development project(ASDP).
Kwa mujibu wa Midelo Juni 8 mwaka huu Halmashauri ya
manispaa ya Songea ilipokea taarifa za miradi hiyo mitatu kutoka kwa mdhibiti
na mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali katika kipindi cha mwaka 2014/2015
ikionesha miradi yote mitatu imepata Hati Safi.
Hata hivyo amesema hivi sasa menejimenti ya manispaa hiyo
inaendelea na mchakato wa kujibu hoja ambazo zimetolewa kwenye miradi hiyo
kisha kupelekwa kwa CAG kwa ajili ya kuhakikiwa,kufungwa na kufutwa kwa hoja
zinazohusika ndani ya siku 21 kuanzia Juni 8 mwaka huu.
Wakati huo huo Halmashauri ya manispaa ya Songea
imependekeza kufuta wadaiwa saba sugu wanaodaiwa zaidi ya shilingi milioni 14.7 katika
kipindi cha kuanzia mwaka 2011/2012 ambapo Halmashauri ya manispaa hiyo ilipata
Hoja za Ukaguzi ambazo zilitokana na kutokusanywa kwa fedha za mtu binafsi na
vikundi vya wanawake kutokana na kukosa
kumbukumbu na orodha ya vikundi.
Ofisa habari huyo wa manispaa ya Songea anabainisha kuwa
vikundi vya wanawake katika kipindi cha mwaka 1997 hadi 2012 walikuwa wanadaiwa zaidi ya shilingi milioni
10 na kwamba Hoja ya kudaiwa vikundi hivyo hadi leo bado haijafungwa kutokana
na wadaiwa kutoilipa manispaa.
“Ufuatiliaji
uliofanyika unaonesha kuwa wadaiwa wote hawajulikani walipo kwa kuwa
vikundi,orodha yao haipo na aliyekuwa mratibu wa kazi ya vikundi hivyo
amefariki Dunia, kwa kuwa Hoja hiyo imeendelea kuwepo hadi sasa mweka hazina mkuu wa manispaa ya Songea
amependekeza kufutwa kwa wadaiwa hawa’’,alisema.
Alisema mwaka 2011/2012 Halmashauri ya manispaa ya Songea
ilipata Hoja za ukaguzi namba 2.2.10.2 ambayo ilitokana na kutokusanywa kwa
fedha za pango za kituo cha mabasi kwa wapangaji sita ambao wanadaiwa jumla ya shilingi milioni 4.6
kwa mwaka wa fedha wa 2007/2008 unaoishia Juni 30 mwaka huu na kwamba hoja
haijafungwa hadi sasa ambapo wadaiwa hawajulikani na wamefunga vibanda vyao.
Amewataja wadaiwa sugu hao kuwa ni Nassoro Suleiman anadaiwa
kuanzia Juni 2009 hadi Mei 2016 jumla ya shilingi 400,000,Kilimanjaro Express
kuanzia Januari 2007 hadi Mei 2016 jumla ya shilingi milioni 1.65,Martin
Massawe kuanzia Januari 2007 hadi Mei 2016 jumla ya shilingi 600,000,Mr.Nyaruke
kuanzia Januari 2007 hadi Mei 2016 shilingi milioni 1.8 na Esta Komba kuanzia
Januari 2007 hadi Mei 2016 shilingi 150,000.
Kwa mujibu wa kifungu cha local Authorities Financial
Memorandum cha mwaka 2009,LAFM Order 44(3) kinaeleza kufuta wadaiwa sugu na
kifungu 104(2) cha local authorities Financial Memorandum cha mwaka 2009
kimeweka umri wa zaidi ya miaka mitano kama kigezo cha madai yasipolipwa
kufutwa.
Mwisho.
Chapisha Maoni