MKUU WA WILAYA YA SONGEA BENSON MPESYA AKIHAMASISHA MAENDELEO
NA MWANDISHI WETU,SONGEA
Mkuu wa wilaya ya
Songea ambaye pia ni kaimu mkuu wa mkoa wa Ruvuma Benson Mpesya amesema Mwenge
wa uhuru unatukumbusha wajibu wa
kujitegemea na kujiletea maendeleo yaliokuwa yamedumaa.
Akizungumza jana
katika kikao cha mwisho cha maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa uhuru kwenye
ukumbi wa Manispaa ya Songea,Mpesya alisema Mwenge ambao unakimbizwa mara moja
kila mwaka una umhimu mkubwa katika kuchochea maendeleo endelevu.
Amewaonya wanasiasa
ambao wanapotosha ukweli kuhusu Mwenge wa uhuru kuacha tabia hiyo badala yake
waungane na serikali ya Chama tawala kuhakikisha wanashiriki kikamilifu na
kuonesha ushirikiano hadi Mwenge utakapopita salama wilayani Songea na Taifa
kwa ujumla.
“Hakuna sababu ya
kugombana na Mwenge,kila mmoja atimize wajibu wake,Mwenge wa uhuru kila unapokimbizwa unasisimua miradi ya maendeleo ambayo ilikuwa imelala hivyo
kufufuliwa upya kwa kuweka mawe ya msingi,kuzinduliwa na kufunguliwa ’’,alisisitiza.
Alisema serikali ya
awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kupitia Mwenge wa Uhuru ambao
unamwakilisha Rais imekusudia
kuimairisha nidhamu ya kazi na ubunifu kwa watumishi wote serikalini ili waweze
kukabiliana na changamoto mbalimbali badala ya kusubiri serikali kwa kila kitu.
Afisa habari wa
manispaa ya Songea Albano Midelo amesema ratiba ya Mwenge wa uhuru katika
manispaa hiyo inaonesha kuwa Mwenge utaingia wilayani Songea Juni 8 ukitokea
wilayani Namtumbo ambao utapokelewa katika eneo la Shule ya Tanga.
Kwa mujibu wa Midelo,katika
manispaa ya Songea Mwenge wa uhuru utaweka mawe ya msingi,kuzindua na kufungua
jumla ya miradi saba yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 800 ikiwemo
uzinduzi wa kituo cha kati cha mabasi cha Songea,kukabidhi madawati 100 ya
shule ya Luhira na uzinduzi wa nyumba ya mkurugenzi wa manispaa ya Songea.
Miradi mingine ni
pamoja kufungua madarasa mawili ya Matokeo makubwa Sasa(BRN) katika shule ya
sekondari Chabruma,Mradi wa kupanda miti ya hifadhi katika chanzo cha maji cha
Luhira kinachotumika na Mamlaka ya maji safi na taka manispaa ya
Songea(SOUWASA) na mradi wa ufugaji wa ng’ombe wa kikundi cha watu wanaoishi na
Virusi vya Ukimwi katika kata ya Mwengemshindo.
Ratiba ya Mbio za
Mwenge wa Uhuru katika wilaya ya Songea inaonesha kuwa Mwenge utapita katika
Halmashauri tatu zilizopo katika wilaya hiyo ambazo ni Halmashauri ya Manispaa
ya Songea Juni 8,Halmashauri ya Songea
Juni 12 na Halmashauri ya Madaba Juni 13.
Kikao hicho cha
mwisho cha mapokezi ya Mwenge wa uhuru wilayani Songea kiliwahusisha
wakurugenzi wa Halmashauri zote tatu za wilaya ya Songea,wakuu wa
idara,viongozi wa vyama vya siasa ngazi ya wilaya pamoja na maafisa watendaji
wa mitaa na kata.
Mwisho.
Chapisha Maoni