MBUNGE GAMA AWALILIA WAJASILIAMALI RIBA ZA MIKOPO
MBUNGE WA JIMBO LA SONGEA MJINI LEONIDAS GAMA
NA STEPHANO MANGO,SONGEA
MBUNGE wa jimbo la Songea mjini kupitia tiketi ya chama cha Mapinduzi(CCM)mkoani Ruvuma Leonidas Gama,amesema kuwa mikopo inayotolewa kwa riba kubwa na baadhi ya taasisi za kifedha mjini hapa imekuwa ni kikwazo cha kupambana na umasikini wa wananchi.
Gama aliyasema hayo jana kwa niaba ya Mbunge wa jimbo la Peramiho Jenista Mhagama ambaye pia ni waziri wa kazi,sera ajira,walemavu na vijana wakati alipokuwa akizungumza na vikundi mbalimbali vya ujasiriamali vinavyoratibiwa na Jumuia ya Mabinti wa Maria Immaculata(DMI)mjini Songea.
Alisema kuwa mikopo hiyo imekuwa sio msaada kwa wananchi na badala yake inachangia kwa kiasi kikubwa kuwaingiza katika dimbwi la umasikini kutokana na baadhi yao wanaposhindwa kurejesha mikopo hiyo uuziwa mali zao ikiwemo nyumba.
Kufuatia hali hiyo mbunge huyo amewataka wananchi kujiunga kwenye vikundi mbalimbali vya ujasiriamali ikiwemo DMI ili waweze kupata mikopo inayotolewa na serikali kwa urahisi na kwa riba nafuu badala ya kuendelea kudhurumika.
Aidha amevipongeza vikundi vya ujasiriamali vinavyoratibiwa na Jumuia hiyo kwa kukidhi vigezo vya kukopesheka jambo ambalo amewataka wanavikundi hao kuepuka kutumia mikopo yao kwa mambo ya anasa,sherehe na kuongeza nyumba ndogo badala yake waitumie kwa nidhamu pamoja na kukopa na kurejesha kwa wakati.
Akizungumza katika mkutano huo Mratibu wa mifuko ya uwezeshaji baraza la Taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi Nyakao Mahemba,alisema kuwa vikundi hivyo vimekidhi vigezo baada kufungua akaunti katika benki ya posta na kujiwekea akiba.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa vikundi hivyo mkoani Ruvuma Speciosa Katambala,amemuhakikishia mbunge huyo kuwa yale yote aliyowaagiza watayafanyia kazi ikiwemo kuendelea kuhamasisha wananchi wilaya zote za mkoa wa Ruvuma kujiunga na vikundi hivyo pamoja na kutumia mikopo watakayopata kwa malengo yaliyokusudiwa.
MWISHO
Chapisha Maoni