WAHANGA WA BOTI MITOMONI WATAMBULIKA
NA STEPHANO MANGO,SONGEA
ABIRIA 9 kati ya abiria 45 waliokuwa wakisafiri kwenye boti kutoka eneo la Mkenda kijiji cha nakawale wilaya ya songea kwenda kijiji cha Mitomoni kata ya Mipotopoto wilayani Nyasa wanahofiwa kufa maji baada ya boti kugonga kingo za mto na kuzama.
Akizungumza na Gazeti hili jana mchana ofisini kwake kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Zuberi Mwombeji alifafanua kuwa tukio hilo lilitokea Julai 2 mwaka huu majira ya saa 9 Alasairi katikati ya mto Ruvuma unaounganisha vijiji vya Nakawale wilayani songea na Mitomoni wilayani Nyasa.
Alisema kuwa inadaiwa kuwa boti hiyo ambayo haijasajiliwa inamilikiwa na Hamisi Mbegu(59) ambaye ni Diwani wa Kata ya Mipotopoto kupitia chama cha mapinduzi na kwamba Boti hiyo imekuwa ikitumika kama kivuko kwa kuwavusha watu kati ya Vijiji hivyo.
Alieleza zaidi kuwa siku hiyo ya tukio kulikuwa na Gulio katika kijiji cha Nakawale kitongoji cha Mkenda Boti ilikuwa inawavusha watu waliotoka kwenye Gulio kutafuta mahitaji yao kwenye kijiji cha mitomoni ambapo boti hiyo wakati inakaribia kufika ukiongoni kufika kwenye eneo la kijiji cha Mitomoni iligonga gema hali iliyosababisha kuyumba na kukosa uelekeo kisha kuwamwaga abiria waliokuwa kwenye Boti hiyo.
Kati ya abiria 45waliokuwa kwenye boti hiyo abiria 36 walinusurika lakini abiria 9 wanahofiwa kufa maji na mpaka sasa hawajaoneka licha ya kuwepo kwa juhudi za kuwatafuta.
Aliwataja wanaohofiwa kufa maji kuwa ni Fatuma Said (41) anayedaiwa kuwa alikuwa ni mjamzito wa miezi sita, Awetu Shaibu (14) mwanafunzi aliyekuwa anasoma darasa la sita katika shule ya msingi mitomoni, Rajabu Machupa mkazi wa kijiji cha Mitomoni na Omari waziri (13) mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi mitomoni.
Wengi wametajwa kuwa ni Zulfa Aly 14 mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi mitomoni, Omari Jela 11 mwanafunzi wa darasa la tatu anayesoma katika shule ya msingi Mitomoni, Fadhiri Hamisi 9 mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya msingi mitomoni, Tupishane Mustafa 5 na Stumai Abdala 5 wote wakazi wa kijiji cha mitomoni.
Kamanda Mwombeji alisema kuwa uchunguzi wa awali umeonesha kuwa boti hiyo ilikuwa imebeba abiria wengi tofauti na uwezo wake hali iliyomfanya mwendesha boti hiyo kushindwa kuendesha na kwamba mpaka sasa juhudi za kuitafuta miili ya watu wanahofiwa kufa maji inaendelea.
MWISHO
Chapisha Maoni