WANANCHI WAWEKA MAGOGO BARABARANI KUZUIA KAMATI NA MWEKAZAJI
NA STEPHANO MANGO,MAKETE
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida wananchi wa kijiji cha
Mbalatse wilayani Makete mkoa wa Njombe, wameweka magogo makubwa barabarani
kuzuia Kamati iliyoundwa na uongozi wa wilaya hiyo kwenda kijijini hapo
kuchunguza mgogoro wa ardhi uliopo kati ya wananchi wa kijiji hicho na
mwekezaji wa Kampuni ya Silverland Tanzania, kwa madai kuwa amepora ardhi yao
zaidi ya hekta 3,000 ambazo zilikuwa zikiwasaidia kuzalisha mazao ya aina
mbalimbali.
Wananchi hao ambao walionekana kuwa na jazba walizuia magari
yaliyowaleta wajumbe wa kamati hiyo na mwekezaji huyo katika ofisi za makao
makuu ya kata hiyo, walionekana kuwa na hasira huku wengine wakiimba nyimbo kwa
sauti kubwa wakisema, “tunataka turudishiwe mashamba yetu, aliyotunyang’anya
mwekezaji.
Tukio hilo la aina yake lilitokea Julai 14 mwaka huu majira
ya mchana kwenye eneo la ofisi za kata ya Mbalatse, ambako umati mkubwa wananchi
ulikusanyika kwa lengo la kujua hatma ya mgogoro huo uliopo kati yao na mwekezaji.
Aidha wananchi hao wamemuomba Waziri wa ardhi, nyumba na
maendeleo ya makazi William Lukuvi kuona umuhimu wa kuingilia kati kutatua mgogoro
huo ambao unatishia usalama wa maisha yao.
Walisema kuwa kufuatia ardhi hiyo kuchukuliwa na mwekezaji
huyo, wananchi hao wanakosa maeneo ya kulima mazao ya chakula na biashara jambo
ambalo hivi sasa, baadhi yao wanalazimika kwenda kwenye maeneo karibu na vyanzo
vya maji kulima mazao hayo.
Wakihojiwa na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti,
wananchi hao walifafanua kuwa miaka iliyopita kwa muda mrefu walikuwa wakilima
mahindi kwa wingi katika eneo hilo ambalo ni maarufu kwa jina la Ludodolela,
ambalo lina rutuba tofauti na maeneo mengine yaliyopo kwenye kata hiyo.
Aloyce Chaula mkazi wa kijiji cha Mbalatse alifafanua kuwa
tangu kuzaliwa kwake miaka ya 60 iliyopita wazazi wake pamoja na wananchi
wengine wa kata hiyo walikuwa na mashamba yao katika eneo hilo ambalo amepewa
mwekezaji, bila wananchi kushirikishwa hivyo wanaiomba serikali kupitia Wizara
hiyo kunusuru hali hiyo ili wananchi wa kata hiyo waweze kurejeshewa mashamba
yao.
“Ndugu waandishi wa habari mnaliona kundi hili kubwa la
wananchi wakilalamikia kuporwa maeneo yao, kwani awali huyu mwekezaji alikuja
hapa kwetu kijijini kuomba eneo dogo kwa muda kwa ajili ya kufanya majaribio ya
kupanda mbegu za zao la shairi, lakini tuna mshangaa ghafla amemilikishwa eneo
kubwa na sisi wazawa tumefukuzwa huku akiendelea na uzalishaji wa zao hili la
shairi”, alisema Chaula.
Kwa upande wake Damian Mwinuka mkazi wa kijiji hicho alieleza
kuwa kufuatia mwekezaji huyo kunyang’anya eneo hilo la mashamba bila kufuata
taratibu za utwaaji ardhi, hivi sasa vijana wengi wanakwenda mikoa ya jirani
kwenda kutafuta mashamba ya kulima wakati nyumbani kwao kulikuwa na eneo kubwa
la kuweza kuzalisha mazao mbalimbali ikiwemo viazi mviringo, ufuta, alizeti na
ngano.
Alisema kuwa kutokana na usumbufu huo wanaoupata sasa, bado
wanalazimika kuiangukia serikali ili iweze kuwasaidia na ardhi yao irejeshwe
mikononi mwao na sio vinginevyo.
Uchunguzi uliofanywa na waandishi wa habari umebaini pia
katika mashamba hayo yanayolalamikiwa, mwekezaji huyo wa Silverlands Tanzania yenye
makao makuu yake Ifunda mkoani Iringa ndiyo inayoendesha shughuli za kilimo cha
zao la shairi kwenye eneo hilo linalolalamikiwa na wananchi hao.
Waandishi hao wamezungumza na Meneja wa Kampuni hiyo Steven
Maina alisema kuwa ndani ya eneo hilo, wao wana hati miliki na kwamba kuna
kiwanja cha ndege ambacho kimekuwa kikitumika ndege kutua kipindi cha kiangazi,
wakati wa mavuno ya zao hilo na kwamba pia kumejengwa majengo ya ofisi na
nyumba za kuishi wafanyakazi wa shamba hilo.
Maina alifafanua kuwa sehemu ya shamba hilo kumezalishwa kwa
wingi zao la shairi alizeti, ngano na mboga mboga pamoja na miti ya asili na
kwamba haoni sababu ya mgogoro huo kuendelezwa huku akishauri kwamba kuna kila
sababu ya serikali kuchukua hatua ya kumaliza tofauti zilizopo.
Naye diwani wa kata ya Mbalatse, Edson Msigwa alisema kuwa
malalamiko hayo ya wananchi ni ya kweli kwa kile alichodai kuwa mwekezaji huyo
alipewa ekari 70 tu kwa muda kwa lengo afanye majaribio ya kupanda mbegu za zao
la shairi, lakini wanashangaa kuona amezalisha ekari zaidi ya 3,000 na
kujimilikisha maeneo hayo bila wananchi kushirikishwa.
Msigwa alisema kuwa kufuatia kuwepo kwa mkanganyiko huo,
tayari hatua zimechukuliwa kwa kwenda halmashauri ya wilaya ya Makete kuutaka
uongozi husika kuona namna ya kumaliza tatizo hilo, kabla machafuko hayajatokea
kama ilivyo kwa maeneo mengine ya nje ya mkoa wa Njombe.
“Wananchi wa kata yangu wapo tayari kufunga safari kwenda
kuonana na Waziri mwenye dhamana, ili waweze kupata haki zao za msingi juu ya
madai haya ya ardhi yao kutokana na hivi sasa wanakosa maeneo ya kuzalisha
chakula”, alisema Msigwa.
Pia baada ya diwani huyo kutuliza hasira za wananchi hao,
ndipo walichukua hatua ya kuyaondoa magogo makubwa waliyokuwa wameyaweka
barabarani kwa lengo la kuzuia magari ya wajumbe wa kamati hiyo na mwekezaji
yaweze kuondoka mara baada ya kamati hiyo kukamilisha taratibu zake.
Hata hivyo Kaimu Mkuu wa wilaya ya Makete, Merina Ijiko
ambaye pia ni afisa tawala wa wilaya hiyo alipozungumza na gazeti hili alisema
kuwa kitendo walichofanya wananchi hao cha kuzuia magari hayo ni kosa, kwa kuwa
Kamati hiyo imeundwa kisheria kwa ajili ya kuchunguza mgogoro huo kati yao na mwekezaji
huyo hivyo amewataka kupunguza jazba wakati tatizo hilo linafanyiwa kazi.
MWISHO.
Chapisha Maoni