0
Mkurugenzi Mtendaji Mantra Tanzania LTD Fred Kibodya wakati wa hafla ya kukabidhi madawati 500 kwa Serikali ya Mkoa wa Ruvuma
Mkurugenzi Mtendaji Mantra Tanzania LTD Fred Kibodya wa pili kutoka kushoto akisalimiana na Mkandarasi aliyetengeneza madawati 500 Izack Mtumbika kabla hajayapokea na kumkabidhi Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt Binilith Mahenge

NA STEPHANO MANGO,SONGEA

WADAWA mbalimbali wa maendeleo wa ndani na nje ya mkoa wa Ruvuma wametakiwa kusaidia jitihada za Serikali kuweza kukamilisha madawati 5,263 ya shule za msingi yaliyobakia ili kuendana na kasi ya Rais John Magufuli

Wito huo umetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt Binilith Mahenge wakati akipokea msaada wa madawati 500 yenye thamani ya milioni 40 uliotolewa na Kampuni ya Mantra Tanzania kwa kushirikiana na shirika la la ROSATOM

Akizungumza kwenye hafla fupi iliyofanyika kwenye viwanja vya majengo Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa   mkoa huo una jumla ya shule za msingi 782 ambapo kati ya hizo za Serikali ni 766 na zisizo za Serikali ni 16

Mahenge alisema kuwa hadi kufikia machi 31 mwaka huu wanafunzi wa awali walioandikishwa walikuwa 47,502 kati yao wavulana 23,638 na wasichana walikuwa 23,864 na kwamba darasa la kwanza walioandikishwa walifika 57,942 kwa maana wavulana 29443 na wasichana 28499


Alisema kuwa kumekuwepo na ongezeko kubwa la uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali na la kwanza kwa mwaka 2016 kutokana na sera ya elimu bure ambapo awali walikuwa watoto wengi wanakosa haki ya kupata elimu

Alieleza zaidi kuwa hadi juni 30 mwaka huu,mkoa umetengeneza madawati 102,853 ya shule za msingi na madawati 42,842 ya shule za sekondari na kufanya idadi ya upungufu ya madawati ni 9,107 ambapo mahitaji kwa shule za msingi ni 108,616 na upungufu tulio nao ni madawati 5,763 hadi kufikia juni 30

Kwa upande wa shule za sekondari mahitaji ni madawati 46,186 hadi kufikia juni 30,2016 ambapo upungufu ni madawati 3,344 na kwamba Halmashauri ya Manispaa ya Songea imemaliza kazi hiyo na wamebaki na ziada ya madawati 350, huku Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ikiwa inaupungufu wa madawati 2,749

“Naipongeza sana Kampuni ya Mantra Tanzania kwa kutukabidhi madawati 500 yenye thamani ya milioni 40 kwani madawati hayo yanatufanya tuwe na upungufu wa madawati 5,263 yanayotakiwa kutosheleza mahitaji ya shule za msingi”alisema Mahenge

Awali Mkurugenzi Mtendaji Mantra Tanzania LTD Fred Kibodya akizungumza katika hafla ya kukabidhi madawati alisema kuwa katika jitihada za kuunga mkono uamuzi wa Rais John Magufuli wa kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi Sekondari imeamua kutoa msaada huo


Kibodya alisema kuwa Mantra kama sehemu yake ya uwajibikaji wa Taasisi kwa jamii(CSR) imeamua kuchangia madawati 500 yenye thamani ya shilingi milioni 40 ili kusaidia kuongeza ubora wa elimu kwa kuboresha mazingira ya kujisomea

“Kampuni ya Mantra inaamini kwamba madawati haya yatatoa mchango chanya katika kuleta ari ya kujifunza kwa watoto 1500 na kuwahamasisha kwenda shule kila siku kwa vile wataweza kukaa vizuri kwenye madawati na kuwa makini kumsikiliza mwalimu na kushiriki katika shughuli za darasani”alisema Kibodya

Alisema kuwa pia madawati hayo yatawasaidia wanafunzi kujipanga vizuri na kuandika mwandiko mzuri tofauti na kukaa chini sakafuni au kukaa kwa kubanana kama ilivyokuwa awali ,hivyo ni imani ya Mantra kuwa msaada huo utaboresha kiwango cha elimu katika mkoa wa Ruvuma ambako Mantra inafanya shughuli zake

Alieleza kuwa tangu Mantra ianze utafiti wa urani katika mradi wake wa mto Mkuju imekuwa na bidii katika kuchangia kuboresha upatikanaji wa elimu bora mkoani Ruvyma hususani Wilaya ya Namtumbo kwa kuchangia madawati

Vitabu na maktaba miongoni mwa shule za msingi na za sekondari,nishati ya jua,ujenzi wa maabara ya sayansi na mambo mengine,pia imekuwa ikisaidia katika sekta ya mazingira na sekta ya afya kwa Namtumbo na Taifa kiujumla

Alisema kuwa mpango wa CSR ulio bora ni mpango wake wa kupambana na ujangili kwani inatambua kuwa tembo wa Tanzania ndio miongoni mwa wanaotishiwa zaid duniani,hivyo kampuni imechukua hatua kwa kuzindua operesheni kali nay a teknolojia ya juu kupambana na ujangili kwa kushirikiana na Idara ya Wizara ya Maliasili na Utalii

Kama mshirika wa maendeleo na katika ari ya ushirikiano wa sekta ya umma na sekta binafsi(Public Private Partnership) itaendelea kuiunga mkono serikali ili kukuza vipaumbele vyake vya kisekta
MWISHO

Chapisha Maoni

 
Top