NA STEPHANO MANGO,SONGEA
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, linamshikilia Frank Ndunguru
(33) ambaye ni dereva wa Kampuni ya mabasi ya Makeo inayosafirisha abiria
kutoka Manispaa ya Songea kwenda wilaya ya Mbinga mkoani humo, baada ya
kusababisha ajali na kuua watu watatu.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji
alisema kuwa tukio hilo lilitokea Julai 30 mwaka huu majira ya saa 1:30 usiku
katika kijiji cha Mkako kata ya Mkako wilayani Mbinga, ambapo dereva huyo
alikuwa akiendesha gari lenye namba za usajili T. 534 CPV ambalo linamilikiwa
na Mohamed Makeo mkazi wa Songea mjini.
Mwombeji alifafanua kuwa chanzo cha ajali hiyo kinatokana na
uzembe wa dereva huyo, baada ya kuendesha gari katika mwendo kasi na hatimaye kushindwa
kukata kona kali kisha kusababisha ajali hiyo baada ya gari kupoteza mwelekeo.
“Dereva wa gari hili yupo mikononi mwa Polisi, tunaendelea
kumuhoji na kukamilisha hatua za upelelezi ili aweze kuchukuliwa hatua za
kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani”, alisema Mwombeji.
Kamanda huyo wa Polisi alitoa wito kwa madereva wa magari
hapa mkoani Ruvuma, kuzingatia sheria za usalama barabarani, ili isiweze
kutokea uzembe kama huo ambao unasababisha watu kupoteza maisha na wengine kuwa
na ulemavu wa kudumu.
Alisema kuwa Jeshi hilo litaendelea kuchukua hatua kali kwa
madereva wa aina hiyo, ikiwemo kufutiwa leseni zao ili madhara ysiweze kutokea
mara kwa mara na kupoteza nguvu kazi ya taifa hili.
“Tunaendelea kuwaelimisha hawa wadau wetu wanaosafirisha
abiria kuwa makini barabarani pale wanapoendesha vyombo vya moto, uzembe huu
haukubaliki kabisa”, alisema.
Kadhalika aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Robert Roter
(67) ambaye ni raia wa nchi ya Ujerumani, Cosmas Kambona (54) ambaye ni tingo
wa gari hilo mkazi wa Songea na mmoja anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 33 ambaye
jina lake bado halijatambuliwa.
Aliongeza kuwa katika gari hilo kulikuwa na majeruhi 14
ambapo kati ya hao baadhi yao, walilazwa hospitali ya wilaya Mbinga
wameruhusiwa na kwamba 10 bado wanauguza majeraha waliyonayo hospitali ya mkoa
Songea.
Pamoja na mambo mengine, Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali
ya mkoa Songea, Jonas Lulandala amethibitisha kupokea majeruhi hao ambao hali
zao bado ni mbaya na vifo hivyo kutokea.
MWISHO.
Chapisha Maoni