0

NA STEPHANO MANGO,SONGEA

MKURUGENZI wa manispaa ya Songea Tina Sekambo amewaasa wakuu wa idara na vitendo  katika manispaa hiyo kufanyakazi kwa kushirikiana ili kumaliza kero mbalimbali zinazowakabili watumishi wanaowaongoza na wananchi.

Sekambo aliyasema hayo wakati anazungumza na watendaji wakuu hao katika kikao cha kwanza cha kujitambulisha tangu alipoteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mkurugenzi wa manispaa hiyo akichukua nafasi ya Jenifa Omolo ambaye ameteuliwa kuwa mkurugenzi wa Kibaha.

Pia amewaagiza wakuu wa idara kushughulikia kero kubwa katika manispaa ya Songea ikiwemo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi na kusimamia usafi wa mazingira hasa katika maeneo ya pembezoni mwa mji huo.

Katika hatua nyingine Sekambo amewataka wakuu wa idara pamoja na watumishi wote wa umma katika manispaa hiyo kuacha kufanyakazi kama walivyozoea badala yake kufanyakazi kwa juhudi na kufuata misingi ya utumishi wa umma.

“Katika utawala wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk.John Magufuli ,mtumishi wa umma ili ubakie salama unatakiwa kuwa mkweli,ukidanganya katika kazi haupo salama,utafuatiliwa,ukweli pekee ndiyo utakaokulinda’’,alisisitiza Sekambo.

Mkurugenzi huyo pia amewaagiza wakuu wa idara kufuatilia watumishi wanaosoma kuhakikisha kama kweli wapo chuoni,kutokana na kubainika kuwa kuna baadhi ya watumishi wameruhusiwa kusoma lakini wanafanyakazi sehemu nyingine hivyo wanalipwa mishahara miwili.

Sekambo pia amemuagiza mkaguzi wa ndani wa mahesabu kufuatilia ruzuku ya serikali kuona matumizi ya fedha katika shule  yanaendana na idadi ya wanafunzi waliopo.
Mwisho.

Chapisha Maoni

 
Top