NA STEPHANO MANGO,SONGEA
BAADHI ya wanachama wa Chama
cha Mapinduzi wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wamekitaka chama hicho ngazi ya
Mkoa kumchukulia hatua za kinidhamu Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa Joseph
Mhagama kwa kitendo chake cha kujihusisha na kufanikisha harakati za Chama cha
Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA)
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti wanachama hao walisema kuwa kitendo cha kada huyo kushirikiana na
Diwani wa kata ya Kilagano Bathromeo Nkwera ambaye ni kada wa Chadema kinaleta
wasiwasi wa imani ya Joseph Mhagama katika chama chake cha Ccm na hasa baada ya
kutangaza nia ya kutaka kugombea ubunge katika jimbo la Peramiho kupitia ccm.
Wanceraus Komba ambaye ni
Kada wa Ccm na Mwenyekiti wa Ujenzi wa Zahanati ya Mhepai alisema kuwa hali ya
Kisiasa ya Jimbo la Peramiho inavurugwa sana na Joseph Mhagama kwani amekuwa
akishawishi baadhi ya viongozi wamuunge mkono katika harakati za ubunge kupitia
Ccm huku akiwa muda mwingi anautumia kumsaidia diwani wa chadema katika mipango
yake.
Komba alisema kuwa hali hiyo
inasikitisha sana na kuwafanya viongozi mbalimbali wa Chama katika Jimbo hilo kutoelewa
imani yake katika chama na mwenendo mzima wa harakati zake kwani zinatutia
shaka sana katika uendelezaji wa majukumu na ilani ya chama ya 2010 na 2015
Alisema kuwa pia inasikitisha
sana kuona chama kinamuachia Mhagama kuanza kampeni mapema ya kutaka ubunge
kabla ya wakati huku akijua kuwa muda uliobaki ni muhimu kuhakikisha kuwa ilani
ya uchaguzi inatekelezwa ili muda wa kampeni ukifika wananchi waelezwe ahadi za
chama namna zilivyotekelezwa.
Alieleza kuwa vitendo hivyo
vyote vya kumsaidia Diwani wa Chadema na kuanza kampeni mapema vinapaswa
vichunguzwe na vichukuliwe hatua kali za kinidhamu ili chama kibaki salama
wakati huu ambao tunalekea kwenye uchaguzi mkuu wa Udiwani, ubunge na urais.
Akizungumza na gazeti hili Joseph
Mhagama alisema kuwa toka mwaka 2010 amekuwa akisaidia mambo mbalimbali kwenye
kata zote za halmashauri ya wilaya ya Songea ambayo ndio Jimbo la Peramiho.
Mhagama alisema kuwa amekuwa
akitoa fedha, mipira, jezi na misaada mingine ambayo wanamuomba na wala habagui
ila Diwani wa Kata ya Kilagano Nkwera amekuwa akimuomba misaada mara kwa mara
na hivyo amekuwa akimpatia.
Kwa Upande wake Katibu wa
Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Songea Rajabu Uhonde alisema kuwa amesikitishwa
sana na mwenendo wa Joseph Mhagama na hasa akiwa ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa
ya Mkoa wa Ruvuma kwani anaamini kuwa anafahamu fika kuwa lengo la Ccm ni
kushika dola.
Uhonde alisema kuwa kada huyo
anafahamu sheria na kanuni za chama hivyo kwa hayo ambayo anayafanya ana
hatarisha uhai wa chama na kutokana na makosa hayo ambayo wanachama
wanamlalamikia basi ni vyema chama kikamfuatilia na kumchukulia hatua stahiki
kulingana na yale ambayo yatabainika
Alisema kuwa licha ya kupata taarifa za
kukiuka kanuni za chama pia Mhagama amekuwa akilalamikiwa kuyagawa makundi
ndani ya jumuiya za chama kwa kufanya vikao mbalimbali ambavyo vinaashiria
kutengeneza safu yake ya ushindi wa ubunge huku akijua kuwa mbunge aliyopo bado
anatekeleza ilani husika.
MWISHO
Chapisha Maoni