NA STEPHANO MANGO,SONGEA
MWENYEKITI wa bodi ya mamlaka ya maji safi na usafi wa mzingira (SOUWASA) mkoani Ruvuma mhandisi Wilson Mandia amesema kuwa mamlaka hiyo kwa sasa ina hali ngumu kutokana na taasisi za serikali kutolipa madeni jambo ambalo linakwamisha kutoa huduma ya mtandao wa maji kwa watu wanaohitaji kuunganishiwa huduma hiyo.
Hayo ameyasema jana kwenye ziara ya baadhi ya waandishi wa habari ambao walitembelea vyanzo vya maji vya mto Ruhila ambako kunamradi wa mkubwa wa ujenzi wa bwawa la kuhifadhia maji yatakayotumika kipindi cha kiangazi na bwawa la kuchujia maji lililopo kata ya matogoro katika manispaa ya Songea kwenye maadhimisho ya wiki ya maji.
Alisema kuwa taasisi za serikali zimekuwa tatizo kubwa kwenye ulipaji wa ankara za maji ambapo amezitaja tasisis ambazo zinaogngoza kwa madeni makubwa kuwa ni Hospitali ya Mkoa (HOMSO)ambayo hadi sasa inadaiwa kiasi cha sh. milioni 100 ikifuatiwa na taasisi ya jeshi la wananchi.
Hata hivyo amesema kuwa SOUWASA imejipanga kupita kwenye taasisi hizo na kuwapa muda wa wiki mbili wawe tayari wamekamilisha kulipa madeni yao ambayo wanadaiwa vinginevyo watasitisha huduma hiyo ya maji.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na maji taka Songea (SOUWASA) Injinia Fransis Kapongo amewataka wakazi wa manispaa ya Songea kuheshimu maeneo ya vyanzo vya maji na kuacha mara moja tabia za uchomaji moto kwenye maeneo hayo.
Alisema kuwa kwa kipindi cha mwaka jana na mwaka huu hali imekuwa mbaya kutokana na uharibifu wa mazingira kwenye maeneo ya vyanzo vya maji kwani zimekuwa za hali ya juu sana hasa uchomaji moto licha ya kuweka ulinzi shirikishi kwa wananchi wa maeneo husika lakini bado limekuwa ni tatizo.
“Unajuwa ndugu waandishi haya maeneo ya vyanzo vya maji watu walikuwa wanayatumia kwa kulima bustani ndogondogo lakini ulipoanzishwa mradi huu wa maji wananchi waliambiwa waache mara moja kulima kwenye vyanzo hivyo sasa inaonekana ni tatizo kwani hawajalipokea vizuri agizo hilo matokeo yake wamekuwa wakifanya hujuma ya kuchoma moto nyakati za usiku kwa makusudi”alisema Kapongo.
Injinia kapongo alieleza zaidi kuwa kwa sasa SOUWASA imejipanga kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji katika manispaa hiyo kwa kujenga bwawa kubwa lenye ukuta wa zege ambalo litasaidia kwa kiasi kikubwa kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji kipindi cha kiangazi kwani litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji meta za ujazo zaidi ya 12,800.
Hata hivyo amesema kuwa kwa sasa hali siyo mbaya sana kwani kiwango cha upatikanaji wa maji kipo kwa asilimia 60 ni baada ya mvua kuanza kunyesha ndio imefanya kupungua kwa makali ya upatikanaji wa maji na kwamba mvua za masika zitakapoendelea kunyesha hali itakuwa nzuri.
SOUWASA inawateja zaidi ya 12,000 waliounganishiwa mtandao wa maji safi na kwamba kwa hivi sasa kuna mpango mkubwa wa kupanda miti ambayo ni rafiki wa maji kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji licha ya kuwa kila mwaka zoezi la upandaji miti linakuwepo.
MWISHO.
Chapisha Maoni